SOMO 1: Mdo. 15:1-2, 22-29
Walishuka watu waliotoka Uyahudi wakawafundisha wale ndugu ya kwamba, Msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka. Basi baada ya Paulo na Barnaba kushindana na watu hawa na kuhojiana nao sana, ndugu wakaamuru kwamba Paulo na Barnaba na wengine miongoni mwao wapande kwenda Yerusalemu kwa mitume na wazee kwa habari ya swali hilo. Basi ikawapendeza mitume na wazee na kanisa lote kuwachagua watu miongoni mwao na kuwapeleka Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba; nao ni hawa, Yuda aliyeitwa Barsaba, na Sila, waliokuwa watu wakuu katika ndugu. Wakaandika hivi na kupeleka kwa mikono yao.
Mitume na ndugu wazee, kwa ndugu zetu walioko Antiokia na Shamu na Kilikia, walio wa Mataifa; Salamu. Kwa kuwa tumesikia ya kwamba watu waliotoka kwetu wamewasumbua kwa maneno yao, wakipotosha roho zenu, ambao sisi hatukuwaagiza; sisi tumeona vema, hali tumepatana kwa moyo mmoja, kuwachagua watu na kuwapeleka kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo, watu waliohatarisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Basi tumewatuma Yuda na Sila, watakaowaambia wenyewe maneno yayo hayo kwa vinywa vyao. Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima, yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. Wasalamu.
Wimbo Wa Katiukati: Zab. 67:1-5, 7
- Mungu na atufadhili na kutubariki,
Na kutuangazia uso wake.
Njia yake ijulikane duniani,
Wokovu wake katikati ya mataifa yote.
(K) Watu na wakushukuru, Ee Mungu,
Watu wote na wakushukuru.
- Mataifa na washangilie,
Naam, waimbe kwa furaha,
Maana kwa haki utawahukumu watu,
Na kuwaongoza mataifa walioko duniani. (K) - Watu na wakushukuru, Ee Mungu,
Watu wote na wakushukuru.
Mungu atatubariki sisi;
Miisho yote ya dunia itamcha Yeye. (K)
SOMO 2: Ufu. 21:10-14, 22-23
Siku ile, mimi Yohana, Nilichukuliwa katika Roho mpaka mlima mkubwa, mrefu, akanionyesha ule mji mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu; wenye utukufu wa Mungu, na mwangaza wake ulikuwa mfano wa kito chenye thamani nyingi kama kito cha yaspi, safi kama bilauri; ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu, wenye milango kumi na miwili, na katika ile milango malaika kumi na wawili; na majina yameandikwa ambayo ni majina ya kabila kumi na mbili za Waisraeli. Upande wa mashariki milango mitatu; na upande wa kaskazini milango mitatu; na upande wa kusini milango mitatu; na upande wa magharibi milango mitatu. Na ukuta wa mji ulikuwa na misingi kumi na miwili, na katika ile misingi majina kumi na mawili ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana-Kondoo. Nami sikuona hekalu ndani yake, kwa maana Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo, ndio hekalu lake. Na mji ule hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni Mwana-Kondoo.
SHANGILIO Yn. 14:23
Aleluya, aleluya,
Yesu alisema: Mtu akinipenda, atalishika neno langu;
Na Bana yangu atampenda; nasi tutakuja kwake.
Aleluya.
INJILI: Yn. 14:23-29
Yesu aliwaambia wafuasi wake: “Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka. Hayo ndiyo niliyowaambia wakati nilipokuwa nikikaa kwenu. Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia. Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo.
Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga. Mlisikia ya kwamba mimi naliwaambia, ‘Naenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba; kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi. Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini.”’
TAFAKARI
ROHO MTAKATIFU HAJI KUKOROFISHA MAFUNDISHO YA YESU: Yesu Kristo yupo karibu kurudi katika utukufu wake wa mbinguni, na hivyo anazungumzia anavyotamani mambo yawe baada ya yeye kuondoka duniani. Kwanza anamfafanua mtu anayempenda anavyoweza kujipambanua. Anasema, “Mtu atakayekuwa anampenda atakuwa analishika neno lake.”
Baada ya kumzungumzia mtu binafsi, Yesu anawazungumzia watakaomfuata katika ujumla wao. Akidokeza kwa namna fulani zawadi ijayo ya Pentekoste, Yesu anasema ili watakaomfuata wasibaki kama yatima, kwa jina lake, Baba atawapelekea Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu hatakuja kukorofisha mafundisho ya Yesu. Anayetenda kinyume na Yesu ni Shetani “mtakafujo”.
Somo la kwanza linatuonesha tayari jinsi waamini walivyokaribia kuvurugana lakini wazee kwa msaada wa Roho Mtakatifu waliweza kuliokoa Kanisa. Tatizo lilianzia kwenye kuwataka wabatizwa kutoka kwa Mataifa kufuata desturi za Kiyahudi hususan tohara. Wazee walisikia jinsi watu waliotoka Yerusalemu walivyowaendea Wakristo waliotoka kwa Mataifa na kuwasumbua kwa maneno yao, wakipotosha roho zao, ambao wao hawakuwaagiza. Kwa sababu hii wazee waliona vema kuwachagua watu na kuwapeleka kwa wale wanaosumbuliwa pamoja na akina Barnaba na Paulo. Ndipo wakawatuma Yuda na Sila, aliowaambia maneno yayo hayo kwa vinywa vyao.
Wakatoa hoja ya kutowasumbua watu kwa mafundisho ya ovyo. Walisema ilimpendeza Roho Mtakatifu na wao, wasiwatwike wabatizwa mzigo isipokuwa mambo yaliyo ya lazima tu, yaani, kujiepusha na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Wazee waliwahakikisha watu kwamba wakijizuia na mambo waliyoorodhesha katika barua, watafanya vema sana.
Somo la pili linaongelea watakavyotunukiwa watu waaminifu kwa mafundisho ya Yesu au watu watakaoshirikiana vyema na Mungu. Watajaliwa kukaribishwa katika maskani ya Mungu Baba na Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Maskani ya Mungu ni mji mtakatifu, mji wenye utukufu wa Mungu, na mwangaza ulio kama kito chenye thamani nyingi kama kito cha yaspi, safi kama bilauri; mji wenye ukuta mkubwa, mrefu, na milango kumi na miwili iliyoandikwa majina ya kabila kumi na mbili za Waisraeli, mji usio na hekalu ndani yake, kwa vile Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo, ndio hekalu lake; mji usiohitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa vile utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni Mwana-Kondoo.
Kwa hali hii, tusikubali kupokeleshwa Roho Mtakatifu aliye hasimu wa Yesu Kristo na mafundisho yake. Kumbe, tukae tukijua kitu chochote, mathalani, kinachofundisha habari za laana, mizimu, miti ya ukoo na kukataa sakramenti ya Kanisa na mamlaka yake hakitoki kwa Roho Mtakatifu na mwalimu wake si Roho Mtakatifu. Tukikimbie kitu kama hicho kwa spidi kali kabisa.
SALA: Ee Mungu Mwenyezi, tunakuomba tushirikiane vyema na Roho Mtakatifu ili tusiyaache mafundisho sahihi ya Kanisa letu. Usituache tudanganywe na chochote kinachojidai ni Roho Mtakafitu. Amina.