Juni 27,2022; Jumatatu: Juma La 13 La Mwaka

Mt. Sirili wa Alexandria, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Zaburi: Juma 1
SOMO I: Amo. 2:6-10, 13-16
Haya ndiyo asemayo Bwana; “Kwa makosa matatu ya Israeli, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wamewauza wenye haki kwa fedha, na maskini kwa jozi ya viatu; nao hutwetea mavumbi yaliyo juu ya vichwa vya maskini, na kuipotosha njia ya wenye upole; na mtu na baba yake humwendea mwanamke mmoja, hata kulitia unajisi jina langu takatifu; nao hujilaza karibu na kila madhabahu juu ya nguo zilizowekwa rehani, na katika nyumba ya Mungu wao hunywa divai ya watu waliotozwa fedha. Lakini nalimwangamiza mwamori mbele yao, ambaye urefu wake ulikuwa kama urefu wa mierezi, tena alikuwa na nguvu kama mialoni; lakini naliyaangamiza matunda yake toka juu, na mizizi yake toka chini. Pia naliwapandisha ninyi kutoka nchi ya Misri, nikawaongoza muda wa miaka arobaini jangwani, ili mpate kuimiliki nchi ya Mwamori. Tazameni, nitawalemea ninyi, kama gari lilemeavyo lililojaa miganda. Naye apigaye mbio atapotewa na kimbilio; wala aliye hodari hataongeza nguvu zake; wala shujaa hatajiokoa nafsi yake; wala apindaye upinde hatasimama; wala aliye mwepesi wa miguu hataokoka; wala apandaye farasi hatajiokoa nafsi yake; naye mwenye moyo mkuu miongoni mwa mashujaa atakimbia uchi siku ile,” asema Bwana.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 50:16-23

 1. Mtu asiye haki, Mungu amwambia,
  Una nini wewe kuitangaza sheria yangu,
  Na kuliweka agano langu kinywani mwako?
  Maana wewe umechukia maonyo,
  Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.

(K) Yafahamuni hayo, ninyi mnaomsahau Mungu.

 1. Ulipomwona , mwivi ulikuwa radhi naye,
  Ukashirikiana na wazinzi.
  Umekiachia kinywa chako kinene mabaya,
  Na ulimi wako watunga hila. (K)
 2. Umekaa na kumsengenya ndugu yako,
  Na mwana wa mama yako umemsingizia.
  Ndiyo ulivyofanya, name nikanyamaza;
  Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe.
  Walakini nitakukemea;
  Nitayapanga hayo mbele ya macho yake. (K)
 3. Yafahamuni hayo,
  Ninyi mnaomsahau Mungu.
  Nisije nikawararueni,
  Asipatikane mwenye kuwaponya.
  Atoaye dhabihu za kushukuru,
  Ndiye anayenitukuza.
  Naye autengenezaye mwenendo wake,
  Nitamwonyesha wokovu wa Mungu. (K)

INJILI: Mt. 8:18-22

Yesu alipoona makutano mengi wakimzunguka, aliamuru kuvuka kwenda ng’ambo. Mwandishi mmoja akamwendea, akamwambia, “Mwalimu, nitakufuata ko kote uendako.” Yesu akamwambia, “Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana vioto; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake.” Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, “Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu.” Lakini Yesu akamwambia, “Nifuate; waache wafu wazike wafu wao.”

TAFAKARI
WITO WA TOBA NA HAKI: Amosi anafanya unabii wake karne ya sita kabla ya Kristo, nyakati zilizogubikwa na vita, migogoro ya kijamii, kisiasa na kidini. Wanyonge walijikuta kwenye dhuluma kubwa. Kwa kujihami kwa siraha ya neno la Mungu na Sala, manabii walipigana kwa ajili ya haki, heshima na uhuru wa wanyonge. Amosi anatabiri hukumu waasi wasipotubu machukizo yao manne makubwa; kudorora kwa haki na utu, unyanyasaji wa wanyonge, zinaa kati ya ndugu na starehe kwa jasho la wanyonge. Zaburi inataja maswala yanayomchukiza Mungu na kutahadharisha kwa kupendekeza toba. Yesu aliwahi kuonya, ‘mtaangamia wote vivyo hivyo msipotubu’. Kwenye injili anawaacha kwanza wanaomsonga na kwenda faraghani kwa sala akiwahimiza wanaopenda kumfuata.
Kanisa na waamini wanahimizwa kuhubiri toba, kuwaonya wanaopotea na kuwa watetezi wanaodhulumiwa.

SALA: Ee Mungu, utujalie kusikiliza sauti yako kupitia wanyonge, na kupigana dhidi ya dhuluma kwa neno lako na sala.