Mei 20,2022; Ijumaa: Juma la 5 la Pasaka

Mt. Bernadini wa Siena, Padre
Nyeupe
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Mdo. 15: 22-31
Siku zile, baada ya mtaguso wa Yerusalemu, ikawapendeza mitume na wazee na kanisa lote kuwachagua watu miongoni mwao na kuwapeleka Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba; nao ni hawa, Yuda aliyeitwa Barnaba, na Sila, waliokuwa watu wakuu katika ndugu. Wakaandika hivi na kupeleka kwa mikono yao, mitume na ndugu wazee, kwa ndugu zetu walioko Antiokia na Shamu na Kilikia, walio wa mataifa; Salamu. Kwa kuwa tumesikia ya kwamba watu waliotoka kwetu wamewasumbua kwa maneno yao, wakipotosha roho zenu, ambao sisi hatukuwaagiza; sisi tumeona vema, hali tumepatana kwa moyo mmoja, kuwachagua watu na kuwapeleka kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo, watu waliohatarisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Basi tumewatuma Yuda na Sila, watakaowaambia wenyewe maneno yayo hayo kwa vinywa vyao. Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima, yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. Wasalamu. Hata hao wakiisha kupewa ruhusa wakatelemkia Antiokia; na baada ya kuwakusanyia jamii yote wakawapa ile barua. Nao walipokwisha kuisoma, wakafurahi kwa ajili ya faraja ile.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 57:7-11

 1. Ee Mungu, moyo wangu u thabiti,
  Moyo wangu u thabiti.
  Nitaimba, nitaimba zaburi,
  Amka, utukufu wangu.
  Amka, kinanda na kinubi,
  Nitaamka alfajiri.
  (K) Ee Bwana, nitakushukuru kati ya watu.
 2. Ee Bwana, nitakushukuru kati ya watu,
  Nitakuimbia zaburi kati ya mataifa.
  Maana fadhili zako ni kubwa hata mbinguni,
  Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu,
  Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako. (K)

INJILI: Yn. 15:12-17
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu. Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni. Haya nawaamuru ninyi, mpate kupendana.”

TAFAKARI
NI MIMI NILIYEWACHAGUA NINYI: Kristo anawahimiza mitume wake kupendana, na kutoa mfano wa kifo chake mwenyewe kama ishara kuu ya upendo. Kwa kuwa wameyajua yaliyo moyoni mwake, Kristo anawaita marafiki na sio watumishi. Anasisitiza kwamba sio mitume waliomchagua, lakini ni Yesu mwenyewe aliyewaita kwanza, ili wazae matunda ya kudumu. Baada ya mtaguso wa Yerusalemu, mitume wanawachagua wawili kati yao ili kwenda na waraka wa kuwaunganisha waumini wa Antiokia. Wanaonyesha umoja na upendo mkubwa kati yao, hasa wanaposuluhisha migogoro kati yao. Walitambua kwamba walichaguliwa ili wamshuhudie Kristo kama mitume wake, na kwa hivyo walizingatia sana amri ya upendo.
Waumini wote wanawiwa kuzingatia amri kuu ya Kristo, na kuitumia kama msingi wa kusuluhisha matatizo yote yanayowakuta. Mungu atujalie kujua kwamba wote tumechaguliwa naye, ili tumshuhudie kwa upendo.

SALA:Ee Kristo, utujalie kutambua kwamba wewe ndiwe uliyetuita kwanza, ili tuwe mashahidi wa upendo wako.