Juni 15,2022; Jumatano: Juma La 11 La Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO I: 2Fal. 2:1, 6-14

Bwana alipopenda kumpandisha Eliya mbinguni kwa upepo wa kisulisuli, Eliya alitoka Gilgali pamoja na Elisha. Eliya akamwambia, “Tafadhali kaa hapa; maana Bwana amenituma niende mpaka Yordani.” Akasema, “Kama Bwana aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha.” Wakaendelea mbele wote wawili. Basi watu hamsini wa wale wana wa manabii wakaenda wakasimama, kuwakabili kwa mbali; na hao wawili wakasimama karibu na Yordani. Eliya akalitwaa vazi lake la juu, akalikunja, akayapiga maji, yakagawanyika huku na huku, na hao wawili wakavuka pakavu. Hata ikawa, walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, “Omba kwangu lo lote utakalo nikutendee, kabla sijaondolewa kwako.” Elisha akasema, “Nakuomba, sehemu mara dufu ya roho yako iwe juu yangu.” Akasema, “Umeomba neno gumu; lakini, ukiniona nitakapoondolewa kwako, utalipata; la, hukuniona, hulipati.” Ikawa walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea, tazama! Kukatokea gari la moto, na farasi wa moto, likawatenga wale wawili; naye Eliya akapanda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli. Naye Elisha akaona, akalia, “Baba yangu, baba yangu,” Gari la Israeli na wapanda farasi wake! Asimwone tena kabisa; akashika mavazi yake mwenyewe, akayararua vipande viwili. Kisha akaliokota lile vazi la Eliya lililomwangukia, akarudi, akasimama katika ukingo wa Yordani. Akalitwaa lile vazi la Eliya lililomwangukia, akayapiga maji, akasema, “Yuko wapi Bwana, Mungu wa Eliya?” Naye alipoyapiga maji, yakagawanyika huko na huko, Elisha akavuka.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 31:19, 20, 23

 1. Jinsi zilivyo nyingi Fadhili zako
  Ulizowawekea wakuchao;
  Ulizowatendea wakukimbiliao
  Mbele ya wanadamu!

(K) Iweni hodari, mpige moyo konde,
ninyi nyote mnaomngoja Bwana.

 1. Utawasitiri na fitina za watu
  Katika sitara ya kuwapo kwako. (K)
 2. Mpendeni Bwana,
  Ninyi nyote mlio watauwa wake.
  Bwana huwaifadhi waaminifu,
  Humlipa atendaye kiburi malipo tele. (K)

INJILI: Mt. 6:1-6, 16-18

Yesu aliwaambia wanafunzi wake; “Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni. Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu. Amin, nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume; sadaka yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu.”

Amin, nawaambia, “Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao; ili waonekane na watu kuwa wanafunga, Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.”

TAFAKARI
IBADA ITOKAYO MOYONI SIO MAONYESHO: Nabii Eliya anapokaribia kuchukuliwa mbinguni anampa mwandamizi wake Elisha fursa ya kuomba lolote. Elisha anaomba kujaliwa roho ya Eliya maradufu. Kati ya sifa za Eliya ni roho ya unabii, anayemsikiliza Mungu, na kuwapatanisha wanadamu na Mungu. Kristo katika injili anawahimiza mitume wanapotoa sadaka, wanaposali na wanapofunga, wasijionyeshe ila matendo yao yawe katika usiri wa mioyo yao aonapo Mungu. Haya ndio mazoea ya manabii wengi; waliwasiliana na Mungu kila mara katika usiri wa mioyo yao, kisha wakaurudia umati kuwaletea ujumbe wa Mungu.
Yesu hakutafuta kusifiwa na watu. Alijitenga mara nyingi kwenda faraghani kuomba, hasa kabla ya hatua kubwa katika utume wake. Tunafundishwa kujenga ibada na sala ya kweli kutoka moyoni, ili tukubalike mbele za Mungu kuliko kusifiwa na watu.

SALA: Ee Bwana, utujalie roho wako, ibada ya kweli, uzima na amani kutoka moyoni.