Julai 23,2022; Jumamosi: Juma La 16 La Mwaka

Mt. Birgita, Mtawa

Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Yer. 7:1-11

Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema, “Simama langoni pa nyumba ya Bwana, ukatangaze hapo neno hili, ukisema, Sikilizeni neno la Bwana, ninyi nyote wa Yuda, mnaoingia katika malango haya ili kumwabudu Bwana. Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli,” asema hivi, tengenezeni njia zenu, na matendo yenu, nami nitawakalisha ninyi mahali hapa. Msitumainie maneno ya uongo, mkisema, ‘Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana ndiyo haya!’ Maana kama mkitengeneza kabisa njia zenu na matendo yenu; kama mkihukumu hukumu ya haki kati ya mtu na jirani yake; kama hamwonei mgeni wala yatima, wala mjane, wala kumwaga damu isiyo na hatia mahali hapa, wala kuifuata miungu mingine kwa hasara yenu wenyewe; ndipo nitakapowakalisha mahali hapa, katika nchi hii niliyowapa baba zenu, tokea zamani hata milele. Angalieni, mnatumainia maneno ya uongo, yasiyoweza kufaidia. Je! Mtaiba, na kuua, na kuzini, na kuapa kwa uongo, na kumfukuzia Baali uvumba, na kuifuata miungu mingine ambayo hamkuijua; kisha mtakuja na kusimama mbele zangu katika nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, na kusema, tumepona; ili mpate kufanya machukizo hayo yote? Je! Nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, imekuwa pango la wanyang’anyi machoni penu? Angalieni, mimi, naam, mimi, nimeliona jambo hili, asema Bwana.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 84:2-5, 7, 10

 1. Nafsi yangu imezionea shauku nyua za Bwana,
  Naam na kuzikondea.
  Moyo wangu na mwili wangu,
  Vinamlilia Mungu aliye hai.

(K) Maskani zako zapendeza kama nini,
ee Bwana wa majeshi.

 1. Shomoro naye ameona nyumba,
  Na mbayuwayu amejipatia kioto,
  Alipoweka makinda yake.
  Kwenye madhabahu zako, ee Bwana wa majeshi,
  Mfalme wangu na Mungu wangu. (K)
 2. Heri wakaao nyumbani mwako
  Wanakuhimidi daima.
  Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako,
  Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake. (K)
 3. Huendelea toka nguvu hata nguvu,
  Huonekana Sayuni kila mmoja mbele za Mungu.
  Hakika siku moja katika nyua zako
  Ni bora kuliko siku elfu.
  Ningependa kuwa awabu
  Nyumbani mwa Mungu wangu,
  Kuliko kukaa hema za uovu. (K)

INJILI: Mt. 13:24-30

Yesu aliwatolea makutano mfano akisema, “Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, ‘Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu?’ Akawaambia, ‘Adui ndiye aliyetenda hivi.’ Watumwa wakamwambia, ‘Basi, wataka twende tukayakusanye?’ Akasema, ‘La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.’”

TAFAKARI
MATENDO YETU YANATENGENEZA KESHO YETU: Waswahili wana msemo usemao “matendo husema zaidi kuliko maneno”. Katika somo la kwanza tunamuona Nabii Yeremia akipewa ujumbe mzito na Mungu kuwapelekea wana wa Yuda. Ujumbe huu unahusu mkataba kati yao na Mungu juu ya makazi aliyowapa baba zao tangu zamani na kwa milele. Mwenyezi Mungu anachohitaji kutoka kwao ni kwanza kuwa na uhusiano mzuri na wa kimapendo na jirani; “na pili uhusiano kati yao na Mungu. Mkataba huu ni kwa faida yao wala si ya Mungu, kwani ni binadamu anayehitaji msaada kutoka kwa Mungu na kwa binadamu mwenzake, tena kwa kuweka utaratibu wa mmoja kutoonewa, kunawafanya wote wawe sawa na wasaidiane hasa wakati wa shida au mahitaji ya pekee. Mkataba huu ambao Mungu aliuweka na wana wa Yuda, ndio huo huo anauweka nasi leo. Tutambue kuwa matendo yetu kwa jirani na kwa Mungu ndiyo yatakayotufanya tudumu katika nyumba yake milele au tuangamie milele. Tusisahau kuwa Mungu kwa busara yake hatukatilii mbali kutokana na maovu yetu, anatuacha tu ili tukiamua kubadilika tubadilike mara, la hatupo tayari basi tusubiri siku ya mavuno.

SALA: Mungu Mwenyezi, tunakuomba utusaidie tuweze kudumu katika nyumba yako, Amina.