Juni 9,2022; Alhamisi: Juma La 10 La Mwaka

Mt. Efrem, Shemasi na Mwalimu wa Kanisa
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: 1Fal. 18:41-46

Eliya alimwambia Ahabu, “Haya! Inuka, ule, unywe; kwani pana sauti ya mvua tele.” Basi Ahabu akainuka ili ale na kunywa. Naye Eliya akapanda juu mpaka kilele cha Karmeli; akasujudu kifudifudi, akainama uso mpaka magotini. Akamwambia mtumishi wake, “Kwea sasa, utazame upande wa bahari.” Akakwea, akatazama, na kusema, “Hakuna kitu.” Naye akanena, “Enenda tena mara saba.” Ikawa mara ya saba akasema, “Tazama, wingu linatoka katika bahari, nalo ni dogo kama mkono wa mtu.” Akanena, “Enenda, umwambie Ahabu, ‘Tandika, ushuke, mvua isikuzuie.’” Ikawa, muda si muda, mbingu zikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, ikanya mvua nyingi. Ahabu akapanda garini, akaenda zake Yezreeli. Mkono wa Bwana ulikuwa juu ya Eliya; akajikaza viuno, akapiga mbio mbele ya Ahabu mpaka kuingia Yezreeli.

(K) Ee Mungu, sifa zakuilaki katika Sayuni. Zab. 65:9-12

INJILI: Mt. 5:20-26

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue; na mtu akiua, itampasa hukumu.” Bali mimi nawaambieni, ‘Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto. Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako , upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako. Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani.’” Amin, nakuambia, “Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho.”

TAFAKARI
WEMA WENU UYAZIDI MALIMWENGU: Nabii Eliya baada ya kuhangaishwa na Mfalme Ahabu hadi kukimbia na kuishi kwenye upweke na kwa msaada wa mwanamke wa Serapta, anarudi tena na kwa moyo wa ibada anapanda hadi kilele cha Mlima Karmeli kuomba mvua. Hakufanikiwa hadi mara ya saba. nabii Eliya anaonyesha wema mkuu kuiombea mvua kwa muda mrefu nchi iliyomhangaisha. Hakuhifadhi uadui moyoni mwake. Anaonyesha umuhimu wa msamaha na msisitizo katika sala. Kristo anafundisha kwamba wema wa wafuasi wake uzidi ule wa Mafarisayo na waandishi. Watende mema kutoka mioyoni mwao na wala sio kwa kuiiga sheria tu.
Ili kuwa wasafi wa moyo na kuuangazia ulimwengu kwa wema wetu, inatulazimu kutumia muda wa kutosha kwenye tafakari na sala bila kuchoka. Inatulazimu pia kumaliza chuki na uhasama kati yetu, ili Mungu asikilize sala zetu.

SALA: Ee Bwana, utujalie tuyainjilishe malimwengu kwa matendo yetu mema.