Mei 18,2022; Jumatano: Juma la 5 la Pasaka

Mt. Yohane I, Baba Mt. Na Shahidi
Nyeupe
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Mdo. 15:1-6
Siku zile, walishuka watu waliotoka Uyahudi wakawafundisha wale ndugu ya kwamba, “Msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka.” Basi baada ya Paulo na Barnaba kushindana na watu hawa na kuhojiana nao sana, ndugu wakaamuru kwamba Paulo na Barnaba na wengine miongoni mwao wapande kwenda Yerusalemu kwa mitume na wazee kwa habari ya swali hilo. Basi, wakisafirishwa na kanisa, wakapita kati ya nchi ya Foinike na Samaria, wakitangaza habari za kuongoka kwao mataifa; wakawafurahisha ndugu sana. Walipofika Yerusalemu wakakaribishwa na kanisa na mitume na wazee, nao wakawaeleza mambo yote Mungu aliyoyafanya pamoja nao. Lakini baadhi ya madhehebu ya Mafarisayo walioamini wakasimama wakisema, “Ni lazima kuwatahiri na kuwaagiza kuishika torati ya Musa. Mitume na wazee wakakusanyika wapate kulifikiri neno hilo.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 122:1-5

 1. Nalifurahi waliponiambia
  Na twende nyumbani kwa Bwana.
  Miguu yetu imesimama
  Ndani ya malango yako, ee Yerusalemu.
  K: Nalifurahi waliponiambia,
  Na twende nyumbani kwa Bwana.
 2. Ee Yerusalemu uliyejengwa
  Kama mji ule ulioshikamana,
  Huko ndiko walikopanda kabila,
  Kabila za Bwana. (K)
 3. Ushuhuda kwa Israeli,
  Walishukuru jina la Bwana.
  Maana huko viliwekwa viti vya hukumu,
  Viti vya enzi vya mbari ya Daudi. (K)

INJILI: Yn. 15:1-8
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa. Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia. Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea. Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.”

TAFAKARI
KRISTO MZABIBU WA KWELI : Kristo anajifananisha na mzabibu ambapo Mungu Baba ndiye mkulima na mitume wake ni matawi. Bila kuhudumiwa na mkulima, mzabibu haubaki imara. Nayo matawi hunyauka na kutenganishwa na mzabibu. Yote yanategemea juhudi na msaada wa mkulima, na tawi halistawi wala kuzaa likiwa lenyewe. Kwa mfano huu Kristo anawafundisha mitume wake kubaki daima wakiwa wameunganika naye, sawa na vile alivyounganika na Baba. Somo la kwanza linasimulia matatizo wanayokumbana nayo waumini wa Kanisa la mwanzo. Inawalazimu kuamua kufuata tamaduni zao, ama kufuata mafundisho ya Kristo, ya kuwa na taifa na familia moja ya Mungu. Wanachagua kuambatana na Kristo. Imani yetu inakabiliwa na namna nyingi za mabadiliko katika ulimwengu wetu. Inatulazimu kubaki imara kwa msaada ya Mungu, na kumruhusu Mungu kupunguza na kukata yote yanayotuzuia kuzaa matunda mema na kwa wengi.

SALA: Ee Mungu, tujalie kubaki daima kwako uliye mzabubi wa kweli.