Julai 12,2022 Jumanne: Juma la 15 la Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Isa. 7:1-9

Ilikuwa katika siku za Ahazi, mwana wa Yothamu, mwana wa Uzia, mfalme wa Yuda, Resini, mfalme wa Shamu, na Peka, mwana wa Remalia, mfalme wa Israeli, wakapanda wakaenda Yerusalemu ili kupigana nao, lakini hawakuweza kuushinda. Kisha watu wa nyumba ya Daudi wakaambiwa kwamba Shamu wamefanya mapatano na Efraimu. Na moyo wake ukataharuki, na moyo wa watu wake, kama miti ya mwituni itikiswayo na upepo. Basi Bwana akamwambia Isaya, “Haya, toka, umlaki Ahazi, wewe na Shear-yashubu mwana wako, huko mwisho wa mfereji wa birika la juu, katika njia kuu ya uwanja wa dobi; ukawaambie, ‘Angalia, ukatulie; usiogope wala usife moyo, kwa sababu ya mikia hii miwili ya vinga hivi vitokavyo moshi; kwa sababu ya hasira kali ya Resini na Shamu, na mwana wa Remalia. Kwa kuwa Shamu amekusudia mabaya juu yako, pamoja na Efraimu na mwana wa Remalia, wakisema, haya, na tupande ili kupigana na Yuda na kuwasumbua, tukabomoe mahali tupate kuingia, na kummilikisha mfalme ndani yake, huyo mwana wa Tabeeli.’” Bwana Mungu asema hivi, “Neno hili halitasimama wala halitakuwa. Kwa maana kichwa cha Shamu ni Dameski, na kichwa cha Dameski ni Resini; na katika muda wa miaka sitini na mitano Efraimu atavunjika vipande vipande, asiwe kabila ya watu tena; tena kichwa cha Efraimu ni Samaria, na kichwa cha Samaria ni mwana wa Remalia. Kwamba hamtaki kusadiki, bila shaka hamtathibitika.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 48:1-7

 1. Bwana ndiye aliye mkuu,
  Na mwenye kusifiwa sana
  Katika mji wa Mungu,
  Katika mlima wake mtakatifu.
  Kuinuka kwake ni mzuri sana,
  Ni furaha ya dunia yote.

(K) Mji wa Mungu wetu ataufanya imara hata milele.

 1. Mlima Sayuni pande za kaskazini,
  Mji wa Mfalme mkuu.
  Mungu katika majumba yake
  Amejijulisha kuwa ngome. (K)
 2. Maana, tazama,wafalme walikusanyika;
  Walipita wote pamoja.
  Waliona, mara wakashangaa;
  Wakafadhaika na kukimbia. (K)
 3. Papo hapo tetemeko liliwashika,
  Utungu kama wa mwanamke azaaye.
  Kwa upepo wa mashariki
  Wavunja jahazi za Tarshishi. (K)

INJILI: Mt. 11:20-24

Yesu alianza kuikemea miji ile ambamo ndani yake ilifanyika miujiza yake iliyo mingi, kwa sababu haikutubu. “Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu.” Walakini nawaambieni, “Itakuwa rahisi Taro na Sidoni kustahimili adhabu zao siku ya hukumu kuliko ninyi. Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa mpaka mbinguni? Utashushwa mpaka kuzimu; kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika katika Sodoma, ungalikuwapo mji huo hata leo.” Walakini nawaambieni, “Itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe.”

TAFAKARI
MIUJIZA YA YESU ITUBADILISHE: Miujiza mingi aliyoifanya Yesu ilikuwa na nia ya kuonyesha uwezo wa Mungu, na kuwafanya watu waamini na kubadili maisha yao yamwelekee Mungu. Lakini si wote walioiona miujiza hiyo waliamini au kubadilika. Wapo waliyoibeza kwa kusema anatumia nguvu za mkuu wa pepo (Mt. 22:24), na wapo walioiona na kuipuuzia. Leo katika Injili, Yesu anaongea kwa uchungu juu ya miji ya Korazini, Bethsaida na Kapernaumu kutokana na kutokuamini kwao. Walipata bahati ya kuona na kufanyiwa miujiza mingi, lakini hawakutubu bali waliendelea na maisha yao ya dhambi na kiburi kwa Mungu. Ama kweli kwenye miti hakuna wajenzi! Yawezekana ikawa rahisi sana kuwasema watu wa miji hii anayoisikitikia Yesu, hebu tujiulize? Tumeelezwa mengi juu ya Maandiko Matakatifu jinsi Mungu alivyowatendea wema na hata wabaya walivyokuwa. Tumesikia na kujifunza namna Yesu alivyowatendea wanadamu na ahadi kwa waliomfuata kwa uaminifu. Tena sisi wenyewe tumeona namna Mungu anavyotubariki, kutusaidia na kutusimamia katika mambo mengi. Je, haya yote yametusaidia kubadilika na kumuishi Kristo? Ni miujiza gani zaidi tunayotaka tutendewe ili tubadilike? Nasi tunaambiwa ole wetu!

SALA: Ee Yesu wangu mwema, Neno lako litusaidie kubadilika, Amina.