Mei 24,2022; Jumanne: Juma la 6 la Pasaka

Nyeupe
Zaburi: Juma 1
SOMO I: Mdo. 16:22-34
Siku ile pale Filipi, wenyeji waliwakamata Paulo na Sila, wakawaendea, makadhi wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakatoa amri wapigwe kwa bakora. Na walipokwisha kuwapiga kwa mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana. Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale. Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa. Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia. Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, “Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa.” Akataka taa ziletwe, akarukia ndani, akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila; kisha akawaleta nje akasema, “Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.” Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake.
Akawakaribisha saa ile ile ya usiku, akawaosha mapigo yao, kisha akabatizwa, yeye na watu wake wote wakati huo huo. Akawaleta juu nyumbani kwake, akawaandalia chakula, akafurahi sana, yeye na nyumba yake yote, maana amekwisha kumwamini Mungu.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 138:1-3, 7-8

 1. Nitakushukuru kwa moyo wangu wote,
  Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
  Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu,
  (K)Utanyosha mkono, Ee Bwana, utaniokoa.
 2. Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako,
  Kwa maana umeikuza ahadi yako,
  Siku ile niliyokuita uliniitikia,
  Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu. (K)
 3. Utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu,
  Na mkono wako wa kuume utaniokoa.
  Ee Bwana, fadhili zako ni za milele;
  Usiziache kazi za mikono yako. (K)

INJILI: Yn. 16:5-11
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Sasa mimi naenda zangu kwake yeye aliyenipeleka, wala hakuna mmoja wenu aniulizaye, Unakwendapi? Ila kwa sababu nimewaambia hayo huzuni imejaa mioyoni mwenu. Lakini mimi nawambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke; kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu. Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu. Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi; kwa habari ya haki, kwa sababu mimi naenda zangu kwa Baba, wala hamnioni tena; kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.”

TAFAKARI
MSIHUZUNIKE, KWA IMANI MTAWEZA : Yesu anapowaaga mitume wake anaahidi kuwa pamoja nao na kuwatumia Msaidizi. Ahadi hii haikuwa kwa ajili ya kuwatuliza mioyo iliyohuzunika, lakini ilikuwa ni ahadi kweli. Kwenye uinjilishaji wao Paulo na Sila wanakamatwa, wanavuliwa nguo, wanapigwa fimbo na kutupwa gerezani. Lakini imani yao kwa Kristo iliwapa ujasiri wa kuendelea kumtukuza Mungu hata kifungoni. Kristo anaonyesha uwepo wake katika mateso yao anapowaondoa magerezani kwa muujiza, na kugeuza dhiki yao kuwa furaha ya kumuona mlinzi wao akiongoka. Kristo alidhihirisha msaada wake kwa mitume wanapohangaishwa kama alivyoahidi.
Changamoto za maisha mara nyingine zinatuweka katika huzuni kubwa. Lakini Kristo anatuhimiza kumwamini yeye na kutafuta msaada wa Roho Mtakatifu huku tukijitahidi kufanya tuwezavyo. Maana atakuja na kutuhangaikia tutakapomhitaji na kuigeuza dhiki kuwa fursa ya uinjilishaji na sababu ya Mungu kutukuzwa.

SALA: Ee Yesu, utujalie kukuamini na kukutumaini tunapokumbwa na huzuni moyoni.