Juni 7,2022 Jumanne: Juma La 10 La Mwaka Kijani

Zaburi: Juma 4
SOMO I: 1Fal. 17:7-16

Baada ya siku kupita, kile kijito kikakauka, kwa sababu mvua haikunya katika nchi. Neno la Bwana likamjia Eliya, kusema, “Ondoka, uende Sarepta, uliko mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe.” Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, “Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa.” Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, “Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako.” Naye akasema, “Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe.” Eliya akamwambia, “Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, ‘Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi.’” Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 4:1-4, 6-7

 1. Ee Mungu wa haki yangu, uniitikie niitako;
  Umenifanyizia nafasi wakati wa shida;
  Umenifadhili na kusikia sala yangu.
  Enyi wanadamu,
  Hata lini utukufu wangu utafedheheka?

(K) Bwana, utuinulie nuru ya uso wako.

 1. Bali jueni ya kuwa Bwana amaejiteulia mtauwa:
  Bwana atasikia nimwitapo.
  Mwe na hofu wala msitende dhambi,
  Tafakarini vitandani mwenu na kutulia. (K)
 2. Wengi husema, Nani atakayetuonyesha mema?
  Bwana utuinulie nuru ya uso wako.
  Umenitia furaha moyoni mwangu,
  Kupita yao wanapozidishiwa nafaka na divai. (K)

INJILI: Mt. 5:13-16

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.”

TAFAKARI
NURU YENU IANGAZE : Nabii Eliya hakusikilizwa na mfalme Ahabu aliyetarajiwa kuwa na ufahamu wa Mungu. Anaelekezwa kwa mwanamke wa Serapta, wa mataifa, na anamhudumia kwa ukarimu. Wanakutana watu wawili wenye matatizo na wanafarijiana. Eliya ana njaa na anaomba chakula, naye yule mama anamalizia chakula chake cha mwisho. Yule mwanamke anamlisha chakula nabii, naye nabii anampa matumaini ya kuishi kwa kuzidisha chakula chake. Kristo anawafundisha mitume kuwa wao ni chumvi na nuru ya kuangazia ulimwengu. Tukio la Eliya na mwanamke wa Serapta ni mfano hai wa nuru na chumvi vinavyowafaidi wanaokutana navyo. Kila mmoja anakuwa chachu na mwanga kwa mwenzake.
Tuyapokee mafundisho ya Yesu ya kuwa chumvi na mwanga wa ulimwengu hasa tukizingatia giza lililotutawala na ukosefu wa ladha ulio ndani mwetu.

SALA: Ee Yesu, neno lako liwashe mwanga na kurudisha ladha ya maisha ndani mwetu, ili tuwafaidi tunaokutana nao.