Mt. Henri
Nyeupe
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Isa. 10:5-7, 13-16
Bwana asema hivi: Ole wake Ashuru! Fimbo ya hasira yangu, ambayo gongo lililo mkononi mwake ni ghadhabu yangu! Nitamtuma juu ya taifa lenye kukufuru, nitampa maagizo juu ya watu wa ghadhabu yangu, ateke nyara, na kuchukua mateka, na kuwakanyaga kama matope ya njiani. Lakini hivyo sivyo akusudiavyo mwenyewe, wala sivyo moyo wake uwazavyo; maana katika moyo wake akusudia kuharibu, na kukatilia mbali mataifa, wala si mataifa machache. Kwa maana amesema, “Kwa nguvu za mkono wangu nimetenda jambo hili, na kwa hekima yangu; maana mimi nina busara; nami nimeiondoa mipaka ya watu, nikaziteka akiba zao, nikawaangusha waketio juu ya viti vya enzi kama afanyavyo shujaa. Na mkono wangu umezitoa mali za mataifa kama katika kioto cha ndege; na kama vile watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa, ndivyo nilivyokusanya dunia yote; wala hapana aliyetikisa bawa, wala kufum”bua kinywa, wala kulia. Je! Shoka lijisifu juu yake alitumiaye? Je! Msumeno ujitukuze juu yake auvutaye? Ingekuwa kana kwamba bakora ingewatikisa waiinuao, au fimbo ingemwinua yeye ambaye si mti. Kwa hiyo Bwana, Bwana wa majeshi, atawapelekea kukonda watu wake walionona; na badala ya utukufu wake kutawashwa kuteketea kama kuteketea kwa moto.”
Wimbo Wa Katikati: Zab. 94:5-10, 14-15
- Ee Bwana wanawaseta watu wako;
Wanauseta urithi wako;
Wanamwua mjane na mgeni;
Wanawafisha yatima.
(K) Bwana hatawatupa watu wake.
- Nao husema Bwana haoni;
Mungu wa Yakobo hafikiri.
Enyi wajinga miongoni mwa watu fikirini;
Enyi wapumbavu, lini mtakapopata akili? (K) - Aliyelitia sikio mahali pake asisikie?
Aliyelifanya jicho asione?
Awaadibuye mataifa asikemee?
Amfundishaye mwanadamu asijue? (K) - Kwa kuwa Bwana hatawatupanwatu wake.
Wala hatauacha urithi wake,
Maana hukumu itairejea haki,
Na wote walio wanyofu wa moyo wataifuata. (K)
INJILI: Mt. 11:25-27
Wakati ule Yesu alijibu akasema, “Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako.” Akasema, “Nimekabidhiwa vyote na baba yangu; wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia.”
TAFAKARI
TUSHUKURU KWA KILA JAMBO: Bwana wetu Yesu Kristo leo anatoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kutokana na mambo mengi aliyoyatenda. Kwa namna ya pekee katika sehemu hii ya Injili ambayo ni mwishoni mwa sura ya 11, anamshukuru Mungu kwa kujulishwa siri za mbinguni. Siri ambazo wamefichwa watu wenye hekima na akili na kufunuliwa watoto wachanga. Yesu hana tatizo na wenye hekima ila anaona ndani yake hatari itokanayo na kiburi kitokanacho na kujiona una hekima na akili. Tumewaona wengi na hata sisi wenyewe, baada ya kupata nafasi fulani katika jamii tunajaa kiburi na kuwanyanyasa walioko chini yetu kama vile sisi ni miungu midogo. Kiburi kinatujaa hadi tunataka kuabudiwa. Ni lazima nafasi au vyeo tulivyokabidhiwa tutambue kuwa ni dhamana tuvitumie kwa ajili ya maslahi ya jamii nzima. Tukitaka kweli kuyajua mapenzi ya Mungu na siri zake, ni lazima tujiweke chini ya Kristo na kufuata mafundisho yake kama vile mtoto anavyokuwa mtiifu na mnyenyekevu kwa wazazi wake.
SALA: Mungu Baba yetu, tunaomba hekima yako ituongoze daima na tuwe na shukrani kwako, Amina.