Julai 18,2022; Jumatatu: Juma La 16 La Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Mik. 6:1-4, 6-8

Sikieni asemavyo Bwana; “Simama, ujitetee mbele ya milima, vilima navyo na visikie sauti yako. Sikieni, enyi milima, mateto ya Bwana, na ninyi, enyi misingi ya dunia iliyo imara; kwa maana Bwana ana mateto na watu wake, naye atahujiana na Israeli. Enyi watu wangu, nimewatenda nini? Nami nimewachosha kwa habari gani? Shuhudieni juu yangu. Kwa maana nalikupandisha kutoka nchi ya Misri, na kukukomboa utoke katika nyumba ya utumwa, nami naliwapeleka Musa, na Haruni, na Mariamu, watangulie mbele yako.” Nimkaribie Bwana na kitu gani, na kuinama mbele za Mungu aliye juu? Je! Nimkaribie na sadaka za kuteketezwa, na ndama za umri wa mwaka mmoja? Je! Bwana atapendezwa na elfu za kondoo waume, au na elfu kumi za mito ya mafuta? Je! Nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa kosa langu, mzao wa mwili wangu kwa dhambi ya roho yangu? Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!

Wimbo Wa Katikati: Zab. 50:5-6, 8-9, 16-17, 21, 23

  1. Nikusanyieni wacha Mungu wangu.
    waliofanya agano nami kwa dhabihu.
    Na mbingu zitatangaza haki yake,
    kwa maana Mungu ndiye hakimu.

(K) Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.

  1. Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako,
    na kafara zako ziko mbele zangu daima.
    Sitatwaa ng’ombe katika nyumba yako.
    wala beberu katika Mazizi yako. (K)
  2. Mtu asiye haki, Mungu amwambia,
    una nini wewe kuitangaza sheria yangu.
    Maana wewe umechukia maonyo,
    Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako. (K)
  3. Ndivyo ulivyofanya nami nikanyamaza,
    ukadhani ya kuwa mimi ni kama wewe.
    Atoaye dhabihu za kushukuru ndiye anayenitukuza,
    Nitamwonyesha wokovu wa Mungu. (K)

INJILI: Mt. 12:38-42

Baadhi ya waandishi wa Mafarisayo walimjibu Yesu wakasema, “Mwalimu, twataka kuona ishara kwako.” Akajibu, akawaambia, “Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona. Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi. Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, nao watawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona; na hapa yupo aliye mkuu kuliko Yona. Malkia wa kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka pande za mwisho za dunia ili asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani.”

TAFAKARI
JE, BADO TUNATAFUTA ISHARA? Historia au kumbukumbu ya matukio mbalimbali hutusaidia sana katika maisha yetu. Kupitia historia tunaweza kufahamu ni yapi mema na mazuri. Yesu katika mafundisho yake, alitumia historia kuwafundisha watu ili kumrudia Mungu. Leo anaeleza namna watu wa wakati wa Yona walivyoyapokea mafundisho ya Nabii Yona na kutubu. Sisi wa leo tunatafuta ishara? Hivi tumeshasahau namna Mwenyezi Mungu alivyotunusuru na janga la UVIKO19 (COVID19)? Kama si Mungu ni nani basi? Hata hili halitoshi kutusaidia kukua kiimani kuwa kweli Mungu yupo na anatupigania? Tukumbuke kuwa ishara kubwa tunayopaswa kuikumbuka ni ishara ya mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Tuungane na Nabii Mika anayetutaka tubadilike, na mabadiliko ya kweli yatatokana na kutenda haki, kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako! Tuamue sasa kumkimbilia Mungu hasa katika upungufu wetu wa imani.

SALA: Ee Baba Mungu, tunakushukuru kwa zawadi ya mwanao aliye ishara tosha ya wokovu wetu, Amina.