Mei 31,2022; Jumanne: Juma la 7 la Pasaka

Bikira Maria kwenda kumwamkia Elizabeti
Sikukuu
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku
SOMO 1: Sef. 3:14-18
Imba, Ee binti Sayuni; piga kelele Ee Israeli; furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, Ee binti Yerusalemu. Bwana ameziondoa hukumu zako, amemtupa nje adui yako; mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; hutaogopa uovu tena. Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa, usiogope, Ee Sayuni; mikono yako isilegee. Bwana, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa; atakushangilia kwa furaha kuu, atatulia katika upendo wake. Atakufurahia kwa kuimba.

Wimbo Wa Katikati: Isa. 12:2-6

  1. Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu;
    Nitatumaini wala sitaogopa;
    Maana Bwana Yehova ni nguvu zangu na wimbo wangu;
    Naye amekuwa wokovu wangu.
    Basi, kwa furaha mtateka maji katika visima vya wokovu
    (K) Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako.
  2. Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake;
    Yatangazeni matendo yake kati ya mataifa,
    Litajeni jina lake kuwa limetukuka. (K)
  3. Mwimbieni Bwana; kwa kuwa ametenda makuu;
    Na yajulikane haya katika dunia yote.
    Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sayuni;
    Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako. (K)

INJILI: Lk. 1:39-56
Mariamu aliondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti. Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, “Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi? Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.” Mariamu akasema, “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu; Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa; Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu, Na jina lake ni takatifu. Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi Kwa hao wanaomcha. Amefanya nguvu kwa mkono wake; Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao; Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza. Wenye njaa amewashibisha mema, Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu. Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; Ili kukumbuka rehema zake; Kama alivyowaambia baba zetu, Ibrahimu na uzao wake hata milele.” Mariamu akakaa naye kadiri ya miezi mitatu, Kisha akarudi kwenda nyumbani kwake.

TAFAKARI
MWENYEZI MUNGU AMENITENDEA MAKUU: Adhimisho hili limesheheni furaha na shukrani kwa Mungu. Mama Bikira Maria kwa uchangamfu mkubwa, anamtembelea Elizabeti aliyejaliwa makuu ya kipekee. Huu ni mkutano sio tu wa Bikira Maria na ndugu yake Elizabeti, bali wanaunganika pia Yohane Mbatizaji anayehitimisha Agano la Kale na kutanguliza Agano Jipya, na Yesu Kristo anayefungua ukurasa mpya katika historia ya wokovu. Kanisa linatualika kutafakari kwa kina matukio ya kinabii yanayofanyika kupitia wanawake hawa wawili. Bikira Maria anamtafuta Elizabeti ili kumsimulia alivyomwambia malaika, akijua kwamba Elizabeti atamwamini na kumwelewa. Anampokea, anamsifia na kumsikiliza. Elizabeti kwa zamu yake anasimulia makuu Mungu aliyomjalia. Huu ni muunganiko wa mioyo miwili inayokutana na kushirikishana yaliyo ndani mwao.
Tujaliwe kuuona uzito wa tukio hili la kimungu, kinabii na kihistoria, Mungu anapotimiza ahadi yake iliyosubiriwa vizazi vingi.

SALA. Ee Mungu, utufungue mioyo, tutafakari na kuelewa makuu ya wokovu wako.