Mt. Ireneo, Askofu na Shahidi
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Amo. 3: 1-8; 4: 11-12
Lisikieni neno hili alilolisema Bwana juu yenu, “Enyi wana wa Israeli, juu ya jamaa yote niliowapandisha kutoka nchi ya Misri, nikisema, ‘Ni ninyi tu niliowajua katika jamaa zote zilizo duniani; kwa sababu hiyo nitawapatiliza ninyi maovu yenu yote. Je! watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana? Je! simba atanguruma mwituni, asipokuwa na mawindo? Mwanasimba atalia pangoni mwake, ikiwa hakupata kitu? Je! ndege ataanguka mtegoni juu ya nchi, mahali asipotegewa tanzi? Mtego utafyatuka juu ya nchi, bila kunasa kitu cho chote? Je! tarumbeta itapigwa mjini, watu wasiogope? Mji utapatikana na hali mbaya, asiyoileta Bwana? Hakika Bwana Mungu hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake. Simba amekwisha kunguruma, ni nani asiyeogopa?’” Bwana Mungu amenena, “Ni nani awezaye neno ila kutabiri? Baadhi yenu nimewaangamiza, kama hapo Mungu alipoiangamiza Sodoma na Gomora, nanyi mkawa kama kinga kilichonyakuliwa motoni; lakini hamkunirudia mimi,” asema Bwana. “Basi nitakutenda hivi, Ee Israeli; na kwa sababu nitakutenda hivi, ujiweke tayari kuonana na Mungu wako, Ee Israeli.”
Wimbo Wa Katikati: Zab. 5: 4-7
- Huwi Mungu apendezwaye na ubaya;
Mtu mwovu hatakaa kwako;
Wajivunao hawatasimama mbele za macho yako.
(K) Bwana uniongoze kwa haki yako.
- Unawachukia wote watendao ubatili.
Utawaharibu wasemao uongo;
Bwana humzira mwuaji na mwenye hila. (K) - Bali mimi, kwa wingi wa Fadhili zako,
Nitaingia nyumbani mwako;
Na kusujudu kwa kicho,
Nikielekea hekalu lako takatifu. (K)
INJILI: Mt. 8:23-27
Yesu alipanda chomboni, wanafunzi wake wakamfuata. Kukawa msukosuko mkuu baharini, hata chombo kikafunikizwa na mawimbi; naye alikuwa amelala usingizi. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, “Bwana, tuokoe, tunaangamia.” Akawaambia, “Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba?” Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu. Wale watu wakamaka wakisema, “Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii?”
TAFAKARI
BWANA TUOKOE TUNAANGAMIA: Nabii Amosi anatumia maswali bila majibu ili kulishawishi taifa la Mungu kupokea ujumbe wake kujiandaa kukutana na Mungu. ‘ujiweke tayari kuonana na Mungu wako.’ Katika hatari ya kuangamia mitume wanamwamsha Yesu aliyelala chomboni wanapokumbwa na dhoruba. Anawahoji kuhusu hofu yao;‘mbona mmekuwa waoga?’, kisha anatuliza dhoruba, huku wanafunzi wake wakimshangaa. Amosi alikuwa mjumbe wa Mungu katika taifa lililokumbwa na hatari ya kuangamizwa na maasi ya ulimwengu wao. Japo hawakumwita hadi ujio wa Amosi, Mungu alikuwa daima kati yao. Kristo yupo kimya chomboni, hadi wanafunzi wanapomwamsha.
Mungu daima yupo kati ya wanaomheshimu na kumtumainia. Anasikia kilio cha wote wanaomwomba msaada na kuwahudumia kupitia watumishi wake. Tumwamini Mungu aliyepo daima ndani ya Kanisa lake. Tumshukuru tunapokuwa na kheri. Tumwite tunapokumbwa na dhoruba na atatuokoa.
SALA: Ee Bwana, utujalile kukutambua wewe uliye daima kati yetu, na utupe ujasiri wa kukuita tunapojikuta hatarini.