Mei 12,2022; Alhamisi: Juma la 4 la Pasaka

Wat. Nerei na Akilei, Mashahidi/ mt. Pankrasi, Shahidi
Nyeupe
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Mdo. 13: 13-25
Paulo na wenziwe wakang’oa nanga wakasafiri kutoka Pafo, wakafika Perge katika Pamfilia. Yohane akawaacha akarejea Yerusalemu. Lakini wao wakatoka Perge, wakapita kati ya nchi, wakafika Antiokia, mji wa Pisidia, wakaingia katika sinagogi siku ya sabato, wakaketi. Kisha, baada ya kusomwa torati na chuo cha manabii, wakuu wa sinagogi wakatuma mtu kwao, na kuwaambia, “Ndugu, kama mkiwa na neno la kuwafaa watu hawa lisemeni.” Paulo akasimama, akawapungia mkono, akasema, “Enyi waume wa Israeli, nanyi mnaomcha mungu, sikilizeni. Mungu wa watu hawa Israeli aliwachagua baba zetu, akawatukuza watu hao, walipokuwa wakikaa kama wageni katika nchi ya Misri, na kwa mkono ulioinuliwa akawatoa, akawaongoza. Na kwa muda wa miaka kama arobaini akawavumilia katika jangwa.
Na alipokwisha kuwaharibu mataifa saba katika nchi ya Kanaani akawapa nchi yao iwe urithi kwa muda wa miaka kama mia nne na hamsini; baada ya hayo akawapa waamuzi hata zamani za nabii Samweli. Hatimaye wakaomba kupewa mfalme; Mungu akawapa Sauli mwana wa Kishi, mtu wa kabila ya Benyamini, kwa muda wa miaka arobaini. Na alipokwisha kumwondoa huyo, akamwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, ‘Nimemwona Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu yote.’ Katika uzao wake mtu huyo Mungu amewaletea Israeli Mwokozi, yaani, Yesu, kama alivyoahidi; Yohane alipokuwa amekwisha kuwahubiri watu wote wa Israeli habari za ubatizo wa toba, kabla ya kuja kwake. Naye Yohane alipokuwa akimaliza mwendo wake alinena, ‘Mwanidhani mimi kuwa nani? Mimi siye. Lakini, angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye mimi sistahili kumlegezea viatu vya miguu yake.”’

Wimbo Wa Katikati: Zab. 89:1-2, 20-21, 26-27

 1. Kwa kinywa change
  Nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.
  Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele;
  Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako.
  K “Fadhili zako, ee Bwana, nitaziimba milele.”
 2. Nimemwona Daudi, mtumishi wangu,
  Nimempaka mafuta yangu matakatifu.
  Ambaye mkono wangu utakuwa thabiti kwake,
  Na mkono wangu utamtia nguvu. (K)
 3. Yeye ataniita, Wewe baba yangu,
  Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.
  Nami nitamjalia kuwa mzaliwa wangu wa kwanza,
  Kuwa juu sana kuliko wafalme wa dunia. (K)

INJILI: Yn. 13:16-20
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Amin, amin, nawaambia ninyi, Mtumwa si mkuu kuliko bwana wake; wala mtume si mkuu kuliko yeye aliyempeleka. Mkiyajua hayo, heri ninyi mkiyatenda. Sisemi habari za ninyi nyote; nawajua wale niliowachagua; lakini andiko lipate kutimizwa, aliyekula chakula changu ameniinulia kisigino chake. Tangu sasa nawaambia kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini ya kuwa mimi ndiye. Amin, amin, nawaambieni, Yeye ampokeaye mtu ye yote nimpelekaye, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi ampokea yeye aliyenipeleka.

TAFAKARI
KUMFUASA KRISTO KATIKA UTII: Mtume Paulo anafafanua kwamba Yesu Kristo ndiye Mkombozi aliyeahidiwa na kutabiriwa ujio wake tangu enzi za Israeli. Anafundisha ndani ya sinagogi, na kuwaasa kumwamini Kristo. Kristo katika injili anajishusha na kumtukuza Mungu aliyemtuma. Anawaalika mitume kumfuata. Kuwa mfuasi wa Kristo ni kuwa mtendaji wa injili, na kumuiga katika utii na unyenyekevu wake. Wanaompokea mtume wanampokea Yesu Kristo mwenyewe. Aidha, Kristo anawatambua wasiomwamini na wasaliti wake, ambao watashirikiana na watesi wake kumwangamiza. Kwa mapendo makubwa anawaruhusu kutumia uhuru wao kubadilika wakipenda na kumfuata.
Sawa na mitume, watumishi wa Kristo wanafundisha ukombozi katika Kristo. Kila mmoja anaalikwa kumfuasa Mkombozi kwa kuifuata njia anayoelekeza, njia inayolazimu utii wa Neno la Mungu na unyenyekevu. Wasiomwamini wanashauriwa kuongoka na kujiunga na kundi la wanaomwamini.

SALA: Ee Mkombozi wetu uliye utimilifu wa ahadi za Mungu kwa taifa la Israeli, utujalie kukutambua, kukutii na kukufuata.