SOMO 1: Isa. 66:10-14
Furahini pamoja na Yerusalemu, shangilieni kwa ajili yake, ninyi nyote mmpendao; furahini pamoja naye kwa furaha, ninyi nyote mliao kwa ajili yake; mpate kunyonya, na kushibishwa kwa maziwa ya faraja zake, mpate kukama, na kufurahiwa kwa wingi wa utukufu wake. Maana Bwana asema hivi, “Tazama, nitamwelekezea amani kama mto, na utukufu wa mataifa kama kijito kifurikacho, nanyi mtapata kunyonya; mtabebwa; na juu ya magoti mtabembelezwa. Mfano wa mtu ambaye mama yake amfariji, ndivyo nitakavyowafariji ninyi; nanyi mtafarijiwa katika Yerusalemu. Nanyi mtaona, na mioyo yenu itafurahi, na mifupa yenu itasitawi kama majani mabichi; na mkono wa Bwana utajulikana, uwaelekeao watumishi wake.”
Wimbo Wa Katikati: Zab. 66:1-7, 16, 20
- Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote,
Imbeni utukufu wa jina lake.
Tukuzeni sifa zake,
Mwambieni Mungu, Matendo yako yatisha kama nini!
(K) Mpigie Mungu kelele za shangwe nchi yote.
- Nchi yote itakusujudia na kukuimbia,
Naam, italiimbia jina lako.
Njoni yatazameni matendo ya Mungu,
Hutisha kwa mambo awatendayo wanadamu. (K) - Aligeuza bahari ikawa nchi kavu;
Katika mto walivuka kwa miguu;
Huko ndiko tulikomfurahia,
Atawala kwa uweza wake milele. (K) - Njoni, sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu,
Nami nitayatangaza aliyonitendea roho yangu.
Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu,
Wala kuniondolea fadhili zake. (K)
SOMO 2: Gal. 6:14-18
Mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu. Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya. Na wote watakaoenenda kwa kanuni hiyo, amani na iwe kwao na rehema, naam, kwa Israeli wa Mungu. Tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu. Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. Amina.
SHANGILIO: Yn. 1:12,14
Aleluya, aleluya,
Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu;
Wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu.
Aleluya.
INJILI: Lk. 10:1-12, 17-20
Baada ya hayo Bwana aliweka na wengine, sabini, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe. Akawaambia, “Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Enendeni, angalieni, nawatuma kama wana kondoo kati ya mbwa-mwitu. Msichukue mfuko, wala mkoba, wala viatu; wala msimwamkie mtu njiani. Na nyumba yo yote mtakayoingia, semeni kwanza, ‘Amani iwemo nyumbani humu’; na akiwamo mwana wa amani, amani yenu itamkalia; la, hayumo, amani yenu itarudi kwenu. Basi, kaeni katika nyumba iyo hiyo, mkila na kunywa vya kwao; maana, mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake. Msihame-hame kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii. Na mji wo wote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu; wapozeni wagonjwa waliomo, waambieni, ‘Ufalme wa Mungu umewakaribia.’ Na mji wowote mtakaouingia, nao hawawakaribishi, tokeni humo, nanyi mkipita katika njia zake semeni, Hata mavumbi ya mji wenu yaliyogandamana na miguu yetu tunayakung’uta juu yenu. Lakini jueni hili, ya kuwa Ufalme wa Mungu umekaribia. Nawaambia ya kwamba siku ile itakuwa rahisi zaidi Sodoma kuistahimili adhabu yake kuliko mji huo.”
Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, “Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako.” Akawaambia, “Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru. Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.”
*Somo fupi
TUANDIKISHE MAJINA YETU MBINGUNI SIYO KATI YA WATU: Wazo hili linakuja kufuatia kauli ya Yesu inayosahihisha furaha ya wafuasi sabini na wawili. Walikuwa wametumwa kuyafanya mazoezi ya kuihubiri Injili na kupewa mamlaka dhidi ya Shetani. Kama anavyosema mwenyewe, amri ya kukanyaga nyoka na nge na nguvu zote za yule adui. Alikuwa amewahakikishia usalama wasidhurike na kitu chochote. Aliwapa maelekezo mengi kusudi wafanye kazi kwa ufanisi. Aliwakataza sana wasitafute kukidhi raha. Ndipo aliwataka wajitambue wametumwa kama wana kondoo kati ya mbwa-mwitu. Halafu wasichukue vitu vya kuwaghasi kama vile mifuko, mikoba na viatu. Aliwakataza hata kuwaamkia watu njiani. Akawaagiza kuwapa watu zawadi ya amani watakapokuwa wanaingia kwenye nyumba yo yote. Akawaomba wasiwe watu wa madai makubwa wakae katika nyumba watakayo ingia na kula na kunywa vya hapo kwa sababu kila mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake. Aliwakanya dhidi ya uroho. Aliwakataza wasifanane na paka wenye kutafuta vinono vya watu hata kuwa na tabia ya kuhama-hama kutoka nyumba moja kwenda nyumba nyingine. Akawataka mji wowote wakiingia na kukaribishwa, kwa vile pasipo kuchagua vyakula vitakavyowekwa mbele yao; wawapoze wagonjwa waliomo humo, wakiwaambia ufalme wa Mungu umewakaribia. Pamoja na hayo aliwaagiza wakikataliwa na mji wowote wafanye ishara ya kutoka pale pasipo lawama kwa kuwakung’utia mavumbi yaliyogandamana na miguu yao.
Katika mazingira ya siku hizi kutumwa kwao kulilingana na jinsi wanafunzi wa ualimu wanavyotumwa na walimu wao kwenye mazoezi ya kufundisha. Kwa Kiingereza mazoezi hayo huitwa “Block Teaching Practice – BTP.” Wanafunzi wa ualimu wakiwa katika mazoezi hayo hukaguliwa na walimu wao. Hukaguliwa wakiwa mahali pa kazi ili kuwaona wanavyofanya kazi katika uhalisia wake na walimu huwapa alama za ufaulu. Yesu hakwenda kuwakagua isipokuwa walifanya kazi peke yako na waliripoti wenyewe mambo yalivyokwenda. Kumbe jinsi walivyoripoti walionyesha udhaifu mkubwa katika kujua vitu vyenye thamani kiroho. Walichoona cha maana Yesu alikikataa. Katika yote waliyofanya wao walifurahia zaidi kuona wanamwangusha Shetani. Inaonekana mafanikio hayo yaliwapa heshima na utukufu machoni pa watu. Hapo ndipo alipowasahihisha. Alitaka wafurahie jinsi walivyoandikisha majina yao mbinguni kwa kazi waliyochapa. Wanaposahihishwa wao tunasahihishwa sisi zote. Kumbe, Bwana anataka tujitume katika wito na utume wetu tuandikshe majina yetu mbinguni na siyo kufurahia mafanikio yanayoshangiliwa katika dunia hii. Kumbe, furaha ya kweli lazima ihusike na kuwafarijiwa na Bwana na siyo kushangiliwa na watu duniani.
Somo la kwanza linaelekeza vizuri kitu cha kufurahia. Linasema watu wafurahie kushibishwa kwa maziwa ya faraja za Mungu. Wakame na kufurahia wingi wa utukufu wake. Ndio maana Mungu alisema Waisraeli wafurahi kwa misingi hiyo hapo watakapo elekezewa amani kama mto na utukufu wa mataifa kama kijito kifurikacho, yaani hapo watakapopata kunyonya na kubebwa; hapo watakapowekwa na Mungu juu ya magoti na kubembelezwa kama mtu anayefarijiwa na mama yake. Kifupi, furaha isiyounganishwa na Mungu ni dhalili kabisa.
Somo la pili linatuelekeza kwenye uelewa wa juu kabisa wa furaha ya kweli. Linatueleza mtu anayeifahamu furaha ya kweli anaweza kufurahia hata mateso ilmradi yamemwelekeza mtu kwenye zawadi ya uzima wa milele. Ndipo mtume Paulo anayeona jinsi msalaba ulivyomwelekeza mtu kwenye uzima wa milele anatamba akisema haoni fahari juu ya kitu cho chote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwake, na yeye kwa ulimwengu. Anaongeza kusema kwake kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, isipokuwa kiumbe kipya. Mwisho anawatakia wote watakaoenenda kwa kanuni hiyo, amani na iwe kwao na rehema. Kumbe, tungekuwa na uelewa kamili juu ya furaha ya kweli, tusingebabaishwa na maumivu ya dunia hii, wala machungu ya uhitaji wowote pamoja na kifo chenyewe. Tunalalamika katika kila adha kwa sababu tunashindwa kuona hata yale yanayounganika na njia ya wokovu wetu. Mungu atusaidie tuelewe na kutathimini vizuri mambo ya dunia hii. Tuwinde zaidi kuandikisha majina yetu mbinguni wala siyo fahari na kutukuzwa na ulimwengu huu.
SALA: Ee Yesu Kristo, Bwana wetu uliyetuagiza katika miito na utume mbalimbali, kwa baraka na rehema zako, pamoja na hekima ya Roho Mtakatifu, tufanikishe katika kazi zetu na uyaandike majina yetu madhubuti kitabuni mwako. Amina.