Mei 13,2022; Ijumaa: Juma la 4 la Pasaka.

Our Lady of Fatima
Nyeupe
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Mdo. 13:26-33
Paulo alisimama akawapungia mkono, akasema: ndugu zangu, wana wa ukoo wa Ibrahimu, na hao miongoni mwenu wanaomcha Mungu, kwetu sisi neno la wokovu huu limepelekwa. Kwa maana wakaao Yerusalemu, na wakuu wao, kwa kuwa hawakumjua yeye, wala maneno ya manabii yanayosomwa kila sabato, wameyatimiza kwa kumhukumu. Na ijapokuwa hawakuona sababu ya kumfisha wakamwomba Pilato auawe. Hata alipokwisha kumaliza yote aliyoandikiwa, wakamtelemsha katika ule mti, wakamweka kaburini. Lakini Mungu akamfufua katika wafu; akaonekana siku nyingi na wale waliopanda naye kutoka Galilaya hata Yerusalemu, ambao sasa ndio walio mashahidi wake mbele ya watu. Na sisi tunawahubiri habari njema ya ahadi ile waliyopewa mababa, ya kwamba Mungu amewatimizia watoto wetu ahadi hiyo, kwa kumfufua Yesu kama ilivyoandikwa katika zaburi ya pili, Wewe ndiwe Mwanangu, mimi leo nimekuzaa.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 2:6-11

 1. Nami nimemweka mfalme wangu
  Juu ya Sayuni, mlima wangu mtakatifu
  Nitaihubiri amri; Bwana aliniambia
  Ndiwe mwanangu, mimi leo nimekuzaa.
  K: Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa.
 2. Uniombe, name nitakupa mataifa kuwa urithi wako,
  Na miisho ya dunia kuwa milki yako.
  Utawaponda kwa fimbo ya chuma,
  Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi. (K)
 3. Na sasa, enyi wafalme, fanyeni akili,
  Enyi waamuzi wa dunia, mwadibiwe.
  Mtumikieni Bwana kwa kicho,
  Shangilieni kwa kutetemeka. (K)

INJILI: Yn. 14:1-6
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia, maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi muwepo. Nami niendako mwaijua njia.” Tomaso akamwambia, “Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia?” “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.”

TAFAKARI
YESU KRISTO NI HABARI NJEMA : Mtume Paulo alisisitiza kuwa Kristo ni Habari Njema ya utimilifu wa ahadi ya Israeli, ambaye ujio wake ulishuhudiwa na wanaomcha Mungu. Kwamba japo alikufa kwa hila ya wasioyajua maandiko, Mungu alimfufua kutoka kwa wafu na akawafanya mitume kuwa mashahidi wake. Kristo anawasihi mitume wake wasifadhaishwe na kuondoka kwake, bali wamwamini, maana, ‘nyumbani kwa Baba kuna makao mengi’, anakwenda kuwaandalia makao. Anawaaga na kuwafariji. Watamfuata kwa maana wanamjua Yeye aliye njia, ukweli na uzima. Kristo ni Habari Njema, kama utimilifu wa ahadi ya Mkombozi ya uzao wa Ibrahimu.
Hii ni Habari Njema kwa ulimwengu wa sasa unaohitaji ukombozi wake, na ni Habari Njema kwa ufalme ujao, anapokwenda kuwaandalia wamwaminio makao. Kwa kutenda kama alivyotenda tutafika aliko Mkombozi wetu.

SALA: Ee Mungu, ulitimiza ahadi yako kwa ujio wa Kristo. Utujalie kumfuata ili kuyafikia makao anayotuandalia.