Juni 3,2022; Ijumaa: Juma La 7 La Pasaka

Wat. Karoli Lwanga na Wenzake, Mashahidi
Kumbukumbu
Nyeupe
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Mdo. 25:13-21

Siku zile, Agripa mfalme wa Bernike walifika Kaisaria, wakimwamkia Festo. Na walipokuwa wakikaa huko siku nyingi, Festo akamweleza mfalme habari za Paulo, akisema, “Yupo hapa mtu mmoja aliyeachwa na Feliki kifungoni; ambaye nilipokuwa Yerusalemu wakuu wa makuhani na wazee wa Wayahudi wakaniarifu habari zake, wakinitaka hukumu juu yake. Nikawajibu kwamba si desturi ya Warumi kumtoa mtu awaye yote, kabla mtu yule aliyeshitakiwa hajaonana na washitaki wake uso kwa uso, na kupewa nafasi ya kujitetea katika mashitaka yake. Basi walipokutanika hapa sikukawia; bali siku ya pili nikaketi katika kiti cha hukumu nikaamuru mtu huyo aletwe. Na wale waliomshitaki waliposimama hawakuleta neno lo lote baya, kama nilivyodhani, bali walikuwa na maswali mengine mengine juu yake katika dini yao wenyewe, na katika habari ya mtu mmoja Yesu, aliyekuwa amekwisha kufa, ambaye Paulo alikaza kusema kwamba yu hai. Nami nikaona shaka jinsi ya kutafuta hakika ya habari hii, nikamwuliza kama anataka kwenda Yerusalemu ahukumiwe huko katika mambo haya. Lakini Paulo alipodai kuwekwa ahukumiwe na Kaisari, nikaamuru alindwe hata nitakapompeleka kwa Kaisari.”

Wimbo Wa Katikati: Zab.103:1-2, 11-12, 19-20

 1. Ee nafso yangu, umhimidi Bwana.
  Naam, vyote vilivyo ndani yangu
  Vilihimidi jina lake takatifu.
  Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
  Wala usizisahau fadhili zake zote.

K: Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni.

 1. Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,
  Kadiri ileile rehema zake ni kuu kwa wamchao.
  Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
  Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. (K)
 2. Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni,
  Na ufalme wake unavitawala vitu vyote.
  Mhimidini Bwana, enyi malaika zake,
  Ninyi mlio hodari, mtendao neno lake,
  Mkiisikiliza sauti ya neno lake. (K)

INJILI: Yn. 21:15-19

Walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, “Je! Simoni wa Yohane, wewe wanipenda kuliko hawa?”| Akamwambia, “Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda.” Akamwambia, “Lisha wanakondoo wangu.” Akamwambia tena mara ya pili, “Simoni wa Yohane wanipenda?” Akamwambia, “Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda.” Akamwambia, “Chunga kondoo zangu.” Akamwambia mara ya tatu, “Simoni wa Yohane, wanipenda?” Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, “Wanipenda?” Akamwambia, “Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda.” Yesu akamwambia, “Lisha kondoo zangu.” Akasema, Amin, amin, nakuambia, “Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka.” Akasema neno hilo kwa kuonyesha ni kwa mauti gani atakayomtukuza Mungu. Naye akiisha kusema hayo, akamwambia, “Nifuate.”

TAFAKARI
JE WANIPENDA? NIFUATE: Mara tatu mfululizo, Yesu Kristo anamhoji Simoni Petro kuhusu upendo wake. Kwa kujibu mara tatu kwa msisitizo tofauti, Mtume Petro anathibitisha upendo wa dhati kwa Kristo na anashuhudia upendo huo. Mtume Paulo anabaki imara anapohangaishwa na watesi wake kuhusu ufufuo wa Kristo, ishara wazi ya utume aliopewa na Kristo kwa upendo wake kwake. Upendo ndicho kiungo cha pekee na cha lazima kinachowaunganisha waliotumwa, aliyemtuma na aliyetumwa kwake. Mahojiano kati ya Kristo na Petro yanathibitisha upendo wa Petro anayetumwa, kwa Kristo anayetumwa na kwa wafuasi anaotumwa kwao. Uchungaji ni tendo linaloanzishwa na kudumishwa na upendo. Mchungaji haendi apendapo na kutenda apendalo, bali anatenda alivyoagizwa.
Watumishi wa Mungu lazima waunganishwe kwake kwa upendo thabiti, na wawe tayari kulilinda kundi walilokabidhiwa na kulionyesha upendo wa Mungu.

SALA: Ee Yesu, uwajalie watumishi wako upendo wa dhati kwako na kwa kundi wanalolihudumia.