Mei 14,2022;Jumamosi: Juma la 4 la Pasaka

Mt. Mathia Mtume
Sikukuu
Nyekundu
Zaburi: Tazama sala ya siku
SOMO 1: Mdo. 1:15-17, 20-26

Siku zile Petro alisimama kati ya ndugu zake (jumla ya majina ilipata mia na ishirini), akasema, “Ndugu, ilipasa andiko litimizwe, alilolinena Roho Mtakatifu zamani kwa kinywa cha Daudi, katika habari za Yuda aliyewaongoza wao waliomkamata Yesu, kwa sababu alikuwa amehesabiwa pamoja na sisi, akapata sehemu ya huduma hii. Kwa maana imeandikwa katika chuo cha Zaburi, ‘Kikao chake na kiwe ukiwa, Wala asiwepo mtu mwenye kukaa humo; tena usimamizi wake autwae mwingine.’”

Basi katika watu waliofuatana nasi wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiingia na kutoka kwetu, kuanza tangu ubatizo wa Yohane, hata siku ile alipochukuliwa kwetu kwenda juu, inapasa mmoja wao awe shahidi wa kufufuka kwake pamoja nasi. Wakaweka wawili, Yusufu, aitwaye Barsaba, aliyekuwa na jina la pili Yusto, na Mathiya. Kisha wakaomba, wakasema, “Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, tuonyeshe ni nani uliyemchagua katika hawa wawili, ashike mahali katika huduma hii na utume huu, alioukosa Yuda, aende zake mahali pake mwenyewe.” Wakawapigia kura; kura ikamwangukia Mathiya; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 113:1-8

 1. Aleluya.
  Enyi watumishi wa Bwana, sifuni,
  Lisifuni jina la Bwana.
  Jina la Bwana lihimidiwe
  Tangu leo na hata milele

(K) Amketishe pamoja na wakuu,
pamoja na wakuu wa watu wake.

 1. Toka maawio ya jua hata machweo yake
  Jina la Bwana husifiwa.
  Bwana ni mkuu juu ya mataifa yote,
  Na utukufu wake ni juu ya mbingu. (K)
 2. Ni nani aliye mfano wa Bwana,
  Mungu wetu aketiye juu;
  Anyenyekeaye kutazama

INJILI: Yn. 15:9-17

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu. Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe.
Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu. Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni. Haya nawaamuru ninyi mpate kupendana.”

TAFAKARI
TUWE MASHAHIDI WA KRISTO: Mtume Matia alitangulia utume wake kwa kushiriki utume wa Yesu Kristo, kama mfuasi tangu ubatizo wa Yesu mtoni Yordani hadi kupaa kwake. Akachaguliwa kuchukua nafasi ya Yuda Iskariote kati ya Mitume. Mitume walisali na kuomba msaada wa Mungu kujua ni nani watakayemchagua. Mtume Matia alijaliwa kuwa shahidi wake Kristo na kutangaza ufufuko wake. Yesu Kristo anawaasa mitume kudumu katika pendo lake na kushika amri zake. Kiini cha mafundisho mengi ya Kristo yalikuwa ni upendo kwa Mungu na kwa jirani. Alitoa mfano mwema wa upendo uliopo katika Utatu Mtakatifu.
Tufuate mafundisho ya Kristo, aliyewaasa mitume kuishi kwa upendo kati yao, ili watambulike kuwa mitume wake. Ushuhuda wa Kristo mfufuka na upendo kwa Mungu na jirani ni vigezo muhimu kwa kila mfuasi wa Kristo.

SALA: Ee Yesu, utujalie kuwa mitume wako, kwa kushuhudia imani kwa Mungu mmoja na upendo kwa Mungu na jirani.