Juni 20,2022; Jumatatu: Juma La 12 La Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: 2Fal. 17:5-8, 13-15, 18

Mfalme wa Ashuru alikwea katikati ya nchi yote, akaenda Samaria, akauhusuru miaka mitatu. Katika mwaka wa kenda wa Hoshea, huyo mfalme wa Ashuru akautwaa Samaria, akawahamisha Israeli mpaka Ashuru, akawaweka katika Hala na Habori, karibu na mto wa Gozani, na katika miji ya Wamedi. Yalitukia hayo kwa sababu wana wa Israeli walikuwa wametenda dhambi juu ya Bwana, Mungu wao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri watoke chini ya mkono wa Farao mfalme wa Misri, wakawaacha miungu mingine. Wakaziendea sheria za mataifa, ambao Bwana aliwafukuza mbele ya wana wa Israeli, na sheria za wafalme wa Israeli walizozifanya. Pamoja na hayo Bwana aliwashuhudia Israeli, na Yuda, kwa kinywa cha kila nabii, na cha kila mwonaji, akisema, Geukeni, na kuziacha njia zenu mbaya, mkazishike amri zangu na hukumu zangu, sawasawa na ile sheria yote niliyowaamuru baba zenu, nikawapelekea kwa kinywa cha manabii watumishi wangu. Walakini hawakutaka kusikia, bali walifanya shingo zao kuwa ngumu, kama shingo za baba zao; wasiomwamini Bwana, Mungu wao. Wakazikataa sheria zake na agano lake, alilolifanya na baba zao; na shuhuda zake alizowashuhudia; wakafuata ubatili, wakawa ubatili, nao wakaandamana na mataifa waliowazunguka, ambao Bwana alikuwa amewaagiza, wasitende kwa mfano wao. Kwa hiyo Bwana akawaghadhibikia Israeli sana, akawahamisha mbali na uso wake; wala hapana aliyesalia ila kabila ya Yuda peke yake.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 60:1-3, 10-11

 1. Ee Mungu, umetutupa na kututawanya,
  Umekuwa na hasira, uturudishe tena.

(K) Uokoe kwa mkono wako wa kuume, ee Bwana, utuitikie.

 1. Umeitetemesha nchi na kuipasua,
  Upaponye palipobomoka, maana inatikisika.
  Umewaonyesha watu wako mazito,
  Na kutunywesha mvinyo ya kutuyumbisha. (k)
 2. Ee Mungu, si Wewe uliyetutupa?
  Wala, Ee Mungu hutoki na majeshi yetu?
  Utuletee msaada juu ya mtesi,
  Maana wokovu wa binadamu haufai. (K)

INJILI: Mt. 7:1-5

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Msihukumu, msije mkahukumiwa ninyi. Kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa. Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au utamwambiaje nduguyo, ‘Niache nikitoe kibanzi katika jicho lako’; na kumbe! Mna boriti ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako.

TAFAKARI
MSIHUKUMU MSIJE MKAHUKUMIWA: Taifa la Israeli, baada ya kukombolewa mikononi mwa Farao na kuona makuu ya Mungu kwa muda mrefu likielekea katika nchi ya ahadi, linamwacha Mungu na kugeukia miungu ya mataifa. Watu hawa wangefikiriwa kuwa wakomavu katika imani yao kwa Mungu mmoja kumbe haikuwa hivyo. Kristo anawafundisha mitume wake kutowahukumu wengine wasije wakahukumiwa wao wenyewe. Inaonekana rahisi kuyaona na kuyasemea makosa ya wengine. Anasisitiza kujitakasa wenyewe ili tuone vema zaidi mapungufu ya wengine na kuwasaidia.
Tusihukumu kwani wote ni wakosefu na tunahitaji daima huruma na msamaha kutoka kwa Mungu, sawa na taifa kosefu la Israeli. Yeye, Mungu Baba anatutendea kwa moyo wa huruma, uvumilivu na upendo. Inatupasa nasi kuwatendea vivyo hivyo ndugu zetu. Aidha, hakuna aonaye moyoni mwa mtu kwa uhakika ila Mungu.

SALA: Ee Bwana, utujalie kukutafuta wewe kwa moyo safi, tujitakase nafsi zetu, na kujiepusha kuwahukumu wengine.