Juni 5,2022; Jumapili: Jumapili Ya Pentekoste

Sherehe
Nyekundu
Zaburi: Tazama sala ya siku
SOMO 1: Mdo. 2:1-11

Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, “Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? Waparthi na Wamedi na Waelami, nao Wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kerene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 104:1, 24, 29-31, 34

 1. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
  Wewe, Bwana, Mungu wetu,
  Umenifanya mkuu sana;
  Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako!
  Dunia imejaa mali zako.

K: Waipeleka roho yako, Ee Bwana,
Nawe waufanya upya uso wa nchi.

 1. Waiondoa pumzi yao, wanakufa,
  Na kuyarudia mavumbi yao,
  Waipeleka roho yako, wanaumbwa,
  Nawe waufanya upya uso wa nchi. (K)
 2. Utukufu wa Bwana na udumu milele;
  Bwana na ayafurahie matendo yake.
  Kutafakari kwangu na kuwe kutamu kwake;
  Mimi nitamfurahia Bwana. (K) SOMO 2: 1 Kor. 12:3b-7, 12-13 Hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu. Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.

SHANGILIO

Aleluya, aleluya,
Uje Roho Mtakatifu,
Uzienee nyoyo za waamini wako uwatie mapendo yako.
Aleluya.

INJILI: Yn. 20:19-23

Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, “Amani iwe kwenu.” Naye akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana. Basi Yesu akawaambia tena, “Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi.” Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.”

TAFAKARI
WATU WATUSIKIE KWA LUGHA ZAO WENYEWE: Wazo hili liko wazi wazi katika masomo ya leo lakini likiwa wazi zaidi katika somo la kwanza. Somo hilo linasimulia jinsi neno la Mungu lilivyowafikia mamia ya watu waliokusanyika mjini Yerusalemu kwa sikukuu ya Pentekoste, sikukuu mojawapo kati ya tatu ambazo kadiri ya torati zilikuwa ni za lazima kuadhimishwa na Wayahudi wanaume wote mjini Yerusalemu. Sikukuu zingine zilikuwa Pasaka na Sikukuu ya Vibanda. Sikukuu hizi tatu zilikuwa zinafurikisha watu mjini Yerusalemu. Zote zilikuwa sikukuu za kuadhimishwa siku saba saba.
Kwa Pasaka walikuwa wanakumbuka jinsi mkono wa nguvu wa Mungu ulivyowakomboa kutoka kwenye utumwa wa Farao huko Misri. Siku hamsini baadaye, ndiyo maana ya neno Pentekoste, walisherehekea hiyo Pentekoste wakikumbuka jinsi taifa lao lilivyoasisiwa wakipewa amri kumi za Mungu na wao wakaashiria kwa kutolea mazao ya kwanza. Sikukuu ya vibanda ilikuwa ikiadhimishwa kukumbuka jinsi walivyoishi katika mabanda na mahema huko jangwani, na waliadhimisha kwa kujenga na kulala nje vibandani na mahemani. Kwa jinsi hii, ni bayana watu waliokusanyika Yerusalemu walitokea kutoka sehemu mbalimbali za mtawanyiko (diaspora). Wayahudi walikuja kwa lazima ya kidini lakini pamoja nao walikuja watu wa makabila mbalimbali kwa kujibanza kwenye sikukuu hiyo na hata wengine labda walikuja kwa kuitumia sikukuu yenye watu wengi kama hiyo kama fursa ya biashara.
Mintarafu lugha wasio Wayahudi kwa vyovyote walikuwa na lugha za mama zao lakini hata Wayahudi waliolowea kukaa nchi za kigeni walizoea zaidi lugha za huko walikotoka. Kwa maelezo haya kulikuwa na hitaji kubwa la lugha ya kuwaunganisha. Ndipo muujiza wa lugha ukatukizwa na Roho Mtakatifu. Mitume na wafuasi, jumla ya watu 120 wakajazwa na Roho Mtakatifu aliyewawezesha kusema lugha mbalimbali zilizosikika vyema na watu kila mtu kwa kadiri ya lugha yake mwenyewe. Jambo hili la ajabu liliwezesha watu kuyasikia makuu ya Mungu na kuchomwa mioyo. Mapato yake tunayajua. Watu walimuuliza mtume Petro wafanye nini naye Petro akawaalika watubu na kubatizwa. Wakabatizwa watu 3,000 na hivyo kuifanya jumuiya ya wafuasi wa Kristo ikue ghafla.
Somo la pili linatangaza kazi ya Roho Mtakatifu katika kuwafanya wanadamu waelewane na kufaidiana katika kutafutiana uzima wa milele. Awali ya yote anawawezesha watu kumkiri Yesu kama Bwana. Pili, anawagawia watu vipaji na karama mbalimbali. Tatu anawezesha huduma mbalimbali na nne anawatendesha watu kazi mbalimbali kusudi watu wafaidiane kama viungo vya mwili vinavyofaidishana katika kuwa tofauti na kufanya kazi tofauti tofauti. Lakini ajabu, mwili unapojengwa kwa viungo vyenye kazi mbalimbali hauvurugwi kwavyo bali ndivyo unavyozidi kuwa mmoja. Kanisa, ambalo ndio mwili wa Kristo, yeye akiwa kichwa na wabatizwa viungo vinavyojenga kiwilwili, ulipaswa usadifu utendaji wa mwili wa mtu na viungo vyake. Anayewezesha viungo visivurugane na kugongana ndiye Roho Mtakatifu. Jambo hilo anawezesha kwa kugawa vipaji na karama mbalimbali lakini zenye kujenga uelewano.
Injili inamng’arisha Mungu katika busara na mipango yake ya kututakia heri na kutuwezesha kusafiri kuelekea kwenye maskani yake. Katika mwendo huo anatuondolea hofu kwa kututakia tuishi katika amani na kutuasisia sakramenti ya Upatanisho (Kitubio) kwani anajua dhambi ni kitu kinachoparanyisha jamii hata kama zilinia mamoja. Katika hilo, Roho Mtakatifu ndiye mwezeshaji mkuu. Roho Mtakatifu ndiye nguzo ya sakramenti ya Kitubio na ndiyo maana anayepuuza au kumkufuru Roho Mtakatifu hufanya dhambi isiyoondoleka kwani anayempuuza au kumkufuru ndiye mwondoaji dhambi mwenyewe. Huyo hulingana na mtu anayeugua malaria na kukataa kwinini ambayo ndiyo dawa yake. Alahaula! Huyo hujipindua na kujiua mwenyewe.
Tuhitimishe maelezo yetu ifuatavyo. Mungu ametuumba watu wa mataifa mbalimbali (198 hivi), makabila (kwa mfano kama 120 nchini Tanzania, 43 Kenya), rangi, jamii na lugha mbalimbali (zaidi ya lugha 3200 duniani) tukiwasiliana katika sehemu na maeneo yetu mbalimbali. Ni sawa, na ni ishara ya kutupenda kama maua yanavyokuwa mengi na kuiletea bustani uzuri. Lakini kwa vile Mungu anakusudia kutuleta pamoja kwake watu wa kila taifa, ukoo, jamaa na lugha (Ufu 7:9) hana budi kutufanyia mambo yenye kutuelekeza kwenye mkusanyiko huo wa pamoja. Kazi hiyo ndiyo anayoishughulikia Roho Mtakatifu.
Kinyume chake, Roho Mtakatifu anatuwezesha kuelewana anapotugawia kwa ukarimu vipaji na karama zake na kuchochea ndani ya kila mwanadamu matunda ya roho: upendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Mambo haya yanapokuwapo na sisi tusisikie kwa lugha zetu wenyewe na kupata amani tuna shida ya kutustahilisha kutupwa jehanamu. Aheri tusikie na tutoe ushirikiano kwa Roho Mtakatifu kusudi watu wengine watusikie pia kwa lugha zao wenyewe. Lugha ya msamaha, upendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi ni ya kimataifa.

SLA: Ee Mungu Roho Mtakatifu, tunakushukuru kwa kuwa mkarimu kwetu unapotugawia kila mmoja vipaji na karama. Tunakuomba uwezeshe kwa hivyo kila mmoja kusikia makuu ya Mungu kwa lugha yake mwenyewe. Amina.