SOMO 1: Mdo. 1:1-11
Kitabu kile cha kwanza nalikiandika, Theofilo, katika habari ya mambo yote aliyoanza Yesu kufanya na kufundisha, hata siku ile alipochukuliwa juu, alipokuwa amekwisha kuwaagiza kwa Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua; wale aliowadhihirishia nafsi yake, kwa dalili nyingi, baada ya kuteswa kwake, ya kwamba yu hai, akiwatokea muda wa siku arobaini, na kuyanena mambo yaliyouhusu ufalme wa Mungu. Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu; ya kwamba Yohane alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache. Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, “Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme?” Akawaambia, “Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalem, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” Akiisha kusema hayo, walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao. Walipokuwa wakikaza macho mbinguni, yeye alipokuwa akienda zake, tazama, watu wawili wakasimama karibu nao, wenye nguo nyeupe, wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.”
Wimbo Wa Katikati: Zab. 47:1-2, 5-6, 7-8
- Enyi watu wote, pigeni makofi,
Mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe,
Kwa kuwa Bwana Aliye juu, mwenye kuogofya,
Ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote.
(K) Mungu amepaa kwa kelele za shangwe,
Bwana kwa sauti ya baragumu. - Mungu amepaa kwa kelele za shangwe,
Bwana kwa sauti ya baragumu.
Mwimbieni Mungu, naam, imbeni;
Mwimbieni mfalme wetu, naam, imbeni. (K) - Maana Mungu ndiye mfalme wa dunia yote,
Imbeni kwa akili
Mungu awamiliki mataifa,
Mungu ameketi katika kiti chake kitakatifu. (K)
SOMO 2: Efe 1:17-23
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.
SHANGILIO Mt. 28:19-20
Aleluya, aleluya,
Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote.
Aleluya.
INJILI: Lk. 24:46-53
Yesu aliwaambia wafuasi wake, “Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya. Na, tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu. Akawaongoza mpaka Bethania, akainua mikono yake akawabariki. Ikawa katika kuwabariki, alijitenga nao; akachukuliwa juu mbinguni.” Wakamwabudu; kisha wakarudi Yerusalemu wenye furaha kuu. Nao walikuwa daima ndani ya hekalu, wakimsifu Mungu.
TAFAKARI
TUMESHUHUDIWA KUSUDI NASI TUSHUHUDIE INJILI: Leo ni sherehe kubwa ya kupaa Bwana wetu mbinguni. Kupaa kwake mbinguni kunamaanisha kurudia kwake utukufu wake wa kimungu. Ni kurejea kwa ushindi kutoka shughuli hizi za kuwakomboa wanadamu, shughuli ambazo zilianza kwa kujimwilisha kwake (Krismasi) na kufikia kilele chake kwa mateso msalabani, kufa na kufufuka (karamu ya mwisho hadi Pasaka). Kwamba anapaa mbinguni baada ya siku arobaini haimaanishi siku za kuhesabu kitarakimu. Arobaini maana yake kipindi cha kutosha kukamilisha jambo. Hivi Yesu alijipatia muda wa kutosha kukamilisha suala la kujitambulisha kwa wafuasi wake kwamba aliyefufuka ni yeye yule aliyewahi kutiwa mbaroni, akateswa, kufa na kuzikwa. Ndiyo maana katika kipindi cha kujitokeza kwa wanafunzi wake alijitahidi kujieleza kwa maneno na matendo kwamba ni Yesu yule yule waliyemfahamu kabla. Kwa kuwa alikuwa anamaliza kazi na kuwakabidhi kazi mitume na wafuasi wake akawahakikishia kwamba atawapa na nguvu ya kutekelezea wito na utume wao. Alisema atawapa Roho Mtakatifu ili kwa nguvu zake waweze kutangaza Injili hadi mwisho wa dunia.
Yesu aliwashuhudisha mitume mambo mbalimbali kwa maneno na matendo. Wakashuhudishwa hivyo hata Yesu alipokufa. Baada ya ufufuko aliwashuhudisha hadi siku ya kupaa kwake mbinguni. Hatimaye, siku ya Pentekoste mitume walipewa nguvu ya Roho Mtakatifu wafaulu kufanya umisionari na Ukristo usambae hadi kuingia katika mabara yote kama tujuavyo leo. Kushuhudishwa huku pamoja na kutiwa nguvu ya Roho vyote vilikusudiwa kutuwezesha wanadamu tushuhudie Injili duniani kote. ndiyo maana tunasema tumeshuhudiwa kusudi nasi tushuhudie Injili.
Somo la kwanza, mwandishi anasema anachukua fursa ya kuandika kitabu cha Matendo ya Mitume ashuhudie mambo ya Yesu Kristo kwa msomaji au wasomaji. Ndipo anapoandika kwamba yuko tayari kushuhudia “habari ya mambo yote aliyoanza Yesu kufanya na kufundisha, hata siku ile alipochukuliwa juu, alipokuwa amekwisha kuwaagiza kwa Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua; wale aliowadhihirishia nafsi yake, kwa dalili nyingi, baada ya kuteswa kwake, ya kwamba yu hai, akiwatokea muda wa siku arobaini, na kuyanena mambo yaliyouhusu ufalme wa Mungu.” Mwenzetu anasema yuko tayari na ameamua kushuhudia habari za Yesu ili zifahamike bila shaka zikifahamika watu wampende Yesu na hatimaye waongoke na kuingia kwenye uzima wa milele.
Somo la pili linawatakia Waefeso, na kwa kupitia wao, sisi sote, wapate roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua Yesu Kristo; macho ya mioyo yao yatiwe nuru, wajue tumaini la mwito wa Kristo jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yao waaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake. Watu wakijua haya yote bila shaka watakuwa wameshuhudiwa na kwa kushuhudiwa hivyo wataichukua Injili hadi kona zote za dunia. Aheri wote tungekuwamo katika mradi huu. Tumwombe Mungu katika sherehe ya leo atuwezeshe wote kuwa mashahidi wa kazi ya ukombozi aliyotenda Yesu Kristo kwa ajili ya wanadamu wote. Hatimaye, mapato ya ushuhuda huo yawe kuupata sote uzima wa milele.
SALA: Ee Yesu Kristo uliwashuhudisha mitume habari za ukombozi ili wazishuhudie ulimwenguni. Unapokaa sasa katika utukufu wako mkono wa kuume wa Mungu utusaidie tuwe mashuhuda wazuri katika enzi zetu hizi. Amina.