Mt. Antoni Maria Zakaria, Padre
Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Hos. 8:4-7, 11-13
Bwana asema hivi: “Wamesimamisha wafalme, lakini si kwa shauri langu; wamejifanyia wakuu, lakini nalikuwa sina habari; kwa fedha yao na dhahabu yao wamejifanyizia sanamu, kusudi wakatiliwe mbali. Amemtupa ndama yako, Ee Samaria! Hasira yangu imewaka juu yao; siku ngapi zitapita kabla ya hao kupata hali isiyo na hatia? Maana katika Israeli kimetokea hata na kitu hiki; fundi ndiye aliyekifanya, nacho si Mungu kamwe; naam, ndama ya Samaria itavunjika vipande vipande. Kwa maana wao hupanda upepo, nao watavuna tufani; nafaka haina bua; machipuko yake hayatoi masuke; hata ikiwa yatoa, wageni watayameza. Kwa kuwa Efraimu ameongeza madhabahu kwa dhambi, madhabahu zimekuwa dhambi kwake. Nijapomwandikia sheria yangu katika amri elfu kumi, zimehesabiwa kuwa ni kitu kigeni. Kwa habari za dhabihu za matoleo yangu, hutoa dhabihu ya nyama na kuila; lakini Bwana hawakubali; sasa ataukumbuka uovu wao, na kuwapatiliza dhambi zao; watarudi kwenda Misri.”
Wimbo Wa Katikati: Zab. 115:3-10
- Mungu wetu yuko mbinguni,
Alitakalo lote amelitenda.
Sanamu zao ni fedha na dhahabu,
Kazi ya mikono ya wanadamu.
(K) Enyi Israeli, mtumainini Bwana.
- Zina vinywa lakini hazisemi,
Zina macho lakini hazisomi,
Zina maskio lakini hazisikii,
Zina pua lakini haziskii harufu. (K) - Mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi,
Wala hazitoi sauti kwa koo zake
Wazifanyao watafanana nao,
Kila mmoja anayezitumainia. (K) - Enyi Israeli, mtumainini Bwana;
Yeye ni msaada wao na ngao yao;
Enyi mlango wa Haruni, mtumainini Bwana;
Yeye ni msaada wao na ngao yao. (K)
INJILI: Mt. 9:32-39
Walimletea Yesu mtu bubu mwenye pepo. Na pepo alipotolewa, yule bubu alinena, makutano wakastaajabu, wakasema, “Haijaonekana hivi katika Israeli wakati wowote.” Lakini Mafarisayo wakasema, “Kwa nguvu za mkuu wa pepo atoa pepo.” Naye Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, “Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake.”
TAFAKARI
KIBURI CHA MAOVU TUYATENDAYO KIMETOKA WAPI? Sisi binadamu ni viumbe tuliojawa na kiburi, matukano na nia mbaya kwa binadamu wenzetu hadi kwa Mungu wetu pia. Hiki ni kiburi cha ajabu. Nabii Hosea katika somo la kwanza anaonyesha uovu wa mwanadamu pale anaposema, “Wamesimamisha wafalme, lakini si kwa shauri langu; wamejifanyia wakuu, lakini nalikuwa sina habari”. Kama haitoshi, katika Injili, watu badala ya kufurahia na kumshukuru Mungu kwa kumponya mtu aliyepagawa na “pepo bubu”, wanadhihaki na kueleza kuwa nguvu za mkuu wa pepo ndizo zilizotumika. Kwa kiburi chetu nasi hatuko mbali na wenzetu waliotutangulia. Jema lolote likitendwa hasa na mtu tusiyemtaka tutasema tu; kabahatisha, hajatenda yeye, imetokea tu au si kawaida yake. Kwa nini tunakuwa wagumu kutambua uwezo na upendo wa Mungu kupitia kwa wenzetu? Tutambue kuwa jema lolote litendwalo, Mungu kahusika, na ovu lolote latokana na kiburi na uovu wa mwanadamu. Tukumbuke wajibu wetu wa kutenda mema daima.
SALA: Ee Mwenyezi Mungu, tunakuomba utuondolee kiburi chetu na hivi kuthamini mema unayotujalia. Amina.