Jul 17,2022; Jumapili: Jumapili Ya 16 Ya Mwaka

SOMO 1: Mwa. 18:1-10a

Bwana alimtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari. Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi, akasema, “Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako. Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu. Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, iwapo mmemjia mtumwa wenu.” Wakasema, “Haya, fanya kama ulivyosema.” Basi Ibrahimu akaenda hima hemani kwa Sara, akasema, “Himiza vipimo vitatu vya unga safi, uukande, ufanye mikate.” Ibrahimu akapiga mbio kwenda kundini, akaleta ndama wa ng’ombe aliye laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akahimiza kuiandaa. Akatwaa siagi na maziwa, na ndama aliyoiandaa, akawaandikia mbele yao, akasimama karibu nao chini ya mti, nao wakala. Wakamwambia, “Yu wapi Sara mkeo?” Akasema, “Yumo hemani.” Akamwambia, “Hakika nitakurudia wakati uu huu mwakani. Na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 15

 1. Bwana, ni nani atakayefanya maskani yake
  Katika kilima chako kitakatifu?
  Ni yeye aendaye kwa ukamilifu,
  Na kutenda haki;
  Asemaye kweli kwa moyo wake,
  Asiyesingizia kwa ulimi wake.

(K) Bwana, ni nani atakayekaa katika hema yako.

 1. Yeye ambaye hakumtenda mwenziwe mabaya,
  Wala hakumsengenya jirani yake.
  Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa,
  Bali huwaheshimu wamchao Bwana. (K)
 2. Yeye ambaye hakutoa fedha yake apate kula riba,
  Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia.
  Mtu atendaye mambo hayo
  Hataondoshwa milele. (K)

SOMO 2: Kol. 1:24-28

Nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu; tena nayatimiliza katika mwili wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani, kanisa lake, ambalo nimefanywa mhudumu wake, sawasawa na uwakili wa Mungu, niliopewa kwa faida yenu, nilitimize neno la Mungu; siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake; ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa, nao ni Kristo ndani yenu; tumaini la utukufu; ambaye sisi tunamhubiri habari zake, tukimwonya kila mtu, na kumfundisha kila mtu katika hekima yote, tupate kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo.

SHANGILIO: Yn. 14:23

Aleluya, aleluya,
Mtu akinipenda, atalishika neno langu;
Na Baba yangu atampenda;
Nasi tutakuja kwake.
Aleluya.
INJILI : Lk. 10:38-42

Ikawa katika kuenenda kwao Yesu aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake. Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake. Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, “Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie.” Bwana akajibu akamwambia, “Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.”

TAFAKARI
TUSIDANGANYIKE, MUNGU YUPO KATIKA WATU: Katika Injili tunamwona Yesu nyumbani mwa Lazaro, Martha na Maria. Yesu, Mungu na mtu, aliitembelea familia yenye kipato cha kawaida. Kwa kuwa wenyeji walimwona Yesu kama mwanadamu mwengine, walijitahidi kutafuta chochote kukidhi njaa na kiu yake. Martha aliwaka sana katika hilo. Ni fadhila yenye thamani kubwa sana, ukarimu. Kinyume na Martha, Maria alikaa kumsikiliza mgeni. Jambo hili nalo ni muhimu kwa mgeni. Wayahudi walithamini wageni, sawia na watu wa mataifa yote. Imekuwa hivyo mpaka hivi karibuni uchoyo ulipopanda chati. Biblia ina nukuu na maelezo mengi kuhusiana na ukarimu kwa wageni (rejea Law 19:33-34, Isa 58:7, Mt 25:42-46, Lk 14:7-14, Mdo 16:33-34, 1Tim 5:10, Tit 1:8, Ebr 13:1, 1Pet 4:8-9, 3Yoh 1:5 na kadhalika).
Tukio la Bethani linavuta hisia zetu kwa namna yake. Katika kumkirimu mgeni Yesu, Yesu alitoa mapya. Alitaja anachohitaji zaidi kwa kuwa yeye alikuwa zaidi ya mgeni. Angeweza kuwaambia kwamba yeye ni Mungu-Mtu na hivyo anatembea na ujumbe wa kimungu kwa mustakabali wa wanadamu wote. Hivyo ilifaa akikutana na watu, watu watafute kwake ujumbe maana hayo ya kula na kunywa yapo daima. Yesu alisema kuwa Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa. Kifupi, aliwaomba akina dada wale wawili wamwone Mungu katika yeye na mkutano na Mungu uishie kwenye kujipatia ujumbe zaidi kuliko kukirimu chakula na chakunywa.
Somo la kwanza lina mfano mzuri sana wa mkutano wa binadamu na Mungu unaoishia katika baraka kubwa. Abrahamu aliwaona wageni watatu aliowapigia mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema. Aliwakaribisha kwa furaha na ukarimu. Wageni wale walikubali. Abrahamu akaenda kwa hema kumhimiza mkewe watayarishie chakula haraka. Mwishoni mwa ukarimu huu wa kibinadamu, Abrahamu alishangaa kupata kitu bora zaidi kutoka kwa wageni wake. Pasipo kuelewa vyema alikutana na Mungu aliyejificha ndani ya wale aliwaona kama wanadamu wa kawaida tu.
Somo la pili linaeleza kwamba mambo mengine ya Mungu yamefichika hata hivyo Mungu huweza kuwatumia watu kuyafichua hadharani kwa manufaa ya Kanisa na ulimwengu mzima. Mtume Paulo anajitolea mfano mwenyewe kwamba yeye amefanywa mmoja wa hao waliopewa kazi ya kuyafunua ya Mungu. Ndipo anasema ni kwa ajili ya mwili wake, yaani, kanisa lake, amefanywa mhudumu wake, sawasawa na uwakili wa Mungu, aliopewa kwa faida ya wanadamu, alitimize neno la Mungu. Mwishowe Paulo anataja lengo la shughuli hiyo yote, ndiyo kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo.
Tukijumlisha tunaweza kusema kuwa ni ukweli wa kwamba Mungu amejificha katika watu tunaokutana nao, katika maisha yetu ya kila siku. Zawadi ya kuwakaribisha wageni ina masafa marefu. Kama hatutapata hapa duniani, basi ni lazima tuipate mbinguni maana Mungu amesema chochote tutakachomfanyia mgeni au kumpa mgeni au mwenye dhiki hatakisahau (Mt 10:42). Ndiyo maana kuwakaribisha wageni (ukarimu) ni moja ya matendo saba ya huruma ya kimwili yatakayompatia mwanadamu uzima wa milele (Mt 25: 42-46).
Tatizo kubwa linalotufanya tusipate baraka za wageni ni kule kufumbika kwetu machoni kwamba wageni hawa ni wenzetu wa kawaida. Hima tulikabili tatizo hili kusudi tupanue wigo wa kumwona Mungu katika wageni na wenzetu.

SALA: Ee Mungu Mwenyezi, unayetutembelea mara kwa mara katika wageni, itengeneze mioyo yetu kiasi hiki tuwe radhi na wepesi kukupokea katika kujificha kwako. Amina.