Mt. Antoni wa Padua, Padre na Mwalimu wa Kanisa
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO I: 1Fal. 21:1-16
Nabothi Myezreeli alikuwa na shamba la mizabibu katika Yezreeli, karibu na nyumba ya kifalme ya Ahabu mfalme wa Samaria. Ahabu akasema na Nabothi, akamwambia, “Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, maana ni karibu na nyumba yangu; nami nitakupa badala yake shamba la mizabibu lililo zuri zaidi; au ukipenda, nitakupa fedha sawasawa na thamani yake.” Nabothi akamwambia Ahabu, “Bwana apishe mbali nikupe urithi wa baba zangu.” Basi Ahabu akaenda nyumbani kwake, ana moyo mzito, tena amekasirika, kwa sababu ya neno lile aliloambiwa na Nabothi Myezreeli, akisema, “Sitakupa urithi wa baba zangu.” Akajilaza kitandani pake, akageuza uso wake, akakataa kula. Lakini Yezreeli mkewe akamwendea, akamwambia, “Kwa nini roho yako ina huzuni hata usile chakula?” Akamwambia, “Kwa sababu nimesema na Nabothi Myezreeli,” nikamwambia, “Unipe shamba lako la mizabibu kwa fedha, au, ukipenda, nitakupa shamba la mizabibu lingine badala yake.” Akajibu, “Sitakupa shamba langu la mizabibu.” Yezebeli mkewe akamwambia, “Je! Sasa wewe unaumiliki ufalme wa Israeli? Ondoka, ule chakula, moyo wako ufurahi; mimi nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli.” Basi, akaandika nyaraka kwa jina la Ahabu, akazitia muhuri yake, akazipeleka zile nyaraka kwa wazee, na kwa watu wenye nguvu waliokuwa katika mji wake, waliokaa pamoja na Nabothi. Akaandika katika zile nyaraka, akasema, “Pigeni mbiu ya watu kufunga, mkamweke Nabothi juu mbele ya watu; mkainue watu wawili, watu wasiofaa, ili wamshitaki, na kumshuhudia, kunena, ‘Umemtukana Mungu na mfalme.’ Kisha mchukueni nje, mkampige kwa mawe, ili afe.” Wale wazee wa mji wake, na walio wenye nguvu waliokaa mjini mwake, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza, kama ilivyoandikwa katika nyaraka alizowapelekea. Wakapiga mbiu ya watu kufunga, wakamweka Nabothi juu ya mbele ya watu. Na hao watu wawili, watu wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia Nabothi mbele ya watu, wakasema, “Nabothi amemtukana Mungu na mfalme.” Ndipo wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa. Wakampelekea Yezebeli habari, wakasema, “Nabothi amepigwa kwa mawe, amekufa.” Ikawa Yezebeli aliposikia ya kwamba Nabothi amepigwa kwa mawe na kufa, Yezebeli akamwambia Ahabu, “Inuka, ulitamalaki shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, alilokataa kukupa kwa fedha, maana Nabothi hako hai, lakini amekufa.” Ikawa Ahabu aliposikia ya kwamba Nabothi amekufa, akaondoka, alitelemkie shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, ili alitamalaki.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 5:2-3, 5-7
- Uisikie sauti ya kilio changu,
Ee Mfalme wang una Mungu wangu,
Kwa maana Wewe ndiye nikuombaye.
Bwana, asubuhi utaisikia sauti yangu,
Asubuhi nitakupangia dua yang una kutazamia.
(K) Uisikie sauti ya kilio changu, ee Bwana.
- Wajivunao hawatasimama mbele ya macho yako;
Unawachukia wote watendao ubatili.
Utawaharibu wasemao uongo;
Bwana humzira mwuaji na mwenye hila (K) - Bali mimi, kwa wingi wa fadhili zako,
Nitaingia nyumbani mwako;
Na kusuduju kwa kicho,
Nikielekea hekalu lako takatifu. (K)
INJILI: Mt. 5:38-42
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Mmesikia kwamba imenenwa Jicho kwa jicho, na jino kwa jino; lakini mimi nawaambia, ‘Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili. Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili. Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo.’”
TAFAKARI
USILIPE MABAYA KWA MABAYA: Sheria ya ‘Jino kwa Jino’, ililenga kuzuia adhabu mara mbili kwa kila kosa, na sio kwa nia ya kulipa kisasi. Kristo anaikamilisha kwa kuwaambia wafuasi wake wasilipe kisasi kabisa. Kwa namna hii anawasaidia kuwa wema zaidi kuliko watu wa kawaida. Katika somo la kwanza mfalme Ahabu anaonyesha jinsi kisasi kinavyoweza kustawi kuwa ovu kubwa. Japo halikuwa shamba lake, Mfalme Ahabu anachukia, Nabothi anapomkatalia ombi la kubadilisha shamba lake. Pamoja na mkewe wanamwangamiza Nabothi ili walitwae shamba lake.
Matendo haya yanakumbusha visasi vilivyojaa ulimwenguni watu wawili au makundi yanapogombana kwa maslahi binafsi. Nchi zinaposhambuliana kivita, majirani au ndugu wanapogombania mashamba, mataifa yanapopigania mipaka kati ya mengine. Mafundisho ya Kristo yana wosia wa kinabii kwani alielewa kwamba kujaribu kulipa ovu kwa ovu, uovu yanaongezeka.
SALA: Ee Bwana, utupe moyo wa kulipa ubaya kwa wema, tuukuze wema na kuangamiza maovu.