Juni 12,2022; Jumapili: Utatu Mtakatifu

SOMO 1: Mit. 8:22-31

Bwana alikuwa nami katika mwanzo wa njia yake, Kabla ya matendo yake ya kale, Nalitukuka tokea milele, tangu awali, Kabla haijawako dunia. Wakati visipokuwako vilindi nalizaliwa, Wakati zisipokuwako chemchemi zilizojaa maji. Kabla milima haijawekwa imara, Kabla ya vilima nalizaliwa. Alipokuwa hajaiumba dunia, wala makonde, Wala chanzo cha mavumbi ya dunia; Alipozithibitisha mbingu nalikuwako; Alipopiga duara katika uso wa bahari; Alipofanya imara mawingu yaliyo juu; Chemchemi za bahari zilipopata nguvu; Alipoipa bahari mpaka wake, Kwamba maji yake yasiasi amri yake; Alipoiagiza misingi ya nchi; Ndipo nilipokuwa pamoja naye, kama stadi wa kazi; Nikawa furaha yake kila siku; Nikifurahi daima mbele zake; Nikiifurahia dunia inayokaliwa na watu; Na furaha yangu ilikuwa pamoja na wanadamu.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 8:3-8

 1. Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako,
  Mwezi na nyota uliziratibisha,
  Mtu ni kitu gani hata umkumbuke,
  Na binadamu hata umwangalie?

(K) Wewe, Mungu, Bwana wetu,
Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!

 1. Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu;
  Umemvika taji ya ufukufu na heshima;
  Umemtawaza juu ya kazi ya mikono yako;
  Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake. (K)
 2. Kondoo, na ng’ombe wote pia;
  Naam, na wanyama wa kondeni;
  Ndege wa angani, na samaki wa baharini;
  Na kila kipitiacho njia za baharini. (K)

SOMO 2: Rum. 5:1-5

Tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na tuwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo tunasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu. Wala si hivyo tu, ila na tufurahi katika dhiki pia; tukijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini; na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi.

SHANGILIO Ufu. 1:8

Aleluya, aleluya,
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
Mungu ambaye yupo, aliyekuako, na atakayekuja.
Aleluya.

INJILI: Yn. 16:12-15

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Ningali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa. Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza mimi; kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari. Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasheni habari.”

TAFAKARI
KWA MFANO WA UTATU MTAKAFITU TUUNGANE PASIPO KUTENGANA: Sherehe ya leo ni darasa la wazo hili. Tunasherehekea Utatu Mtakatifu, tunapokiri na kuungama imani yetu kwamba tuna Mungu mmoja lakini katika Nafsi tatu zisizogawanyika. Imani hii ya dini ya Kikristo tu, hakuna dini nyingine ulimwenguni, yaani hizo 20 zinazobaki zenye fundisho la msingi la namna hii. Tunapoadhimisha ibada pamoja hivi, yafaa tujichangamotishe katika kulielewa fumbo hili.
Jinsi Mungu mmoja anavyokuwa katika Nafsi tatu tunaweza kudokoa tukianzia kwenye maelezo ya utendaji wa Nafsi zenyewe. Hapo ni mahali salama kuanzia maelezo. Zimeungana pasipo kutengana. Injili tuliyoisikia inaonesha vyema jinsi Mungu Baba, Mungu Mwana na Roho Mtakatifu walivyo na utendaji wa kuungana. Yesu Kristo, ndiye Mungu Mwana, alipiga hema duniani (Yn 1:14) akawafundisha wanadamu mambo chungu nzima kwa maneno na matendo yake azizi.
Kufuatia kazi hiyo iliyofanyika ikilenga kuwaongoza wanadamu kwenye ukombozi anasema Roho Mtakatifu atafuatia kushadidia na siyo kuanzisha mapya ama kuvuruga yaliyofanikishwa. Anasema wakati utakapowadia Roho Mtakatifu atawadia na kuwaongoza watu katika kweli yote. Utakuwa ni utendaji wenye kushikamanisha Utatu Mtakatifu kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha wanadamu habari yake. Anazidi kufafanua kwamba Mungu Roho Mtakatifu atanitukuza Mungu Mwana; kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yake na kuwapasha wanadamu habari. Hapo Yesu anajumlisha mambo kwa kusema mambo yote ya Mungu Baba ni yake pia; na ni kwa sababu hiyo alisema kwamba Mungu Roho Mtakatifu atatwaa katika yaliyo yake, na kuwapasheni wanadamu habari.
Utendaji huu ni wa kupatana kwa hali ya juu. Ni utendaji unaoonesha kutogawanyika. Kumbe, kutokana na utendaji huu wa pamoja tunapata picha ya jinsi Mungu mmoja anavyokwenda katika Nafsi tatu. Kumbe, ni katika kutenda huko huko Nafsi zinavyopatikana. Ndiyo kisa kifalsafa ilieleweka vyema kwamba ni katika MUNGU BABA KUJIFIKIRI anavyozaliwa Mungu Mwana. Na kwa vile Mungu Baba hakuanza kufikiri juzi au jana bali tangu milele, Mungu Mwana ni Mungu pia tangu milele na hivyo ana umungu sawa na Baba. Ni Mungu kweli kutoka kwa Mungu kweli. Haya ndiyo yanayojumlishwa na maelezo ya somo la kwanza. Mungu Mwana ndiye aliyekuwa na Mungu Baba katika mwanzo wa njia yake na kabla ya matendo yake ya kale. Ndiye aliyetukuka tokea milele, tangu awali, kabla haijawako dunia. Ndiye aliyezaliwa kabla havijakuwako vilindi na kabla hazijakuwako chemchemi zilizojaa maji.
Lakini Nafsi hizo mbili zinapodumu pamoja katika upendo, kule kupendana kwao ndiko kunakokuwa Nafsi ya tatu, ndiyo Roho Mtakatifu. Ndiyo maana huwa tunasema Roho Mtakatifu anatoka kwa Baba na Mwana na ana umungu mmoja sawa nao na hivyo kustahili kuabudiwa na kutukuzwa pamoja nao.
Umetingwa? Usitingwe. Kwa muhtasari maelezo haya ya kifalsafa ni kwamba Mungu Baba anapojifikiri, kule kufikiri kunakuwa uwapo, ndiye Mungu Mwana na kule kupendana kwa Mungu Baba na Mungu Mwana kunakuwa uwapo ambao ndio Roho Mtakatifu. Kwa nini inakuwa hivyo? Inakuwa hivyo kwa sababu kufikiri kwa Mungu hakuwi hewa na pia kupenda kwa Mungu hakuwi hewa isipokuwa matendo yote mawili yanakuwa UWAPO.
Mshonano wa haya usikupe taabu. Mungu ni mwema ametupatia mambo ya kutusaidia katika uelewa wa mambo yanayotinga akili zetu. Kwamba kitu kinaweza kuwa kimoja katika utendaji wakati kuna vitu kadhaa visivyoweza kubaguliwa na kutenganishwa kunaelezeka katika picha kadhaa zisizokuwa ngeni kwetu. Acha tuziweke mbele yetu picha nne.
Mosi, sote tumewahi kuona majani yenye malepe. Jani hata likiwa na malepe mangapi hubaki kuwa moja ilmradi kikonyo kinabaki kimoja. Ndivyo unavyolingana na Utakatifu, umungu mmoja katika sura tatu zilizo sawa.
Pili, sisi Waafrika tunayajua meko zetu za mafiga. Jiko linakuwa moja ijapokuwa huwako mafiga matatu. Mafiga yale matatu hajafanyi meko tatu bali jiko moja ambalo ushikilia chombo chochote kinachoinjikwa juu yake katika kona tatu zenye utendaji na umuhimu sawa.
Tatu, sisi sote tunajijua chai. Chai inakuwa chai kwa sababu ya mambo matatu yenye umuhimu sawa: maji, majani ya chai na sukari. Mambo haya yakikutanishwa pamoja yanajenga chai na moja wapo lolote likikosekana chai huwa haipo. Huwezi kupata chai, kimojawapo kati ya hivyo vitatu kikikosekana. Kama unabisha jaribu kuwa na vitu viwili tu huite chai pasipo kuonekana “chizi.”
Nne na mwisho, sisi sote tunazijua sura za binadamu. Sura za binadamu ni mfano mzuri wa utendaji na mjengo wa Utatu Mtakatifu. Kwenye sura ya binadamu, itafakari leo, juu kuna macho yanayong’aa katika kuona na kutambua, hayo ni sawa na Mungu Baba anayeona na kutambua yote. Chini ya sura kuna kinywa kinachofunua na kuyasema yaliyomo ndani ya mtu, kinywa kinafanana kabisa na Mungu Mwana anayefunua mambo ya Mungu na kuyanena vyema. Mungu Mwana ni Neno. Hatimaye, kati ya macho na kinywa kuna kitu kitulivu, pua, inayotia uhai mwili mzimaa. Pua inalingana kabisa na Roho Mtakatifu Bwana na mleta uzima.
Tukijumlisha tuliyoyasema tuambizane jambo lifuatalo. Kwa kuwa sisi tumeumbwa na Mungu anayeishi katika Utatu Mtakatifu usiogawanyika, Utatu Mtakatifu uwe darasa letu la kujifunzia umoja, upendo na ushirikiano usio na unafiki. Kifupi, kwa mfano wa Utatu Mtakafitu tuungane pasipo kutengana. Binadamu lazima tumsadifu aliyetuzaa. Mifarakano katika familia, vigango, parokia, nchi na dunia ni aibu sana hasa kwa sisi Wakristo ambao fundisho la Utatu Mtakatifu ni letu hasa.

SALA: Ee Utatu Mtakatifu tufundisheni umoja na upendo kama ninyi Nafsi mnavyoishi kwa umoja na upendo kiasi kwamba hamwezi kutenganishwa. Amina.