Julai 2,2022; Jumamosi: Juma la 13 la Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 3
SOMO I: Amo. 9:11-15

Bwana asema hivi, “Siku hiyo nitaiinua tena maskani ya Daudi iliyoanguka, na kuziba mahali palipobomoka; nami nitayainua magofu yake, na kuyajenga kama siku za kale; wapate kuyamiliki mabaki ya Edomu, na mataifa yote yaitwayo kwa jina langu,” asema Bwana, afanyaye hayo. “Angalieni, siku zinakuja,” asema Bwana, “ambazo huyo alimaye atamfikiria avunaye, na yeye akanyagaye zabibu atamfikilia apandaye mbegu; nayo milima itadondoza divai tamu, na vilima vyote vitayeyuka. Nami nitawarejeza tena watu wangu Israeli waliohamishwa, nao wataijenga miji iliyoachwa maganjo, na kukaa ndani yake; nao watapanda mizabibu katika mashamba, na kunywa divai yake; nao watafanyiza Bustani, na kula matunda yake. Nami nitawapanda katika nchi yao, wala hawatang’olewa tena watoke katika nchi yao niliyowapa,” asema Bwana, Mungu wako.

Wimbo Wa Katikakati: Zab. 85:8, 10-13

 1. Nisikie atakavyosema Mungu Bwana,
  Maana atawaambia watu wake amani.
  Naam, na watauwa wake pia.
  Bali wasiurudie upumbavu tena.

(K) Bwana anawaambia watu wake amani.

 1. Fadhili na kweli zimekutana,
  Haki na amani zimebusiana.
  Kweli imechipuka katika nchi,
  Haki imechungulia kutoka mbinguni. (K)
 2. Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
  Na nchi yetu itatoa mazao yake.
  Haki itakwenda mbele zake,
  Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia. (K)

INJILI: Mt. 9: 14-17

Wanafunzi wake Yohane walimwendea Yesu wakasema, “Kwa nini sisi na Mafarisayo twafunga, bali wanafunzi wako hawafungi?” Yesu akawaambia, “Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga. Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; maana kile kilichotiwa huondoa kipande cha lile vazi, na pale palipotatuka huzidi. Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama wakitia, vile viriba hupasuka, divai ikamwagika, na viriba vikaharibika; bali hutia divai mpya katika viriba vipya, vikahifadhika vyote.”

TAFAKARI
TUKIWA NA KRISTO HATUNA SABABU YA KUFUNGA: Sala na matendo yote ya ibada kwa Mungu ni ya muhimu sana katika maisha yetu kama wafuasi wa Kristo. Mafundisho mbalimbali ya Yesu, Mitume wake, kina baba wa Kanisa na viongozi wa Kanisa wanasisitiza sana umuhimu na umaana wa Sala. Pia kufunga na kutenda matendo ya huruma na ibada kwa ajili ya nia mbalimbali zinazompendeza Mwenyezi Mungu. Lakini Kanisa pia limetuwekea vipindi mbalimbali katika mwaka wa liturjia ili vitusaidie kutimiza wajibu wetu wa kiimani kwa Mungu. Kwa mfano, kuna kipindi cha Kwaresima ambacho Kanisa linatuhimiza kufunga, kuongeza moyo wa sala na kutenda matendo ya huruma kama sehemu yetu ya kuomba toba kwa kumkose Mungu. Zaidi kujiandaa kwa ajili ya ufufuko wa Bwana (Pasaka). Leo Kristo anawaeleza wanafunzi wa Yohane, kuwa pindi yu pamoja nao hawana sababu ya kufunga hadi pale atakapoondolewa. Tutambue kuwa tukiwa ndani ya Yesu, hatuna sababu ya kuhuzunika (kufunga) kwani kaja kutukomboa katika lindi la majonzi na mateso. Hivyo, tuwe naye daima na tufuate kikamilifu kalenda ya liturjia ili itusaidie kuiishi imani yetu.

SALA: Ee Mwenyezi Mungu, tunakuomba uikamilishe furaha yetu kwa kumuishi Kristo siku zote za maisha yetu.