Juni 14,2022; Jumanne: Juma La 11 La Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO I: 1Fal. 21:17-29

Neno la Bwana likamjia Eliya Mtishbi, kusema, “Ondoka, ushuke ukutane na Ahabu mfalme wa Israeli, akaaye katika Samaria; yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ndiko alikoshukia ili alitamalaki.” Ukamwambie, ukisema, “Bwana asema hivi, Je! Umeua, ukatamalaki?” Nawe utamwambia, Bwana asema hivi, “Mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba na damu yako, naam, damu yako.” Ahabu akamwambia Eliya, “Je! Umenipata, ewe adui yangu?” Akamwambia, “Nimekupata, kwa sababu umejiuza utende yaliyo mabaya machoni pa Bwana. Angalia, nitaleta mabaya juu yako; nami nitakuangamiza kabisa, nitamkatia Ahabu kila mume, aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli. Kisha nitaifanya nyumba yako iwe kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa ajili ya chukizo ulilonichukiza, hata kunighadhibisha, ukawakosesha Israeli.” Tena Bwana alinena habari za Yezebeli, akisema, “Mbwa watamla Yezebeli katika kiwanja za Yezreeli. Mtu wa nyumba ya Ahabu afaye mjini, mbwa watamla, na yeye afaye mashamba ndege wa angani watamla.” Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa Bwana, ambaye Yezebeli mkewe alimchochea. Akachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya Waamori, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli. Ikawa, Ahabu alipoyasikia maneno hayo, akayararua mavazi yake, akavaa magunia mwilini mwake, akafunga, akajilaza juu ya magunia, akaenda kwa upole. Neno la Bwana likaja kwa Eliya Mtishbi, kusema, “Huoni jinsi Ahabu alivyojidhili mbele yangu? Basi kwa sababu amejidhili mbele yangu, sitayaleta yale mabaya katika siku zake; ila katika siku za mwanawe nitayaleta mabaya hayo juu ya nyumba yake.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 51:1-4, 9, 15

 1. Ee Mungu unirhemu, sawasawa na Fadhili zako.
  Kiasi cha wimgi wa rehema zako,
  Uyafute maksa yangu.
  Unitakase dhambi zangu.

(K)Ee Mungu uturehemu uyafute makosa yetu.

 1. Maana nimejua mimi makossa yangu,
  Na dhambi yangu I mbele yangu daima.
  Nimekutenda dhambi Wewe peke yako. (K)
 2. Usitiri uso wako usitazame dhambi zangu,
  Uzifute hatia zangu zote.
  Ee Bwana, uifumbue modomo yangu,
  Na kinywa change kitazinena sifa zako. (K)

INJILI: Mt. 5:43-48

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi; ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi, mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru; je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.”

TAFAKARI
WAOMBEENI WANAOWAUDHI: Yesu anawafundisha mitume wake kuwapenda na kuwaombea adui zao, ili wapate kuwa wana wa Baba aliye mbinguni. Anawasihi kuiga mfano wa Mungu anayewatendea mema wema na wabaya, kwani kuwatendea wema ndugu pekee hakuna ushahidi tofauti na watu wa ulimwengu. Eliya anatumwa na Mungu kwa Mfalme Ahabu na mkewe Yezreeli kuwatangazia adhabu ya mauti kwa mauaji ya jirani kwa tamaa. Baada ya kuonyesha ibada ya toba, Mungu anaghairi na kumhurumia.
Mafundisho haya ya toba na msamaha kwa waliokosa badala ya adhabu mara mbili, yanatuelekeza kujitahidi kufanana zaidi na Mungu kwa moyo wa huruma, upendo na msamaha. Upendo kwa adui hauondoi haki kwa mkosewa na uajibikaji wa mkosaji. Mafundisho ya wema na upendo kwa jirani vinalenga kungoa mizizi ya kisasi mioyoni mwa watu.

SALA: Ee Bwana, utujalie kumaliza moyo wa chuki na kisasi, ili tukabiliane na uovu kwa wema na kuuangamiza.