Mei 17,2022; Jumanne: Juma la 5 la Pasaka

Nyeupe
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Mdo.14:19-28
Wayahudi walifika toka Antiokia na Ikonio, wakawashawishi makutano hata wakampiga kwa mawe Paulo, wakamburuta nje ya mji, wakidhani ya kuwa amekwisha kufa. Lakini wanafunzi walipokuwa wakimzunguka pande zote, akasimama, akaingia ndani ya mji; na siku ya pili yake akatoka, akaenda zake pamoja na Barnaba mpaka Derbe. Hata walipokwisha kuhubiri Injili katika mji ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra na Ikonio na Antiokia, wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi. Na walipokwisha kuwachagulia wazee katika kila kanisa, na kuomba pamoja na kufunga, wakawaweka katika mikono ya Bwana waliyemwamini. Wakapita kati ya Pisidia wakaingia Pamfilia. Na baada ya kuhubiri lile neno katika Perge wakatelemka mpaka Atalia. Na kutoka huko wakaabiri kwenda Antiokia. Huko ndiko walipoombewa neema ya Mungu kwa ile kazi waliyokwisha kuitimiza. Hata walipofika wakalikutanisha kanisa, wakawaeleza mambo yote aliyoyafanya Mungu pamoja nao, na ya kwamba amewafungulia mataifa mlango wa imani. Wakaketi huko wakati usiokuwa mchache, pamoja na wanafunzi.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 145:10-13, 21

 1. Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru,
  Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
  Wataunena utukufu wa ufalme wako,
  Na kuuhadithia uweza wako,
  Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu,
  Na utukufu wa fahari ya ufalme wake.

K: Watawajulisha watu matendo yake makuu,
Na utukufu wa fahari wa zamani zote.

 1. Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
  Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote. (K)
 2. Kinywa change kitazinena sifa za Bwana;
  Wote wenye mwili na walihimidi jina lake takatifu
  milele na milele. (K)

INJILI: Yn. 14:27-31
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga. Mlisikia ya kwamba mimi naliwaambia, ‘Naenda zangu, tena naja kwenu.’ Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba; kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi. Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini. Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu. Lakini ulimwengu ujue ya kuwa nampenda Baba; na kama vile Baba alivyoniamuru; ndivyo nifanyavyo. Ondokeni, twendeni zetu.”

TAFAKARI
AMANI. MSIFADHAIKE MIOYONI MWENU: Katika huzuni ya kuagana naye, Yesu anatambua mashaka waliyonayo wanafunzi wake. Anawapa zawadi ya amani, ambayo ulimwengu haungeweza kuwapa, na kuwafariji. Faraja na amani anayotoa Yesu inaleta utulivu wa kipekee ndani ya moyo unaofadhaika. Amani hii inatokana na uhakika wa msamaha kamili na kujua kwamba tumeunganishwa na Mungu, na hakuna lolote linaloweza kuiondoa. Mtume Paulo anashambuliwa kwa mawe na makundi ya kiyahudi karibu kuzirai. Lakini anapoamka, yeye, Barnaba na Mitume wengine hawakusita kuendelea na uinjilishaji. Walifarijika kujua kwamba Mungu alikuwa pamoja nao.
Tufuate mfano wa Mtakatifu Maximilian Kolbe, aliye mfano wa mtu aliyejaliwa amani ya moyoni inayoshinda vyote. Alibaki mtulivu hata kama alipata mateso makali na kuzungukwa na mauaji na ukatili mkubwa kwenye kambi ya mauaji ya halaiki, mjini Auschwitz. Ndio zawadi ya Kristo kwetu. ‘Amani nawaachieni. Msifadhaike mioyoni mwenu.’

SALA: Ee Mfalme wa Amani, uijalie utulivu mioyo wa watu wanaofadhaika.