Julai 22,2022; Ijumaa: Juma La 16 La Mwaka

Mt. Maria Magdalena
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Yer. 3:14-17

“Rudini, enyi watoto wenye kuasi,” asema Bwana; “maana mimi ni mume wenu; nami nitatwaa mtu mmoja wa mji mmoja, na wawili wa jamaa moja, nami nitawaleta hata Sayuni; nami nitawapa ninyi wachungaji wanipendezao moyo wangu, watakaowalisha kwa maarifa na fahamu. Kisha itakuwa, mtakapoongezeka na kuwa wengi katika nchi hiyo,” asema Bwana, “siku zile hawatasema tena, Sanduku la agano la Bwana; wala halitaingia moyoni; wala hawatalikumbuka, wala hawatalizuru, wala hayatafanyika hayo tena. Wakati ule watauita Yerusalemu kiti cha enzi cha Bwana; na mataifa yote watakusanyika huko Yerusalemu, kwa ajili ya jina la Bwana; wala hawatakwenda tena kwa ukaidi wa moyo wao mbaya.”

Wimbo Wa Katikati: Yer. 31:10-13

 1. Lisikieni neno la Bwana, enyi mataifa,
  Litangazeni visiwani mbali,
  mkaseme: aliyemtawanya Israeli atamkusanya,
  na kumlinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.

(K) Bwana anatulinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.

 1. Kwa maana Bwana amemweka huru Yakobo,
  amemkomboa mkononi mwake aliyekuwa Hodari kuliko yeye.
  Nao watakuja na kuimba katika mlima Sayuni,
  wataukimbilia wema wa Bwana, nafaka na divai,
  na mafuta, na wachanga wa kondoo na wa ng’ombe. (K)
 2. Ndipo bikira atafurahi katika kucheza,
  na vijana na wazee pamoja,
  maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha,
  nami nitawafariji
  na kuwafurahisha waache huzuni yao. (K)

INJILI: Mt. 13:18-23

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ninyi sikilizeni mfano wa mpanzi. Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia. Naye aliyepandwa penye miamba, huyo ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha; lakini hana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara huchukizwa. Naye aliyepandwa penye miiba, huyo ndiye alisikiaye lile neno; na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno; likawa halizai. Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kuelewa nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini.

TAFAKARI
TU UDONGO GANI? Bwana wetu Yesu Kristo katoa ufafanuzi mzuri sana juu ya aina ya udongo ambao mpanzi alipanda mbegu zake. Ni wakati mzuri sasa mimi na wewe tuone ni katika udongo gani kila mmoja wetu yupo. Matendo yetu ndiyo yatakayotusaidia kujua mahali tulipo. Kama nimezoea kulisikia Neno juu juu tu nisilielewe vizuri, basi nitambue wazi kuwa mi ni udongo ulio karibu na njia. Tulio wengi tunaweza kuangukia kwenye udongo wenye miamba na wenye miiba. Angalia namna tulivyolipokea Neno kwa furaha kubwa hasa tulipokuwa vijana wadogo, leo hii tupo wapi? Nini kimetufanya tuliache Neno? Fikiria tunavyohangaika na mambo ya dunia hii. Tunakuwa na shughuli nyingi hadi Jumapili iliyo siku rasmi ya Bwana. Mara ngapi wazazi wameishia kuwakumbusha watoto kwenda kusali wakati wenyewe wanaenda kwenye shughuli nyingine. Nabii Yeremia leo anatuita akisema, “Rudini, enyi watoto wenye kuasi”. Anataka tugeuke sasa na kuwa udongo mzuri ili tuweze kuzaa mengi.

SALA: Ee Mungu twakuomba utusamehe kwa kutokuwa udongo mzuri. Amina.