Bikira Maria Mt. wa Mlima Karmeli
Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Mik. 2:1-5
Ole wao wakusudiao mambo maovu, na kutenda mabaya vitandani mwao! Kunapopambazuka asubuhi huyafanya, kwa sababu ya katika uwezo wa mikono yao. Nao hutamani mashamba, na kuyashika; na nyumba pia, nao huzichukua; nao humwonea mtu na nyumba yake, naam, mtu na urithi wake. Basi Bwana asema hivi, “Angalia, nakusudia jambo baya juu ya jamaa hii, ambalo hamtazitoa shingo zenu, wala hamtakwenda kwa kiburi; kwa maana ni wakati mbaya. Siku hiyo watatunga mithali juu yenu, na kuomboleza kwa maombolezo ya huzuni nyingi, na kusema, ‘Sisi tumenyang’anyiwa kabisa; yeye analibadili fungu la watu wangu; jinsi anavyoniondolea hilo! Awagawia waasi mashamba yetu. Kwa hiyo hutakuwa na mtu atakayeitupa kamba kwa kura katika mkutano wa Bwana.’”
Wimbo Wa Katikati: Zab. 10:1-4, 7-8, 14
- Ee Bwana, kwa nini wasimama mbali?
Kwani kujificha nyakati za shida?
Kwa kiburi chake asiye haki
Mnyonge anafuatiwa kwa ukali;
Na wanaswe kwa hila zizo hizo walizoziwaza.
(K) Usiwasahau wanyonge, ee Bwana.
- Maana mdhalimu hujisifia tamaa ya nafsi yake,
Na mwenye choyo humkana Bwana na kumdharau.
Mdhalimu kwa kiburi cha uso wake
Aseme, Hatapatiliza.
Jumla ya mawazo yake ni, Hakuna Mungu. (K) - Kinywa chake kimejaa laana,
Na hila na dhuluma.
Chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu,
Hukaa katika maoteo ya vijiji.
Mahali pa siri humwua asiye na hatia,
Macho yake humvizia mtu duni. (K) - Umeona, maana unaangalia madhara na jeuri,
Uyatwae mkononi mwako.
Mtu duni hukuachia nafsi yake,
Maana umekuwa msaidizi wa yatima. (K)
INJILI: Mt. 12:14-21
Mafarisayo walitoka wakafanya shauri juu ya Yesu jinsi ya kumwangamiza. Naye Yesu hali akiyafahamu hayo akaondoka huko; na watu wengi wakamfuata; akawaponya wote, akawakataza wasimdhihirishe; ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, “Tazama, mtumishi wangu niliyemteua; mpendwa wangu, moyo wangu uliyependezwa naye; nitatia roho yangu juu yake, naye atawatangazia Mataifa hukumu. Hatateta wala hatapaza sauti yake; wala mtu hatasikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima, hata ailetapo hukumu ikashinda. Na jina lake Mataifa watalitumainia.”
TAFAKARI
NIA MBAYA KATU HAZIKUBALIKI NA MUNGU: Mwanadamu ni kiumbe wa ajabu sana. Wakati mwingine tukiwaza, tunaweza tukajiuliza; hivi hii sura na mfano wa Mungu alivyoviweka ndani yetu vimepotelea wapi? Tukijua wazi kuwa Mungu ni upendo, hivyo kwa kuumbwa kwa sura na mfano wake lazima nasi tuna hali ya upendo ndani yetu. Je, uhalisia wa maisha yetu unaonekana hivyo? Kuna tofauti gani kati yangu Mkatoliki na asiyemjua Mungu mintarafu maisha ya upendo, amani na haki? Katika somo la kwanza, tumesikia habari za watu waniao maovu. Nabii Mika anaeleza juu ya nia mbaya aliyonayo mtu moyoni mwake na baadaye anaitekeleza bila kuogopa. Anasahau kuwa mwisho wake ni hukumu kutoka kwa Mungu. Kama hiyo haitoshi, katika Injili tuunasikia habari za Mafarisayo wanaopanga kumwangamiza Yesu. Ukiwauliza kawakosea nini, hawajui sababu. Je, sisi tumepanga kutenda nini? Je, tuyawazayo yanaendana na mapenzi ya Mungu? Je, mawazo na matendo yetu yanaendana na sura na mfano wa Mungu tulionao? Tumuombe Mungu atusaidie kutenda sawasawa na mapenzi yake.
SALA: Mungu mwema, tunakuomba utusaidie tuyawaze yale tu yakupendezayo, Amina.