Julai 14,2022; Alhamisi: Juma la 15 la Mwaka

Mt. Kamili wa Lellis, Padre
Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Isa. 26:7-9, 12, 16-19

Njia yake mwenye haki ni unyofu; wewe uliye mnyofu wainyosha njia ya mwenye haki. Naam, katika njia ya hukumu zako sisi tumekungoja, ee bwana; shauku ya nafsi zetu inaelekea jina lako na ukumbusho wako. Kwa nafsi yangu nimekutamani wakati wa usiku; naam, kwa nafsi yangu ndani yangu nitakutafuta mapema; maana hukumu zako zikiwapo duniani, watu wakaao duniani hujifunza haki. Bwana, utatuamuria amani; maana ni wewe pia uliyetutendea kazi zetu zote. Bwana, katika taabu zao walikwenda kwako; waliomba maombi mengi wakati adhabu yako ilipokuwa juu yao. Kama vile mwanamke mwenye mimba anayekaribia wakati wake wa kuzaa, alivyo na utungu na kulia kwa sababu ya maumivu yake, ndivyo tulivyokuwa sisi mbele zako, ee Bwana. Tumekuwa na mimba, tumekuwa na utungu, tumekuwa kana kwamba tumezaa upepo; hatukufanya wokovu wo wote duniani, wala hawakuanguka wakaao duniani. Wafu wako wataishi, maiti zangu zitafufuka; amkeni, kaimbeni, ninyi mnaokaa mavumbini, kwa maana umande wako ni kama umande wa mimea, nayo ardhi itawatoa waliokufa.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 102:12-20

 1. Wewe, Bwana, utaketi ukimiliki milele,
  Na kumbukumbu lako kizazi hata kizazi.
  Wewe mwenyewe utasimama,
  Na kuirehemu Sayuni,
  Kwa maana ndio wakati wa kuihurumia,
  Naam, majira yaliyoamriwa yamewadia.
  Maana watumishi wake wameyaridhia mawe yake,
  Na kuyaonea huruma mavumbi yake.

(K) Toka mbinguni Bwana ameangalia nchi.

 1. Kisha mataifa wataliogopa jina la Bwana,
  Na wafalme wote wa dunia utukufu wake.
  Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni,
  atakapooneka katika utukufu wake.
  Atakapoyaelekea maombi yake aliye mkiwa,
  Asiyadharau maombi yao. (K)
 2. Kizazi kitakachokuja kitaandika hayo,
  na watu watakaoumbwa watamsifu Bwana.
  Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu,
  toka mbinguni Bwana ameangalia nchi.
  Ili akusikie kuugua kwake yeye aliyefungwa,
  na kuwafungua waliondikiwa kufa. (K)

INJILI: Mt. 11:28-30

Yesu aliwaambia makutano: “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”

TAFAKARI
NJONI KWANGU, NINYI NYOTE MSUMBUKAO: Mungu baba yetu ni mwenye huruma, upendo na haki. Sifa hizi zinatufanya sisi binadamu kumtafuta Mungu kwa nguvu zote ili tuweze kupata mahitaji yetu. Kama tunavyoambiwa na Nabii Isaya katika somo la leo, “Kwa nafsi yangu nimekutamani wakati wa usiku; naam, kwa nafsi yangu ndani yangu nitakutafuta mapema”. Tunakuwa na faraja pale tunapoona kuwa Mungu yu nasi daima na kwake tunapata usalama na amani. Lakini tutambue kuwa kwa kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, nasi tunaweza kutenda mema, kutetea haki na kuwa mabalozi wa amani. Kazi hii yawezekana kwa mtu mwenye imani na upendo kwa Mungu na jirani. Pia lazima tuwe tayari kupitia changamoto. Ndio maana Yesu, katika mazingira hayo anatutaka tusihangaike bali tumwendee yeye pale asemapo, “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha”. Si kwamba kwake tutapata raha tupu bali tutapewa nguvu ya kuibeba mizigo yetu yote.

SALA: Ee Mungu mwema, ni kwako tu tunapata pumziko, Amina.