Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Hos 14:2-9
Bwana anasema: Chukueni maneno pamoja nanyi, mkamrudie Bwana; mkamwambie, “Ondoa maovu yote, uyatakabali yaliyo mema; na hivyo ndivyo tutakavyotoa sadaka za midomo yetu kana kwamba ni ng’ombe. Ashuru hatatuokoa; hatutapanda farasi; wala hatutaiambia tena kazi ya mikono yetu, ninyi ndinyi miungu yetu; maana kwako wewe wasio na baba hupata rehema.” Mimi nitawaponya kurudi nyuma kwao; nitawapenda kwa ukunjufu wa moyo; kwa maana hasira yangu imemwacha. Nitakuwa kama umande kwa Israeli; naye atachanua maua kama nyinyoro, na kuieneza mizizi yake kama Lebanoni. Matawi yake yatatandaa, na uzuri wake utakuwa kama uzuri wa mzeituni, na harufu yake kama Lebanoni. Na wao wakaao chini ya uvuli wa wake watarejea; watafufuka kama ngano, na kuchanua maua kama mzabibu; harufu yake itakuwa kama harufu ya divai ya Lebanoni. Efraimu atasema, “Mimi nina nini tena na sanamu?” Mimi nimeitika, nami nitamwangalia. Mimi ni kama mberoshi wenye majani mabichi. Kwangu mimi nimepatikana matunda yako. Ni nani aliye na hekima, naye atayafahamu mambo haya? Ni nani aliye na busara, naye atayajua? Kwa maana njia za Bwana zimenyoka, nao wenye haki watakwenda katika njia hizo; bali waasio wataanguka ndani yake.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 51:1-2, 6-7, 10-11, 15
- Ee Mungu, unirehemu,
Sawasawa na Fadhili zako,
Uyafute makosa yangu.
Unioshe kabisa na uovu wangu,
Unitakase dhambi zangu.
(K) Ulimi wangu utaiimba haki yako.
- Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni,
Nawe utanijulisha hekima kwa siri,
Unisafishe kwa kwa hisopo nami nitakuwa safi,
Unioshe nami nitakuwa mweupe kuliko theluji. (K) - Ee Mungu, uniumbie Moyo safi,
Uifanye upya roho iiyotulia ndani yangu.
Usinitenge na uso wako,
Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. (K) - Ee Bwana, uifumbue midomo yangu,
Na kinywa changu kitazinena sifa zako. (K)
INJILI: Mt. 10:16-23
Yesu aliwaambia mitume wake, “Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa-mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua. Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu. Na ndugu atamsaliti nduguye ili auawe, na baba atamsaliti mwana, na wana watawainukia wazazi wao, na kuwafisha. Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Lakini watakapowafukuza katika mji huu, kimbilieni mwingine; kwa maana ni kweli nawaambia, Hamtaimaliza miji ya Israeli, hata ajapo Mwana wa Adamu.”
TAFAKARI
KUMUHUBIRI KRISTO YATAKA SADAKA: Bwana wetu Yesu Kristo alipowatuma mitume wake kwenda kulihubiri Neno la Mungu, alijua wazi kuwa watapata upinzani. Upinzani kutoka kwa viongozi wa Kiyahudi, viongozi wa serikali na hata ndugu zao wenyewe. Kwa kulitambua hilo, anawapa mbinu ya kutumia ili wasikate tamaa. Anawaeleza kuwa watumie busara na wawe wapole, wawe na uwezo wa kutambua hali halisi ya mazingira yalivyo na ikibidi basi wahamie sehemu nyingine. Na wala wasihofie juu ya lile watakalosema kwani watajaliwa na Mungu Roho Mtakatifu namna ya kujibu. Pamoja na mbinu hiyo, bado Mitume walipata taabu sana. Wengi waliuawa kwa kuwa waliithamini sana kazi waliyopewa hata hawakuona kuwa maisha yao ni ya maana zaidi ya Kristo. Mazingira ya wakati wa Mitume hayana tofauti sana na mazingira ya sasa. Bado watu wengi hawapendi kulisikia Neno la Mungu, bali wanaishi wapendavyo. Tunakumbushwa na Nabii Hosea, “Chukueni maneno pamoja nanyi, mkamrudie Bwana; mkamwambie, ‘Ondoa maovu yote, uyatakabali yaliyo mema.”’ Kamwe tusikatishwe tamaa na wasiompenda Mungu.
SALA: Ee Mungu, naomba unitie nguvu katika udhaifu wangu wa mwili na roho, Amina.