Mei 7, 2022; Jumamosi: Juma la 3 la Pasaka.

Nyeupe
Zaburi: Juma 3
SOMO I: Mdo. 9:31-42
Kanisa lilipata raha katika Uyahudi wote na Galilaya na Samaria, likajengwa, likiendelea na kuongezeka katika kicho cha Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu. Hata Petro alipokuwa akizunguka-zunguka pande zote akawatelemkia na watakatifu waliokaa Lida. Akamwona mtu mmoja huko, jina lake Ainea, mtu huyo amelala kitandani miaka minane; maana alikuwa amepooza. Petro akamwambia, “Ainea, Yesu Kristo akuponya; ondoka, ujitandikie.” Mara akaondoka. Na watu waliokaa Lida na Sharani wakamwona, wakamgeukia Bwana. Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa. Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani. Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, “Usikawie kuja kwetu.” Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu nae, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao. Petro akawatoa nje wote, akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, “Tabitha, ondoka.”
Naye akafumbua macho yake na alipomwona Petro akajiinua, akaketi. Akampa mkono, akamwinua, hata akiisha kuwaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele yao, hali yu hai. Ikajulikana katika mji mzima wa Yafa; watu wengi wakamwamini Bwana.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 116:12-17

 1. Nimrudishie Bwana nini
  Kwa ukarimu wake wote alionitendea?
  Nitakipokea kikombe cha wokovu;
  Na kulitangaza jina la Bwana.
  K: Nimrudishie Bwana nini
  kwa ukarimu wake wote alionitendea?
 2. Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
  Naam, mbele ya watu wake wote.
  Ina thamani machoni pa Bwana
  Mauti ya wacha Mungu wake. (K)
 3. Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako,
  Mtumishi wako, mwana na mjakazi wako,
  Umenifungua vifungo vyoangu.
  Nitakutolea dhabihu ya kushukuru;
  Na kulitangaza jina la Bwana. (K)

INJILI: Yn. 6:60-69

Siku ile, watu wengi miongoni mwa wanafunzi wake waliposikia maneno ya Yesu juu ya mkate wa uzima, walisema: “Neno hili ni gumu, ni nani awezaye kulisikia?” Naye Yesu akafahamu nafsini mwake ya kuwa wanafunzi wake wanalinung’unikia neno hilo, akawaambia, “Je! neno hili linawakwaza? Itakuwaje basi, mmwonapo Mwana wa Adamu akipaa huko alikokuwako kwanza? Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima. Lakini kuna wengine miongoni mwenu wasioamini.” Kwa maana Yesu alijua tangu mwanzo ni nani wasioamini, naye ni nani atakayemsaliti. Akasema, “Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.” Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, “Je! ninyi nanyi mwataka kuondoka?” Basi Simoni Petro akamjibu, “Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.”

TAFAKARI
FARAJA YA MUNGU KWA KANISA LAKE: Sawa na Kristo Mwenyewe, Kanisa limepitia nyakati za faraja na nyakati za karaha. Mafundisho ya Yesu kama mkate wa uzima yanawarudisha wengine nyuma, ila walioamini wanajaliwa nguvu za pekee. Maana, “hakuna awezaye kuja kwake isipokuwa amejaliwa na Baba.” Somo la kwanza linasimulia mojawapo ya vipindi ambapo Kanisa lilistawi na kuimarika ndani ya tawala za Galilaya na Samaria. Kadiri Kanisa lilivyokuwa, ndivyo neema za Mungu zilivyozindi kudhihirika ulimwenguni. Mtume Paulo anatembelea sehemu nyingi, ikiwemo Lida, ambapo kwa nguvu ya Mungu anamwamsha mfu.
Hadi sasa Nguvu ya Mungu inaendelea kuonekana kupitia Kanisa lake, na kwa mikono ya wale waliojaliwa na Mungu Baba. Kanisa linaendelea kuwafariji wanaohitaji faraja. Ili haya yatimie, imani kwa ‘mkate wa uzima’, Kristo Mfufuka na uweza wake kupitia huduma za Kanisa ni muhimu.

SALA: Ee Bwana, kwa huduma za Kanisa lako, uwafariji wanaokuhitaji.