Mei 25,2022; Jumatano: Juma la 6 la Pasaka

Mt. Beda, Mhashamu, Padre na Mwalimu wa Kanisa/
Mt. Gregori VII Baba Mt./ Mt. Maria Magdalena wa Pazi, Bikira
Nyeupe
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Mdo. 17:15, 22-18:1
Siku zile, wale waliomsindikiza Paulo wakampeleka mpaka Athene; nao wakiisha kupokea maagizo kuwapelekea Sila na Timotheo, ya kwamba wasikawie kumfuata, wakaenda zao. Paulo akasimama katikati ya Areopago, akasema, “Enyi watu wa Athene, katika mambo yote naona ya kuwa ninyi ni watu wa kutafakari sana mambo ya dini kwa sababu nilipokuwa nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya, kwa Mungu asiyejulikana. Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua. Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono; wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote. Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao; ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu. Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda na kuwa na uhai wetu. Kama vile mmoja wetu, mtunga mashairi alivyosema, ‘Maana sisi sote tu wazao wake.’ Basi, kwa kuwa sisi tu wazao wa Mungu, haitupasi kudhani ya kuwa Uungu ni mfano wa dhahabu au fedha au jiwe, vitu vilivyochongwa kwa ustadi na akili za wanadamu. Basi, zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu. Kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu.” Basi waliposikia habari za ufufuo wa wafu wengine walifanya dhihaka; wengine wakasema, “Tutakusikiliza tena katika habari hiyo.”

Basi hivi Paulo akaondoka akawaacha. Baadhi ya watu wakashikamana naye, wakaamini; katika hao alikuwamo Dionisio, Mwareopago, na mwanamke mmoja jina lake Damari, na watu wengine pamoja na hao. Baada ya mambo hayo, Paulo akatoka Athene akafika Korintho.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 148:1-2, 11-14

  1. Aleluya.
    Msifuni Bwana kutoka mbinguni;
    Msifuni katika mahali palipo juu.
    Msifuni enyi malaika zake wote;
    Msifuni, majeshi yake yote.
    (K)Utukufu wako unajaza mbingu na ulimwengu.
  2. Wafalme wa dunia, na watu wote,
    Wakuu, na makadhi wote wa dunia.
    Vijana waume na wanawali,
    Wazee, na watoto. (K)
  3. Na walisifu jina la Bwana,
    Maana jina laki peke yake limetukuka;
    Adhama yake i juu ya nchi na mbingu. (K)
  4. Naye amewainulia watu wake pembe,
    Sifa za watauwa wake wote;
    Wana wa Israeli, watu walio karibu naye. (K)

INJILI: Yn. 16:12-15
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Bado ningali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa. Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza mimi; kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari. Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasha habari.”

TAFAKARI
ROHO ATAWAONGOZA KWENYE KWELI : Yesu anatambua wingi na uzito wa mafundisho yake kwa kulinganisha na uwezo wa mitume wake. Japo anayo mengi ya kuwafundisha, anakiri kwamba hawataweza kuyastahimili. Lakini ujio wa Roho Mtakatifu utakuwa kwao msaada mkubwa, kwani atawaongoza kwenye kweli kwa kuwafundisha na kuwakumbusha yatokayo kwa Mungu kupitia kwa Yesu Kristo. Mtume Paulo kwa kuongozwa na Roho wa Mungu anawasaidia watu wa Athene kutofautisha kati ya miungu waliowachonga na kuwaabudu, na ‘Mungu asiyejulikana’, muumba wa vyote. Ni Mungu hai asiyeishi ndani ya hekalu, na anayewashinikiza watu kumtafuta japo kwa kupapasa-papasa. Yupo daima karibu nasi kwa maana tunaishi ndani mwake.
Hekima ya kumjua Mungu ni kipaji cha Roho Mtakatifu anayetuelekeza kwenye kweli kama alivyoahidi Kristo. Mungu anatushawishi nasi ndani ya dhamiri zetu ili kumtafuta Yeye aliye wa kweli.

SALA: Ee Kristo, utupe Roho wako, Msaidizi atakayetuelekeza kumjua Mungu wa kweli.