Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Mdo. 19:1-8
Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko; akawauliza, “Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini?” Wakamjibu, “La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia.” Akawauliza, “Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani?” Wakasema, “Kwa ubatizo wa Yohane.” Paulo akasema, “Yohane alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye anayekuja nyuma yake, yaani, Yesu.” Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri. Na jumla yao walipata wanaume kumi na wawili. Akaingia ndani ya sinagogi, akanena kwa ushujaa kwa muda wa miezi mitatu, akahojiana na watu, na kuwavuta katika mambo ya ufalme wa Mungu.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 68:1-6
- Mungu huondoka, adui zake wakatawanyika,
Nao wamchukiao huukimbia uso wake.
Kama moshi upeperushwavyo,
Ndivyo uwapeperushavyo wao;
Kama nta iyeyukavyo mbele ya moto,
Ndivyo waovu wapoteavyo usoni pa Mungu.
K: Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu. - Bali wenye haki hufurahi,
Na kuushangilia uso wa Mungu,
Naam, hupiga kelele kwa furaha.
Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake,
Shangilieni mbele zake. (K) - Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane,
Mungu katika kao lake takatifu.
Mungu huwakalisha wapweke nyumbani;
Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa;
Bali wakaidi hukaa katika nchi kavu. (K)
INJILI: Yn. 16:29-33
Wanafunzi walimwambia Yesu: “Tazama, sasa wasema waziwazi, wala huneni mithali yo yote. Sasa tumejua ya kuwa wewe wafahamu mambo yote wala huna haja ya mtu akuulize; kwa hiyo twasadiki ya kwamba ulitoka kwa Mungu.” Yesu akawajibu, “Je! Mnasadiki sasa? Tazama, saa yaja, naam, imekwisha kuja ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao kwao, na kuniacha mimi peke yangu; walakini mimi si peke yangu, kwa kuwa Baba yupo pamoja nami. Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.”
TAFAKARI
YESU AMEUSHINDA ULIMWENGU : Mtume Paulo anawabatiza watu tena waliobatizwa kwa ubatizo wa Yohane. Mara wanajazwa na Roho Mtakatifu. Ubatizo wa Yohane ulikuwa wa toba ; yaani mtu mwenyewe anafanya uamuzi wa kubadilisha maisha yake, awezavyo. Ubatizo kwa jina la Yesu Kristo unatuongezea uhai mpya wa kiroho unaotokana na Roho Mtakatifu. Zaidi ya toba kwa Ubatizo, Kristo anatujalia nguvu mpya ya kupigana vita vya kiroho. Mbatizwa anaishi sio tu kwa juhudi za kimwili, mbali anaukuza uzima wake wa kiroho. Kimwili yupo bado ulimwenguni, lakini kiroho yupo katika Mungu. Ni kwa Nguvu hiyo, ambapo Kristo aliushinda ulimwengu.
Ubatizo kwa jina la Yesu Kristo unatujalia kuzaliwa katika roho. Tunakuwa wenyeji wa mbinguni, tukiwa bado ulimwenguni. Hivyo tunaweza kushinda mapambano ya kimwili kwa msaada wa roho wa Mungu aliye ndani yetu.
SALA:Ee Bwana, uwajalie wabatizwa kuushinda ulimwengu kwa msaada wa Roho wako.