Mt. Elisabeti, Malkia
Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO I: Hos. 2:14-16, 19-20
Bwana asema hivi, “Angalia, mimi nitamshawishi, na kumleta nyikani, na kusema naye maneno ya kumtuliza moyo. Naye ataniitikia huko, kama siku zile za ujana wake, na kama siku ile alipopanda kutoka nchi ya Misri. Tena siku hiyo itakuwa,” asema Bwana, “utaniita Ishi, wala hutaniita tena Baali. Nami nitakuposa uwe wangu kwa milele; naam, nitakuposa kwa haki, na kwa hukumu, na kwa ufadhili, na kwa rehema. Nami nitakuposa kwa uaminifu; nawe utamjua Bwana.”
Wimbo Wa Katikati: Zab. 145:1-2, 8-11, 14, 17
- Ee Bwana wangu, Mfalme, nitakutukuza,
Nilihimidi jina lako milele na milele.
Kila siku nitakuhimidi,
Nitalisifu jina lako milele na milele.
(K) Nitalihimidi jina lako milele na milele.
- Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma,
Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema.
Bwana ni mwema kwa watu wote,
Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote. - Ee Bwana,kazi zako zote zitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
Wataunena utukufu wa ufalme wako,
Na kuuhadithia uweza wako. (K) - Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,
Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote.
Bwana huwategemeza wote waangukao,
Huwainua wote walioinamia chini. (K)
INJILI: Mt. 9:18-26
Yesu alipokuwa akiwaambia hayo, tazama, akaja jumbe mmoja, akamsujudia, akisema, “Binti yangu sasa hivi amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi.” Akaondoka Yesu, akamfuata, pamoja na wanafunzi wake. Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake. Kwa maana alisema moyoni mwake, “Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona.” Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, “Jipe moyo mkuu, binti yangu, imani yako imekuponya.” Yule mwanamke akapona tangu saa ile. Yesu alipofika nyumbani kwa yule jumbe, aliona wapiga filimbi, na makutano wakifanya maombolezo, akawaambia, “Ondokeni; kwa maana kijana hakufa, amelala tu.” Wakamcheka sana. Lakini makutano walipoondoshwa, aliingia, akamshika mkono; yule kijana akasimama. Zikaenea habari hizi katika nchi ile yote.
TAFAKARI
IMANI KWA MUNGU HUPONYA NA KUTUWEKA KARIBU NAYE: Imani ni jambo la muhimu katika safari yetu ya Kristo. Kuna masimulizi mengi yanayoeleza juu ya nguvu ya imani kwa yule aaminiye. Leo tunapewa mifano miwili ya watu wenye imani. Kutokana na imani yao wameweza kutimiziwa haja zao na Yesu. Kwanza ni huyu jumbe aliyefiwa na bintiye, na pili ni mama aliyekuwa na tatizo la kutokwa damu kwa miaka kumi na miwili. Wote hawa, wakisukumwa na imani yao kwa Yesu. Imani hii kwa Mungu inatokana na mwanadamu kutambua kuwa Mungu ndiye mfadhiri, mwenye rehema na haki, anayetutuliza katika mahangaiko ya kibinadamu na pia uhusiano wet una Mungu ni wa milele. Sisi kama taifa la Mungu la leo, tuna wajibu wa kujua Mungu ni nani kwetu, na nafasi yetu kwake ni ipi. Pia tuwe na imani katika nguvu na uweza wake wa kutuponya kimwili na kiroho. Tuache kuweka imani yetu kwa binadamu wenzetu au viumbe wengine kwani Mungu wetu anatosha na ndiye anayetuwezesha mpaka sasa.
SALA: Mungu Mwenyezi, utusaidie katika kutokuamini kwetu.