Juni 2,2022; Alhamisi: Juma La 7 La Pasaka

Wat. Marselino na Petro, Mashahidi
Nyeupe
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Mdo. 22:30;23:6-11

Wakati ule Jemadari alitaka kujua hakika, ni kwa sababu gani Paulo ameshitakiwa na Wayahudi, akamfungua, akawaamuru wakuu wa makuhani na baraza yote wakutane. Akamleta Paulo chini, akamweka mbele yao. Paulo alipotambua ya kuwa sehemu moja ni Masadukayo, na sehemu ya pili ni Mafarisayo, akapaza sauti yake katika ile baraza, ndugu zangu, mimi ni Farisayo, mwana wa Farisayo; mimi ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini la ufufuo wa wafu. Alipokwisha kunena hayo palikuwa na mashindano baina ya Mafarisayo na Masadukayo, mkutano ukafarakana.

Kwa maana Masadukayo husema ya kwamba hakuna kiyama wala malaika wala roho; Bali Mafarisayo hukiri yote. Pakawa na makelele mengi. Waandishi wengine wa upande wa Mafarisayo wakasimama, wakateta, wakisema, hatuoni uovu wowote katika mtu huyu; bali ikiwa roho au malaika amesema naye, ni nini? Ugomvi mkubwa ulipotokea, yule jemadari akachelea Paulo asije akararuliwa nao, akaamuru askari washuke na kumwondoa kwa nguvu mikononi mwao, na kumleta ndani ya ngome. Usiku ule Bwana akasimama karibu naye, akasema, “Uwe na moyo mkuu; kwa sababu, kama ulivyonishuhudia habari zangu Yerusalemu, imekupasa kunishuhudia vivyo hivyo Rumi nako.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 16:1-2, 7-11

 1. Mungu unihifadhi mimi,
  Kwa maana nakukimbilia Wewe.
  Nimemwambia Bwana, ndiwe Bwana wangu,
  Sina wema ila utokao kwako.

K: Mungu unihifadhi mimi,
Kwa maana nakukimbilia Wewe.

 1. Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri,
  Naam, mtima wangu umenifundisha usiku.
  Nimemweka Bwana mbele yangu daima,
  Kwa kuwa yako kuumeni kwangu, sitaondoshwa. (K)
 2. Kwa hiyo moyo wangu unafurahi,
  Nao utukufu wangu unashangilia,
  Naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini.
  Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu,
  Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu. (K)
 3. Utanijulisha njia ya uzima;
  Mbele za uso wako ziko furaha tele;
  Na katika mkono wako wa kuume
  Mna mema ya milele. (K)

INJILI: Yn. 17:20-26

Siku ile, Yesu alisali akisema: “Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi. Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu. Baba mwenye haki, ulimwengu haukukujua; lakini mimi nalikujua, na hao wamejua ya kuwa ndiwe uliyenituma. Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao.”

TAFAKARI
WAKAMILIKE KATIKA UMOJA: Yesu daima alionyesha umoja kamili na wa pekee uliopo kati yake na Mungu. Alipenda nasi pia tushiriki katika umoja huo kwa kuwa na umoja kati yetu sisi, kisha sisi pamoja naye. Umoja huu utakuwa ushuhuda mzito kwa ulimwengu kwamba Yesu Kristo alitoka kwa Mungu. Kristo amewashirikisha utukufu uliotoka kwa Baba ili wakamilike katika umoja. Anawaombea ili kwa umoja kati yao, wafike katika umoja na Baba alimo Yesu Kristo. Mafarakano kati ya Masadukayo na Mafarisayo kwenye mashtaka ya Mtume Paulo ni mfano wa kundi lililokosa umoja na linaloshuhudia kinyume na umoja katika mafundisho ya Kristo.
Umoja na ushirikiano kamili katika Kanisa unaleta maelewano kati yetu, unaunda mwili wa Kristo na kuushuhudia ulimwengu kuhusu umungu wa Yesu Kristo. Umoja pia unatushirikisha katika muungano kamili na Mungu, duniani na katika ufalme wake.

SALA: Ee Mungu, utuunganishe katika umoja na kweli.