Mei 5,2022; Alhamisi: Juma la 3 la Pasaka

Nyeupe
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Mdo. 8:26-40

Malaika wa Bwana alisema na Filipo, akamwambia, “Ondoka ukaende upande wa kusini hata njia ile itelemkayo kutoka Yerusalemu kwenda Gaza; nayo ni jangwa.” Naye akaondoka, akaenda; mara akamwona mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini ya Kandake malkia wa kushi, aliyewekwa juu ya hazina yake yote; naye alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu, akawa akirejea, ameketi garini mwake akisoma chuo cha nabii Isaya. Roho akamwambia Filipo, “Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo.” Basi Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, “Je! Yamekuelea haya unayosoma?” Akasema, “Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza?” Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye. Na fungu la maandiko alilokuwa akilisoma ni hili, “Aliongozwa kwenda machinjoni kama kondoo, na kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake amkataye manyoya, vivyo hivyo yeye naye hafunui kinywa chake. Katika kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa. Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa maana uzima wake umeondolewa katika nchi.” Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, “Nakuomba, nabii huyu asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu mwingine?” Filipo akafunua kinywa chake, naye, akianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari njema za Yesu. Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, “Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?” Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza. Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi. Lakini Filipo akaonekana katika Azoto, na alipokuwa akipita akahubiri Injili katika miji yote, hata akafika Kaisaria.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 66:8-9, 16-17, 20

 1. Enyi mataifa, mtukuzeni Mungu wetu,
  Itangazeni sauti ya sifa zake;
  Aliyeiweka nafsi yenu katika uhai,
  Wala hakuuacha mguu wetu usogezwe.

(K) Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote.

 1. Njoni, sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu,
  Nami nitayatangaza aliyonitendea roho yangu.
  Nalimwita kwa kinywa changu,
  Na sifa kuu zilikuwa chini ya ulinzi wangu. (K)
 2. Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu,
  Wala kuniondolea fadhili zake. (K)

INJILI: Yn. 6:44-51

TAFAKARI
Yesu aliwaambia Wayahudi: “Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho. Imeandikwa katika manabii, Na wote watakuwa wamefundishwa na Mungu. Basi kila aliyesikia na kujifunza kwa Baba huja kwangu. Si kwamba mtu amemwona Baba, ila yeye atokaye kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba. Amin, amin, nawaambia, Yeye aaminiye yuna uzima wa milele. Mimi ndimi chakula cha uzima. Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa. Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni, kwamba mtu akile wala asife. Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.”
WATAONGOKA WAKIINJILISHWA: Matendo ya Mungu kwa mwanadamu yanalenga ukombozi. Mungu anatumia mbinu nyingi kumfikia mtu na kumfikishia wokovu. Filipo anaongozwa na malaika wa Mungu na kumwelekeza kumwinjilisha towashi wa Kushi, aliyesoma maandiko pasipo kuyaelewa. Kwa ufafanuzi wa Filipo, mtu wa mataifa anaongoka na kubatizwa. Katika injili Kristo ananukuu manabii kwamba ‘wote watakuwa wamefundishwa na Mungu.’ Na kwamba ‘Yeye aaminiye ana uzima wa Milele.’ Juhudi kubwa imefanyika ili kuufikishia ulimwengu habari njema. Inawalazimu Wakristo wote waliolipokea na kuliamini, wawe nao pia wajumbe wa kulieneza Neno hilo. Wapo wengi bado ambao hawaifahamu injili kwa sababu hawajafundishwa. Kwa hivyo wanatumikia ulimwengu tu. Ni jukumu la kila mbatizwa kutumia Roho wa Mungu, kujitahidi kwa hali na mali kuwezesha uinjilishaji wa Kristo Mfufuka, ili watu wakombolewe, waamini na kustahili uzima wa milele.

SALA: Ee Mungu, utufanye vyombo vya uinjilishaji, ili maitaifa yakujue na kukupenda.