Juni 8,2022 Jumatano: Juma La 10 La Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO I: 1Fal. 18:20-39

Ahabu alipeleka watu kwa wana wa Israeli wote, akawakusanya manabii pamoja katika mlima wa Karmeli. Naye Eliya akawakaribia watu wote, akanena, “Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini? Bwana akiwa ndiye Mungu, mfuateni; bali ikiwa Baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye.” Wale watu hawakumjibu neno. Ndipo Eliya akawaambia watu, “Mimi nimesalia, mimi peke yangu, nabii wa Bwana; lakini manabii wa Baali ni watu mia nne na hamsini. Kwa hiyo na watutolee ng’ombe wawili; wao na wajichagulie ng’ombe mmoja, wamkatekate na kumweka juu ya kuni, wasitie moto chini; nami nitamtengeza huyo ng’ombe wa pili, na kumweka juu ya kuni, wala sitatia moto chini. Nanyi ombeni kwa jina la mungu wenu, nami nitaomba kwa jina la Bwana; na Mungu yule ajibuye kwa moto, na awe ndiye Mungu.” Watu wote wakajibu wakasema, “Maneno haya ni mazuri.” Eliya akawaambia manabii wa Baali, “Jichagulieni ng’ombe mmoja, mkamtengeneze kwanza; maana ninyi ndio wengi; mkaliitie jina la mungu wenu, wala msitie moto chini.” Wakamtwaa yule ng’ombe waliyepewa, wakamtengeneza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri, wakisema, “Ee Baali, utusikie.” Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu. Nao wakaruka-ruka juu ya madhabahu waliyoifanya. Ikawa, wakati wa adhuhuri, Eliya akawafanyia dhihaka, akasema, “Mwiteni kwa sauti kuu; maana ni mungu huyo; labda anazungumza, au ana shughuli, au anasafiri, au labda amelala, sharti aamshwe.” Wakapiga kelele wakajikata-kata kwa visu na nyembe kama ilivyo desturi yao, hata damu ikawachuruzika. Ikawa, wakati wa adhuhuri ulipopita, walitabiri hata wakati wa kutoa dhabihu ya jioni; lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala aliyeangalia. Kisha Eliya akawaambia watu wote, “Nikaribieni mimi.” Watu wote wakamkaribia. Akaitengeneza madhabahu ya Bwana iliyovunjika. Eliya akatwaa mawe kumi na mawili, kwa hesabu ya kabila za wana wa Yakobo, aliyejiliwa na neno la Bwana na kuambiwa, jina lako litakuwa Israeli. Naye akaijenga madhabahu ya Bwana kwa mawe hayo katika jina la Bwana; akafanya mfereji, kama wa vipimo viwili vya mbegu, ukiizunguka madhabahu. Kisha akazipanga zile kuni, akamkata yule ng’ombe vipande vipande, akaviweka juu ya kuni. Akasema, “Jazeni mapipa manne maji, mkayamwage juu ya sadaka ya kuteketezwa, na juu ya kuni.” Akasema, “Fanyeni mara ya pili.” Wakafanya mara ya pili. Akasema, “Fanyeni mara ya tatu.” Wakafanya mara ya tatu. Yale maji yakaizunguka madhabahu; akaujaza mfereji maji. Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, “Ee Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie.” Ndipo moto wa Bwana ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji. Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi wakasema, “Bwana ndiye Mungu, Bwana ndiye Mungu.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 16:1-2, 4-5, 8, 11

 1. Mungu, unihifadhi mimi,
  Kwa maana nakukimbilia Wewe.
  Nimemwambia Bwana, ndiwe Bwana wangu,
  Sina wema bali utokao kwako.

(K) Mungu, unihifadhi mimi, kwa maana nakukimbilia Wewe.

 1. Huzuni zao zitaongezeka
  Wambadilio mungu kwa mwingine;
  Sitazimimina sadaka zao za damu,
  Wala kuyataja majina yao midomoni mwangu. (K)
 2. Bwana ndiye fungu la posho langu,
  na la kikombe changu;
  Wewe umeishikakura yangu.
  Nimemweka Bwana mbele yangu daima,
  Kwa kuwa yako kuumeni kwangu sitaondoshwa. (K)
 3. Utanijulisha njia ya uzima
  Mbele za uso wako ziko furaha tele.
  Nakatika mkono wako wa kuume,
  Mna mema ya milele. (K)

INJILI: Mt. 5:17-19

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Msidhani ya kuwa nalikuja kutangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.” Kwa maana, amin, nawaambia, “Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie. Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.”

TAFAKARI
MTASITA MPAKA LINI? Yesu anafundisha kwamba hakuja kutengua amri ila kutimiza na anaonya dhidi ya kuvunja amri. Amri ya kwanza ya Mungu inasisitiza, ‘usiabudu miungu wengine.’ Nabii Elia anakabiliana na taifa la Israeli wanaoshawishika kumfuata Baali kama mungu wao. ‘Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini ?’ Baada ya manabii 450 wa Baali kushindwa zoezi alilowapa, Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo anamjibu kwa muujiza wote wakishuhudia. Haya yanahimiza tena mafundisho ya Kristo aliyefundisha kwamba hatuwezi kuwatumikia mabwana wawili.
Ufuasi wa Kristo unalazimu kujitoa bila kujibakiza wala kujigawa. Wapo Wakristo waliokomalia ibada na tamaduni potofu za jadi. Wengine ni imani vuguvugu na nyepesi inayopeperushwa na kila dhoruba. Wengine ni kuiacha kabisa imani kwa changamoto za kupita. Tutasita hadi lini ?

SALA: Ee Mungu, utujalie kuona matendo yako katika maisha yetu na ndani ya Kanisa kupitia watumishi wako, tukuamini bila kusita.