Mei 26,2022; Alhamisi: Juma la 6 la Pasaka

Mt. Filipo Neri, Padre
Kumbukumbu
Nyeupe
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Mdo. 18:1-8
Siku zile, Paulo alitoka Athene akafika Korintho. Akamwona Myahudi mmoja, jina lake Akila, mzaliwa wa Ponto; naye amekuja kutoka nchi ya Italia siku za karibu, pamoja na Prisila mkewe, kwa sababu Klaudio amewaamuru Wayahudi wote watoke Rumi, naye akafikilia kwao; na kwa kuwa kazi yao ya ufundi ilikuwa moja, akakaa kwao, wakafanya kazi pamoja, kwa maana walikuwa mafundi wa kushona hema. Akatoa hoja zake katika sinagogi kila sabato, akajaribu kuwavuta Wayahudi na Wayunani. Hata Sila na Timotheo walipotelemka kutoka Makedonia, Paulo akasongwa sana na lile neno, akiwashuhudia Wayahudi ya kwamba Yesu ni Kristo. Walipopingamana naye na kumtukana, Mungu akakung’uta mavazi yake, akawaambia, “Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu; mimi ni safi; tangu sasa nitakwenda kwa watu wa mataifa.” Akaondoka huko akaingia katika nyumba ya mtu mmoja jina lake Tito Yusto, mcha Mungu, ambaye nyumba yake ilikuwa mpaka mmoja na sinagogi. Na Krispo, mkuu wa sinagogi, akamwamini Bwana pamoja na nyumba yake yote. Wakorintho wengi waliposikia, waliamini, wakabatizwa.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 98:1-4

 1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
  Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
  Mkono wa kuume wake mwenyewe,
  Mkono wake matakatifu umemtendea wokovu.
  (K)Bwana ameufunua wokovu wake,
  Machoni pa mataifa:
 2. Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
  Amezikumbuka rehema zake,
  Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)
 3. Miisho yote ya dunia imeuona
  Wokovu wa Mungu wetu.
  Mshangilieni Bwana, nchi yote,
  Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)

INJILI: Yn. 16:16-20
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni; na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona.” Basi baadhi ya wanafunzi wake wakasemezana, “Neno gani hilo asemalo, Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona? na hilo, Kwa sababu naenda zangu kwa Baba?” Basi walisema, “Neno gani hilo asemalo; hilo, Bado kitambo kidogo? Hatujui asemalo.” Yesu alifahamu ya kwamba wanataka kumwuliza, akawaambia, “Ndilo hilo mnaloulizana, ya kuwa nalisema, Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona? Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.”

TAFAKARI
WOKOVU KWA MATAIFA ; Wayahudi na wayunani wanapingana na Mtume Paulo kuhusu Yesu Kristo. Wanaposhindana, wachache wanakubali kubatizwa. Anawaonya na kuwageukia mataifa. Zaburi inamsifu Bwana kwa kuufunua wokovu kwa mataifa. Kristo anawaaga na kuwafariji mitume wake kwa maneno, ‘mimi nitawaona tena na mioyo yenu itafurahi.’ Mtume Paulo anawaunganisha Wayahudi na mataifa mengine kwa imani moja chini ya Yesu Kristo. Kristo anatangaza kurudi kwa Baba. Kuondoka kwake sio kuliacha kundi lake katika upweke, lakini anakuwa pamoja nao kwa namna tofauti. Kupaa kwake na kuketi kuume kwa Mungu Baba, analiunganisha kundi alilolikomboa na Mungu Baba. Mitume wanaunganisha mataifa kati yao, naye Kristo analiunganisha Kanisa na Mungu.
Utume wa kila mchungaji na kila mbatizwa ni kuliinjillisha na kuliunganisha kundi la Kristo, kwa kujiepusha kutengwa na dhambi, tamaa na mamlaka.

SALA: Ee Mungu, uyajalie mataifa kukufuata katika imani moja chini ya Mkombozi wetu aliyepaa kwako.