Mt. Norberti, Askofu
Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO I: 1 Fal. 17:1-6
Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu. Neno la Bwana likamjia, kusema, Ondoka hapa, geuka, uende upande wa mashariki, ujifiche karibu na kijito cha Kerithi kinachokabili Yordan. Itakuwa utakunywa maji ya kile kijito; nami nimewaamuru kunguru wakulishe huko. Basi akaenda akafanya kama alivyosema Bwana; kwa kuwa akaenda akakaa karibu na kijito cha Kerethi, kinachokabili Yordani. Kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, na mkate na nyama jioni, akanywa maji ya kile kijito.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 121:1-8
- Nitayainua macho yangu niitazame milima;
Msaada wangu utatoka wapi?
Msaada wangu u katika Bwana,
Aliyezifanya mbingu na nchi.
(K) Msaada wangu u katika Bwana,
aliyezifanya mbingu na nchi.
- Asiuache mguu wako usogezwe;
Asisinzie akulindaye;
Naam hatasinzia wala hatalala usingizi,
Yeye alaiye mlinzi wa Israeli. (K) - Bwana ndiye mlinzi wako;
Bwana ni uvuli mkono wako wa kuume.
Jua halitakupiga mchana,
Wala mwezi wakati wa usiku. (K) - Bwana atakulinda na mabaya yote,
Atakulinda nafsi yako.
Bwana atakulinda utokapo na uingiapo,
Tangu sasa n ahata milele. (K)
INJILI: Mt. 5:1-12
Yesu alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia; akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema, “Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika. Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi. Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa. Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema. Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu. Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia, kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.”
TAFAKARI
HERI KUU ZA WATEULE: Eliya nabii wa Mungu anamkemea bila woga na kumuonya mfalme Ahabu dhidi ya kujitajirisha na kustarehe kwa jasho la wanyonge. Inamlazimu kukimbilia kwenye upweke, na huko Mungu anamhudumia. Yesu anaanza utume wake kwa kuwatangazia nafuu wenye heri nane; maskini wa roho, wenye huzuni, wapole, wenye njaa na kiu ya haki, wenye rehema, moyo safi, wapatanishi, na wenye kuudhiwa na kunenewa mabaya. Hili ndilo kundi la watu walioishi kwa matumaini ya kupata unafuu, na ambao Kristo anawaletea Habari Njema. Anawahubiria kuwa ufalme wa Mungu ni wao, watashibishwa, watapata rehema, watamuona Mungu na mengineo. Huku akiwafariji na kuwasemea wanyonge, matumaini anayowapa ni makuu yasioyokuwa na mwisho na yasiyokuwa ya ulimwengu. Habari Njema inafariji na kutupa matumaini ya nyakati njema zijazo. Pia inawatahadharisha watawala na viongozi wasiowathamini wanaowaongoza.
SALA: Ee Mungu, tujalie kutamani mambo ya mbingu na ya kudumu.