Mei 11,2022; Jumatano1; Juma la 4 la Pasaka

Nyeupe
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Mdo. 12:24, 13:5
Siku zile, neno la Bwana likazidi na kuenea. Na Barnaba na Sauli, walipokwisha kutimiza huduma yao, wakarejea kutoka Yerusalemu, wakamchukua pamoja nao Yohane aitwaye Marko. Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, “Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia.” Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao. Basi watu hao, wakiisha kupelekwa na Roho Mtakatifu wakatelemkia Seleukia, na kutoka huko wakasafiri baharini hata Kipro. Na walipokuwa katika Salami wakalihubiri neno la Mungu katika masinagogi ya Mayahudi.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 67:1-2, 4, 5, 7

 1. Mungu na atufadhili na kutubariki,
  Na kutuangazia uso wake.
  Njia yake ijulike duniani,
  Wokovu wake katikati ya mataifa yote.
  K: Watu na wakushukuru, Ee Mungu,
  Watu wote na wakushukuru.
 2. Mataifa na washangilie,
  Naam, waimbe kwa furaha,
  Maana kwa haki utawahukumu watu,
  Na kuwaongoza mataifa walioko duniani. (K)
 3. Watu na wakushukuru, Ee Mungu,
  Watu wote na wakushukuru.
  Mungu atatubariki sisi;
  Miisho yote ya dunia itamcha Yeye. (K)

INJILI: Yn. 12:44-50
Siku ile Yesu alipaza sauti, “Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi bali yeye aliyenipeleka. Naye anitazamaye mimi amtazama yeye aliyenipeleka. Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani. Na mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, ila niuokoe ulimwengu. Yeye anikataaye mimi, asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumuye; neno hilo nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho. Kwa sababu mimi sikunena kwa nafsi yangu tu; bali Baba aliyenipeleka, yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema. Nami najua ya kuwa agizo lake ni uzima wa milele; basi hayo ninenayo mimi, kama Baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo.”

TAFAKARI
KUMJUA KRISTO NI KUMJUA MUNGU: Kristo anatufundisha kwamba amtazamaye yeye na kumwamini anamtazama na kumwamini Yeye aliyempeleka, kwani alitumwa na Mungu ili awe nuru ya ulimwengu. Tunamfahamu Mungu vema zaidi kupitia kwa mwanawe. Yesu Kristo ni Neno la Mungu aliyetwaa mwili na kukaa kwetu. Kila alichofundisha na kukitenda alitimiza mapenzi ya Baba aliyemtuma, na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Ni kwa nguvu hiyo hiyo ambayo mitume wanaeneza Habari Njema. Wanapita sehemu nyingi wakieneza Neno la Mungu na kuwafundisha watu kumjua Mungu kwa ajili ya wokovu wa roho zao. Kristo hamhukumu yeyote kwa kutomwamini, ila neno analolisema linamhukumu kwani anatenda anachoagizwa na Baba.
Kwa kumsikia na kumtii Kristo aliyekufa na kufufuka kwa mapenzi ya Baba ili auokoe ulimwengu, tunamfahamu Mungu anayemwalika mwanadamu katika ufalme wake.

SALA: Ee Yesu Kristo, utujalie kuyaishi mafundisho yako, ili tuweze kumjua Mungu Baba, ili mwishowe tuufikie ufalme wako.