Julai 10,2022; Jumapili: Jumapili ya 15 ya Mwaka

SOMO 1: Kumb. 30:10-14

Ukiwa utaifuata sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa kuyashika maagizo yake, na amri zake zilizoandikwa katika chuo hiki cha torati; ukimwelekea Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote. Kwa maana maagizo haya nikuagizayo leo, si mazito mno kwako, wala si mbali. Si mbinguni, hata useme, “”Ni nani atakayetupandia mbinguni akatuletee, aje atuambie tusikie, tupate kuyafanya?” Wala si ng’ambo ya pili ya bahari, hata useme, “Ni nani atakayetuvukia habari, akatuletee, aje atuambie, tusikie, tupate kuyafanya?” Lakini neno li karibu nawe sana, li katika kinywa chako na moyo wako, upate kulifanya.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 69:13, 16, 29-30, 32-33, 35-36

 1. Maombi yangu nakuomba Wewe, Bwana,
  Wakati ukupendezao; Ee Mungu,
  Kwa wingi wa fadhili zako unijibu.
  Katika kweli ya wokovu wako.
  Ee Bwana, unijibu, maana fadhili zako ni njema,
  Kwa kadiri ya rehema zako unielekee.

(K) Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.

 1. Nami niliye maskini na mtu wa huzuni.
  Mungu, wokovu wako utaniinua.
  Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo,
  Nami nitamtukuza kwa shukrani. (K)
 2. Walioonewa watakapoona watafurahi;
  Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.
  Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji.
  Wala hawadharau wafunga wake. (K)
 3. Maana Mungu ataiokoa Sayuni,
  Na kuijenga miji ya Yuda,
  Wazao wa watumishi wake watairithi,
  Nao walipendao jina lake watakaa humo. (K)

SOMO 2: Kol. 1:15-20

Kristo ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni viti vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye. Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote. Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake, akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni.

SHANGILIO: Mdo. 16:14
Aleluya, aleluya,
Fungua moyo wetu, Ee Bwana, ili tuyatunze maneno ya mwanao
Aleluya.

INJILI: Lk. 10:25-37
Siku ile, mwana-sheria mmoja alisimama amjaribu, akisema, “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Akamwambia, “Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje?” Akajibu akasema, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako.” Akamwambia, “Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi.” Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, “Na jirani yangu ni nani? Yesu” akajibu akasema, “Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa. Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipitia kando. Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapitia kando. Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, ‘Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa.’ Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake, yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi?” Akasema, “Ni huyo aliyemwonea huruma.” Yesu akamwambia, “Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.”

TAFAKARI
KUFANYA UBAYA NI KAZI NGUMU ZAIDI KULIKO KUTENDA WEMA: Wazo hili linadokezwa na Injili na linaungwa mkono sana na masomo mawili yanayoambatana nayo. Kulingana na Injili wanyang’anyi ni wabaya, waliamua kinyume cha dhamiri zao. Dhamiri ya mwanadamu humuhimiza kutenda mema. Hivi kuamua kumvamia mtu, kumvua nguo, kumtia jeraha na kumwacha karibu kufa vyote vyataka dhamiri au roho ngumu. Ndio maana mtu akifanya uovu, dhamiri humsuta kwani alichofanya ni kupingana na sauti nyororo ya kumhimiza afanye wema. Kisha akaja kuhani mkuu. Dhamiri yake ilimwambia amtendee mema mtu yule aliyelala akingoja kifo. Ili kufanya uovu wa kumwacha mhitaji katika dhiki yake ilimpasa ajidai kukumbuka makatazo mengi yaliyomhusu. Kwa kuwa alikuwa na jambo lake alilokuwa akienda kulifanya huko Yeriko, akakataa kuingia gharama. Aidha, alijidai kuwa mtu wa kujali muda. Wala hakujali chagizo mbalimbali kama “Tenda wema uende zako,” “Wema hauozi” na “Leo kwangu, kesho kwako”. Mlawi vivyo hivyo, alilazimika kujitafutia sababu. Kwa nini asimsaidie mhitaji yule kinyume na dhamiri yake?
Kinyume cha hao, yaani wanyang’anyi, kuhani na Mlawi, Msamaria mwema alibaki mwenyewe. Katika kutenda mema dhamiri na amri ya upendo. Kanuni yake ni rahisi, “Mtendee mwenzio yale ungalipenda utendewe mwenyewe.” Msamaria aliandamana na dhamira na moyo wake bila kujali kelele mbishi. Jambo hili lilimpeleka kwenye falsafa ya “Undugu kufaana na siyo kufanana” na “Leo kwangu, kesho kwako.” Baada ya kuisikiliza dhamiri yake na kumhurumia mhitaji yule, matendo laini yalifuata. Wema alioutenda hautaoza, unashuhudiwa na wote hata leo.
Somo la kwanza linaeleza tunayoyasema ya kwamba kutenda ubaya ni vigumu kuliko kutenda wema. Maelezo anayotupa Mungu, si mazito mno kwetu, na wala hayapo mbali; si ng’ambo ya pili ya bahari, bali yapo karibu nasi sana (katika vinywa vyetu na mioyo yetu, tupate kuyafanya). Ayasemayo Mungu, ndiyo yale tunayoambiana kuwa dhamiri ambayo ni sauti ya Mungu mwenyewe: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Kuzisikiliza dhamiri kumbe ni kumsikiliza Mungu mwenyewe. Laiti tungalielewa hivi!
Somo la pili linaeleza wepesi wa kutenda mema. Wepesi huu unatokana na kutambua na kumakinika kwetu kuhusu hoja kuwa tuna kaka mmoja, Yesu Kristo. Ndiye kichwa cha mwili, yaani, Kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, kusudi awe mtangulizi wetu katika yote. Nafasi hii muhimu Yesu aliipata kusudi katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; na yeye avipatanishe vitu vyote na nafsi yake, akiisha kufanya amani kwa damu yake msalabani. Kumbe, ushirikiano na mshikamano na Yesu ungelainisha utendaji wetu.
Tujumlishe kwa kusema inawezekana sana kutenda wema. Amri ya mapendo imeandikwa mioyoni mwetu.

SALA: Ee Mungu Mwenyezi, usiache kutuonyesha kwamba kutenda mema ni rahisi zaidi kuliko kujilazimisha kutenda uovu, kinyume cha dhamiri zetu kama wanadamu. Tusaidie kuziheshimu dhamiri zetu kwa maana ni sauti yako wewe mwenyewe, ee Mungu wetu. Amina.