Juni 19,2022; Jumapili: Mwili Na Damu Ya Bwana Wetu Yesu Kristu

SOMO 1: Mwa. 14:18-20

Melkizedeki mfalme wa Salemu alileta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana. Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi. Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 110:1-4

  1. Neno la Bwana kwa Bwana wangu,
    Uketi mkono wangu wa kuume,
    Hata niwafanyapo adui zako
    Kuwa chini ya miguu yako.

(K) Ndiwe kuhani hata milele, Kwa mfano wa Melkizedeki.

  1. Bwana atainyosha toka Sayuni
    Fimbo ya nguvu zako,
    Uwe na enzi kati ya adui zako. (K)
  2. Kwa uzuri wa utakatifu,
    Tokea tumbo la asubuhi,
    Unao umande wa ujana wako. (K)
  3. Bwana ameapa,
    Wala hataghairi,
    Ndiwe kuhani hata milele,
    Kwa mfano wa Melkizedeki. (K)

SOMO 2: 1 Kor. 11:23-26

Mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema. Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu. Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.

SHANGILIO: Yn. 6:51

Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi chakula chenye uzima
kilichoshuka kutoka mbinguni;
asema Bwana; mtu akila chakula hiki, ataishi milele.
Aleluya.

INJILI: Lk. 9:11-17

Makutano walimfuata Yesu; akawakaribisha, akawa akisema nao habari za ufalme wa Mungu, akawaponya wale wenye haja ya kuponywa. Na jua likaanza kushuka; wakamwendea wale Thenashara, wakamwambia, “Uage mkutano, ili waende katika vijiji na mashamba ya kandokando wapate mahali pa kulala na vyakula, maana hapa tulipo ni nyika tupu.” Akawaambia, “Wapeni ninyi chakula.” Wakasema, “Hatuna kitu zaidi ya mikate mitano na samaki wawili, tusipokwenda tukawanunulie watu hawa wote vyakula.” Kwa kuwa wanaume waliokuwako walipata kama elfu tano. Akawaambia wanafunzi wake, “Waketisheni watu kwa safu, kila safu watu hamsini.” Wakafanya hivyo, wakawaketisha wote. Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni akavibariki, akavimega, akawapa wanafunzi wake ili wawaandikie mkutano. Wakala, wakashiba wote; na katika vile vipande vilivyowabakia walikusanya vikapu kumi na viwili.

TAFAKARI
TUIPOKEE VYEMA SAKRAMENTI YA MUNGU KUTUJALI WANADAMU: Wazo hili ni maana nzima ya kile Yesu alichowafanyia wale waliokuwa wameshinda na njaa wakimsikiliza yeye. Walichoka. Mitume, sawa na sisi wanadamu wengine, walitaka kukwepa jukumu la kuwashughulikia wenye njaa. Walitaka kukwepa suala la kuwapa chakula. Ndivyo tulivyo wanadamu wengi, tunafurahia uwapo wa watu wengine wakati ule tusipodaiwa chochote cha kutoa. Tunapofikia hatua ya kutakiwa tutoe kitu, tunarudi nyuma na pengine kuwakimbia wahitaji hata kama tumetoka nao kumoja. Mwelekeo wetu ni wa kujivua kazi ya kuwashughulikia wenye dhiki. Tunawapenda watu wasipokuwa na dhiki, au wakiwa na dhiki basi dhiki isiyotudai sisi kitu.
Mitume walimwomba Yesu akatishe mafundisho yake, awaage watu wakatafute chakula na mahali pa kulala katika vijiji na mashamba ya kandokando eti kwa vile ilikuwa jioni na pale walipokuwapo palikuwa nyika tupu. Hapo ndipo alipowaambia wawape wao chakula badala ya kuwatimua bila kuwajali. Mitume wakakana uwezo wa kuwapa chakula watu. Wakasema wana mikate mitano na samaki wawili tu wakati pale walikuwapo wanaume wasiopungua elfu tano, yaani bila kuwahesabu akinamama na watoto. Wakatia mashaka mbele ya Yesu kwamba katika hali hiyo wasipoenda kuwanunulia mikate hakutakuwa na jema. Katika hesabu mitume wanatishwa na hesabu ya wanaume waliokuwapo pale kwa sababu wanaume kwa kawaida wanakula zaidi ya akinamama na watoto. Na ni kweli, wanaume wanakula zaidi ya wanawake na watoto kwa sababu mwanaume aliyetimia ana chembe chembe hai za damu asimilia kumi zaidi ya mwanamke na hivyo anachukua asilimia kumi zaidi ya hewa ya oksijeni na hivyo akila chakula cha wanga, wanga ukichomwa mwilini mwake anakuwa na nguvu zaidi ya mwanamke. Lakini kwa nguvu nyingi, akipoteza hizo nguvu, huhitaji kula zaidi ili kuzifidia. Yesu alijua ukweli wa wanaume kula zaidi ya wenzao pia, tena kisayansi na siyo kama mitume kwa uzoefu wa kuwajua wanaume tu.
Wakati mitume wanajikanyaga kanyaga kwa kutokuweza kuwapa chakula watu wengi hivyo wakiwamo kati yao wanaume wanaojulikana kwa kula sana, katika Yn 6:6 imeandikwa alikuwa anawajaribu wanafunzi tu kwa vile yeye mwenyewe alikuwa anajua alichokuwa anataka kufanya. Kifupi, alikuwa anajua anataka kufanya muujiza wa kuwalisha watu wote hao kwa kuwaongezea mikate na hao samaki. Basi, akaacha kupima jinsi mitume wanavyoweza kutatua tatizo la wanadamu wenzao akawaagiza watu wawekwe mafungu mafungu tayari kwa muujiza mkubwa. Waliketishwa, kusudi wapumzike na kustarehe. Tukumbuke enzi zile Wayahudi walikuwa wanapaswa kumsikiliza wangali wamesimama hata kama ingekuwa kwa saa ngapi. Aliwabarikia chakula, akawalisha wote kwa samaki wale wale watano na samaki wawili. Wakashiba na kustaajabu kabisa. Baada ya kushiba watu walitawanyika na kwenda kutafuta mahali pa kulala. Mahali pa kulala si jambo la maana sana kuliko kushiba. Kati ya mahitaji ya mwanadamu kula na kunywa ni hitaji la kwanza kwa sababu linahusika moja kwa moja na uhai. Asiyekula huweza kufa.
Muujiza huu ulikuwa kati ya mambo Mungu aliyokusudia yawaelekeze watu kwenye muujiza wa sakramenti ya Ekaristi Takatifu, chakula cha kiroho kuwakinga dhidi ya kufa kiroho. Kutokana na maringo ya Yesu, kuwafundisha watu mpaka jioni kabisa bila kujali sana kuchwa kwa jua hakika alijua anachotaka kufanya. Hili ni dokezo la karibu kabisa kwamba Mungu alishapanga tangu milele kwamba atawalisha wanadamu kwa chakula cha ajabu kiroho. Ishara za mpango huo zipo katika Agano la Kale na Agano Jipya pia. Ishara za kwanza kwanza ni mkate usiotiwa chachu kule Misri, Wayahudi walipokuwa wanatoka mbio mbio kutoka Misri (Kut 12:1-28). Ishara nyingine ni kushibishwa kwao kwa manna na kware (Kut 16:1-36). Ishara katika Agano Jipya ni miujiza ya kuongeza mikate na kuwalisha maelfu ya watu (Mt 14:13-21, Mk 6:30-44, Lk 9:10-17, Yn 6:1-15)
Kwa kusema hivi tunaweza kuhitimisha ifuatavyo. Ekaristi Takatifu ni chakula kilichopangwa tangu milele kuwekwa kwa ajili ya kuwapa lishe watu kiroho kusudi wapate nguvu katika kumfuasa Mungu. Ni chakula ambacho Mungu alijua ataamua kwa hiyari na upendo wake mwenyewe kuwapa watu. Ni chakula ambacho Mungu alijua kitakuwa chakula atakachokitoa kwa upendo wake tu tofauti na manna ambayo angetoa kufuatia kunung’unikiwa na watu jangwani. Ni chakula ambacho Mungu alijua watu wengi wakila watashiba pasipo kubaki na njaa na katika kula kila mmoja atashiba pasipo mmoja kuwazidi wenzake. Katika umungu wake aliyaona siyo makundi ya wahitaji waliokuwapo pale tu bali hata maelfu na mamilioni ya watu watakaozaliwa vizazi na vizazi hadi mwisho wa dunia. Ni chakula ambacho Mungu alijua kitakuwa mwili na damu ya Yesu Kristo, maana pungufu ya hapo hakiwezi kuwa chakula cha kufaa kiroho. Ni chakula ambacho Mungu alijua kitakuwa chakula cha kuwafurahisha wote na kwamba watu watakikigundua watashukuru na kufurahi sana. Hapo ndipo alijua kitaitwa “ekaristi” yaani neno lenye asili ya neno la Kigiriki “eukaristein” lenye maana ya “kushukuru”. Ni chakula ambacho Mungu alijua kitakuwa sakramenti itakayoasisiwa na Yesu katika karamu ya mwisho, muda mchache kabla ya kusulibiwa na kufa kwake. Ni chakula ambacho Mungu alijua kitakuwa chakula na kinywaji cha kweli. Ni chakula ambacho Mungu alijua watu wa ulimwengu nzima wakikipokea hawatakufa milele bali watafufuliwa siku ya mwisho na kadhalika.
Kumbe kutokana na haya yote ni dhahiri kwamba Ekaristi Takatifu ni chakula kinachoonyesha Mungu alitujali wanadamu na kutufikiria mema tangu milele. Kilikuwa katika fikra zake tangu milele. Alikusudia kwa namna ya pekee atutunze kwacho kiroho. Alikusudia atakapokuwa akitufundisha na kutuelekeza njia ya mbinguni tusipate unyafuzi wa kiroho na kadhalika. Tunaweza kusema mengi mengi katika kulielewa fumbo tunalosherehekea leo. Lakini kwa leo tukomee hapa. Itoshe.
Haya basi tuwajibike kwa chakula kitamu ambacho ni ishara ya wazi ya Mungu kutujali wanadamu tangu milele. Tukipokee kwa shukrani. Mungu ametupenda, basi tujitahidi kumpenda aliyetupenda. Ametujali, tumjali na tujaliane.

SALA: Ee Bwana Yesu Kristo, tusaidie kila siku kuvumbua upendo wako katika Ekaristi Takatifu. Tusaidie kukushukuru na kudumu nawe ili tusipate njaa duniani hapa hadi tufike kwako tutakakoshiba milele katika kukuona na kukaa nawe. Amina.