Mei 8,2022; Jumapili: Juma la 4 la Pasaka

SOMO 1: Mdo. 13:14, 43-52
Paulo na Barnaba walitoka Perge, wakapita kati ya nchi, wakafika Antiokia, mji wa Pisidia, wakaingia katika sinagogi siku ya sabato, wakaketi. Sinagogi lilipofumukana, Wayahudi na waongofu watauwa wengi wakashikamana na Paulo na Barnaba; ambao, wakisema nao, wakawatia moyo kudumu katika neema ya Mungu. Hata sabato ya pili, watu wengi, karibu mji wote, wakakusanyika walisikie neno la Mungu. Bali Wayahudi walipowaona makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana. Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, “Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa. Kwa sababu ndivyo tulivyoamriwa na Bwana, ‘Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa, Upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia.’” Mataifa waliposikia hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini. Neno la Bwana likaenea katika nchi ile yote. Lakini Wayahudi wakawafitinisha wanawake watauwa wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao. Nao wakawakung’utia mavumbi ya miguu yao, wakaenda Ikonio. Na wanafunzi walijaa furaha na Roho Mtakatifu.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 100:1-3, 5

 1. Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote;
  Mtumikieni Bwana kwa furaha;
  Njoni mbele zake kwa kuimba.

K: Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.

 1. Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
  Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
  Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. (K)
 2. Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;
  Rehema zake ni za milele;
  Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (K)

SOMO 2: Ufu. 7:9, 14b-17
Wakati ule, mimi, Yohane, niliona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-Kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao. Mmoja wa wale wazee akiniambia, “Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo. Kwa hiyo wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu, nao wanamtumikia mchana na usiku katika hekalu lake, na yeye aketiye katika kiti cha enzi atatanda hema yake juu yao. Hawataona njaa tena, wala hawataona kiu tena, wala jua halitawapiga, wala hali iliyo yote. Kwa maana huyo Mwana-Kondoo, aliye katikati ya kiti cha enzi, atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na Mungu atayafuta machozi yote katika macho yao.”

SHANGILIO Yn. 10:14

Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi mchungaji mwema;
Nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi.
Aleluya.

INJILI: Yn. 10:27-30
Yesu alisema; “Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu. Mimi na Baba tu umoja.”

TAFAKARI
MUNGU ANATAKA WATU WOTE WA ULIMWENGU TUFIKIWE: Masomo tuliyosomewa yanatuambia jambo hili. Mpango wa Mungu wa kutukomboa wanadamu ni mpana. Ni mpango uliokusudiwa kuwafikia hata wanaoukataa. Injili inasema, watu wakishaupokea mpango huo wanapewa uzima wa milele na kuhakikishiwa ulinzi wasipotee. Yesu anasema yeye hupaswa kuwajibika kwa watu hao ili wasipokonywe mkononi mwake. Kwa kweli wako mkononi mwa Mungu Baba kwa vile Mungu Baba na yeye ni wamoja. Maneno haya ni ya faraja kubwa kwa mfuasi wa Yesu anayejitambua.
Hata hivyo, maelezo haya ya Injili yanaelekea kueleweka kana kwamba wanaokuwa Wakristo hawawezi kuingia jehanamu. Si sawa kuelewa hivyo kwa maana ijapokuwa ni kweli hakuna anayeweza kuwapokonya watu hao kutoka mikononi mwa Mungu, wanadamu kwa akili na utashi wao huweza kuamua kujidondosha kutoka mikononi mwa Yesu. Aidha kwa kumsikiliza Shetani humwasi Yesu na kumsaliti. Humkataa. Hapo ndipo huziweka roho zao rehani. Ndipo hao wataajibika kwa kujipoteza wenyewe. Lakini basi, kwa ujumla, wenye kujituliza na kujidumisha mikononi mwa Mungu hukaa salama salimini.
Somo la kwanza linasimulia mkasa wa Wayahudi kuikataa Injili. Mwandishi wa kitabu cha Matendo ya Mitume anasimulia mambo yalivyokuwa. Anasema Wayahudi walipowaona makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana. Ndipo Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa na kuwasikitikia wakisema, “Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwao kwanza; kwa kuwa wanalisukumia mbali, na kujiona nafsi zao kuwa hawastahili uzima wa milele basi wanawageukia watu wa Mataifa.” Mkasa huu ulisikitisha lakini ndio unadhihirisha pia kwamba Mungu anataka, kwa heri au kwa shida, watu wote wafikiwe na kutangaziwa Habari Njema ya furaha.
Somo la pili linatupa picha ya mambo yatakavyoishia huko mwishoni mwa historia. Linasema mradi utafanikiwa. Watu watapatikana na kufanya mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu atakayeweza kuuhesabu. Watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, watasimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-Kondoo, wakiwa wamevikwa mavazi meupe na kushika matawi ya mitende mikononi mwao. Mungu atawatandia hema yake juu yao nao hawataona njaa tena, wala hawataona kiu tena, wala jua halitawapiga, wala hari iliyo yote. Somo linasema mambo yatakuwa hivyo kwa sababu Yesu, ndiye Mwana-Kondoo, aliye katikati ya kiti cha enzi, atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na Mungu atayafuta machozi yote katika macho yao. Hata hapo mradi wa watu wote kutakiwa kufika na kukaa na Mungu utakuwa umefanikiwa. Hata hivyo wale waliikataa Injili kama hawatakuwa wamejirudi watakuwa wamelipata walilolitafuta maana mwana kulitafuta mwana kulipata. Watakuwa wamejidondosha wenyewe kutoka mikononi mwa Kristo na kujipeleka wenyewe kwenye moto wa milele alioandaliwa Shetani na watu wanaomshabikia kama wao. Jambo hili la mwisho hatutaki litukute. Mungu tusaidie.

SALA: Ee Mungu mwenyezi mpango wako wa kutufikia watu wote tunauelewa pole pole. Tunakuomba utakapoukamilisha kabisa mbinguni, sisi nasi tuwemo kati ya uliowakusanya kwa uzima wa milele. Amina.