Julai 11,2022; Jumatatu: Juma la 15 la Mwaka

Mt. Benedikto, Abati
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Isa. 1:10-17

Lisikieni neno la Bwana, enyi waamuzi wa Sodoma; tegeni masikio msikie sheria ya Mungu wetu, enyi watu wa Gomora. Huu wingi wa sadaka zenu mnazonitolea una faida gani? Asema Bwana. Nimejaa mafuta ya kafara za kondoo waume, na mafuta ya wanyama walionona; nami siifurahi damu ya ng’ombe wala ya wana-kondoo wala ya mbuzi waume. Mjapo ili kuonekana mbele zangu, ni nani aliyetaka neno hili mikononi mwenu, kuzikanyaga nyua zangu? Msilete tena matoleo ya ubatili; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mpya na sabato, kuita makutano; siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada. Sikukuu zenu za mwezi mpya na karamu zenu za mwezi mpya na karamu zenu zilizoamriwa, nafsi yangu yazichukia; mambo hayo yanilemea; nimechoka kuyachukua. Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu. Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 50:8-9, 16-17, 21, 23

 1. Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako,
  Na kafara zako ziko mbele yangu daima.
  Sitatwaa ng’ombe katika nyumba yako,
  Wala bebeeru katika Mazizi yako.

(K) Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.

 1. Una nini wewe kuitangaza sheria yangu,
  Na kuliweka agano langu kinywani mwako?
  Maana wewe umechukia maonyo,
  Na kuyatupa maneno yangunyuma yako. (K)
 2. Ndivyo ulivyofanya, nami nitanyamaza,
  Ukadhani ya kuwa misri ni kama wewe.
  Atoaye dhabihu za kushukuru ndiye anayenitukuza,
  Nitamwonesha wokovu wa Mungu. (K)

INJILI: Mt. 10:34-11:1

Yesu aliwafundisha mitume wake: “Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja kuleta amani, bali upanga.. kwa maana nalikuja kumfitini mtu na babaye, na binti na mamaye, na mkwe na mkwe mtu; na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake. Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili. Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona. Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma. Ampokeaye nabii kwa kuwa ni nabii, atapata thawabu ya nabii; naye ampokeaye mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapata thawabu ya mwenye haki. Na mtu awaye yote atakayemnywesha mmojawapo wa wadogo hawa ngaa kikombe cha maji ya baridi, kwa kuwa ni mwanafunzi, amin, nawaambia, haitampotea kamwe thawabu yake. Ikawa Yesu alipokwisha kuwaagiza wanafunzi wake kumi na wawili, alitoka huko kwenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao.”

TAFAKARI
SADAKA NA MATENDO YETU LAZIMA VIENDANE: Wajibu wetu kwa Mungu kama binadamu, ni kumtolea sadaka. Tunafanya hivi kwa kuwa tunatambua kuwa vyote tulivyo navyo vimetoka kwake hata sisi wenyewe. Lakini tujiulize, tunapoenda mbele ya Mungu na kumtolea sadaka, mioyo yetu ipo safi? Kwa njia gani tumezipata sadaka hizo? Au tuko sawa tu na wenyeji wa Sodoma na Gomora ambao waliacha kutenda haki na huku wanamtolea Mungu sadaka? Tukiwa kama hao, Mwenyezi Mungu atatueleza wazi kuwa “Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema”. Zaidi na hayo, lazima kwanza tuwe tayari kuibeba misalaba ya maisha yetu na kumfuata Kristo. Kuibeba misalaba hiyo ni pamoja na kuwasaidia au kuwahudumia wahitaji kama wagonjwa, yatima, kuwa sauti ya wasio na sauti kwa kutetea haki zao na wala si kuwanyang’anya haki hizo. Tukijitoa wenyewe kwa ajili ya Kristo na wahitaji, na kumtolea sadaka safi Mwenyezi Mungu, tutabarikiwa na kufurahia mema yake.

SALA: Ee Mungu wetu, tukumbushe daima wajibu wetu wa kutenda haki kwa wengine, Amina.