Julai 15,2022; Ijumaa: Juma la 15 la Mwaka

Bonaventura, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Isa. 38:1-6, 21-22, 7-8

Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, “Bwana asema hivi, ‘Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona.’” Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana, akasema, “Ee Bwana, kumbuka haya, nakusihi kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako.” Hezekia akalia sana sana. Kisha neno la Bwana likamjia Isaya, kusema, “Enenda ukamwambie Hezekia, Bwana, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, ‘Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano. Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu.’” Basi Isaya akasema, “Na watwae mkate wa tini, wakauweke juu ya jipu, naye atapona.” Tena Hezekia alikuwa amesema, “Iko ishara gani ya kunionyesha ya kuwa nitapanda niingie nyumbani mwa Bwana?” “Jambo hili liwe ishara kwako, itokayo kwa Bwana, ya kuwa Bwana atalitimiza jambo hili alilolisema; Tazama, nitakirudisha nyuma kivuli madaraja kumi, ambayo kilishuka juu ya duara ya Ahazi kwa sababu ya jua.” Basi jua likarudi madaraja kumi katika hiyo duara, ambayo limekwisha kushuka.

Wimbo Wa Katikati: Isa. 38:10-12, 16

 1. Nalisema, katika usitawi wa siku zangu
  Nitakwenda kuingia malango ya kuzimu;
  Nimenyimwa mabaki ya miaka yangu. (K) Umeniokoa na shimo la uharibifu, ee Bwana.
 2. Nalisema, sitamwona Bwana, yeye Bwana,
  Katika nchi ya walio hai;
  Sitamwona mwanadamu tena pamoja na hao
  wakaao duniani. (K)
 3. Kao langu limeondolewa kabisa,
  Limechukuliwa kama hema ya mchungaji;
  Nimekunja Maisha yangu kama mfumaji.
  Atanikatilia mbali na kitanda cha mfumi;
  Tangu mchana hata usiku wanimaliza. (K)
 4. Ee Bwana kwa mambo hayo watu huishi;
  Na uhai wa roho yangu u katika hayo yote;
  Kwa hiyo uniponye na kunihuisha. (K)

INJILI: Mt. 12:1-8

Wakati ule Yesu alipita katika mashamba siku ya sabato; wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kuvunja masuke, wakala, na Mafarisayo walipoona, walimwambia, “Tazama! Wanafunzi wako wanafanya neno ambalo si halali kulifanya siku ya sabato.” Akawaambia, “Hamkusoma alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenziwe? Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaila mikate ile ya wonyesho, ambayo si halali kwake kuila wala kwa wale wenziwe, ila kwa makuhani peke yao? Wala hamkusoma katika torati, kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato wasipate hatia?” Lakini nawaambieni, “Kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu. Lakini kama mngalijua maana yake maneno haya, ‘Nataka rehema, wala si sadaka,’ msingaliwalaumu wasio na hatia. Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.”

TAFAKARI
NIA NJEMA NA MATENDO SAFI HULETA HURUMA NA MSAMAHA WA MUNGU: Kanisa katika mafundisho yake, hutualika mara zote tuwe na nia njema kwa Mungu na kwa binadamu wenzetu, na tuitimize nia hiyo kwa kutenda matendo mema yampendezayo Mungu. Katika somo la kwanza, tunamuona Hezekieli yuko taabani kwa ugonjwa na nabii Isaya anamweleza wazi juu ya kifo chake. Taarifa hii mbaya kwa Hezekieli haimfanyi akate tamaa bali kwake unakuwa wasaa wa kumuomba Mungu kwa dhati na hasa akimweleza mema mengi aliyoyatenda. Ndipo Mwenyezi Mungu kwa huruma na upendo mkubwa, anaongeza siku zake za kuishi. Katika Injili, tunaelezwa jinsi wanafunzi wa Yesu walivyowakera Mafarisayo walipokula masuke ya ngano. Yesu haangalii tu sheria bali nia yao njema, kwani sheria si ya kuwakandamiza watu bali ni ya kuwaokoa. Wapendwa katika Kristo, tutambue kuwa matendo mema hutuweka salama na kutusaidia kujitetea mbele ya Mungu. Hutufanya tukubalike na Baba na kwa kweli hutuongezea siku zetu za kuishi. Basi tujibidiishe kutenda mema na kusali daima.

SALA: Ee Mungu mwema, ututie nguvu ya kukutumikia kwa kutenda matendo yakupendezayo, Amina.