Mei 21,2022; Jumamosi: Juma la 5 la Pasaka

Nyeupe
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Mdo. 16:1-10
Siku zile, Paulo alifika Derbe na Listra na hapo palikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke Myahudi aliyeamini; lakini babaye alikuwa Myunani. Mtu huyo alishuhudiwa vyema na ndugu waliokaa Listra na Ikonio. Paulo akamtaka huyo afuatane naye, akamtwaa akamtairi kwa ajili ya Wayahudi waliokuwako pande zile; kwa maana wote walijua ya kuwa babaye ni Myunani. Basi walipokuwa wakipita kati ya miji ile wakawapa zile amri zilizoamriwa na mitume na wazee walioko Yerusalemu, ili wazishike. Makanisa yakatiwa nguvu katika ile imani, hesabu yao ikaongezeka kila siku. Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia. Walipofika kukabili Misia, wakajaribu kwenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa, wakapita Misia wakatelemka Troa. Paulo akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, “Vuka, uje Makedonia utusaidie.” Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri Habari Njema.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 100:1-3, 5

 1. Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote
  Mtumikieni Bwana kwa furaha.
  Njoni mbele zake kwa kuimba;
  (K) Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote.
 2. Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
  Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
  Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. (K)
 3. Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;
  Rehema zake ni za milele;
  Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (K)

INJILI: Yn. 15:18-21

Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia. Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu. Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka.”

TAFAKARI
ULIMWENGU UMENICHUKIA, UTAWACHUKIA: Kristo anawatahadharisha kwa kuwaambia wakiwa kweli wafuasi wake, ulimwengu utawachukia. Ikiwa yeye aliukabili ulimwengu uliomchukia, inawapasa wafuasi wake pia wamuige. Kanisa la kwanza linaendelea kustawi kwa matendo ya mitume wakiongozwa na Roho wa Mungu. Mitume wanafurahia kwa muda faraja ya kukubalika na malimwengu. Lakini haitakuwa muda mrefu kabla ulimwengu haujawachukia. Mitume ni mashahidi wa ufufuo wa Kristo, unaopingana na kila namna ya kumgandamiza mwanadamu kimwili na kiroho. Hivyo si ajabu mitume kukutana na pingamizi katika utume wao.
Nasi leo tutambue kwamba tumetumwa kama wafuasi kuuangazia na kuuelekeza ulimwengu kumkubali Mungu. Lazima tusimame katika kweli na haki, hata ikibidi kubaki peke yetu. Karne ya ilisifika sana kwa matukio ya utesi wa Kanisa. Karne ya XXI katika nchi zingine Kanisa linaendelea kutetea haki na kweli kwenye mifumo gandamizi.

SALA :Ee Mungu, ulijalie Kanisa lako kutotafuta sifa tu, bali kutafuta haki na kweli.