Mei 4, 2022; Jumatano: Juma la 3 la Pasaka

Nyeupe
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Mdo. 8:1-8

Siku ile kulitukia adha kuu ya kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume. Watu watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu. Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani. Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno. Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 66:1-7

  1. Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote,
    Imbeni utukufu wa jina lake,
    Tukuzeni sifa zake.
    Mwambieni Mungu, Matendo yako yatisha kama nini!

(K) Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote.

  1. Nchi yote itakusujudia na kukuimbia,
    Naam, italiimbia jina lako.
    Njoni yatazameni matendo ya Mungu;
    Hutisha kwa mambo awatendeayo wnadamu. (K)
  2. Aligeuza bahari kuwa nchi kavu;
    Katika mto walivuka kwa migoo;
    Huko ndiko tulikomfurahia.
    Atawala kwa uweza wake milele;
    Macho yake yawaangalia mataifa;
    Waasio wasijitukuze nafsi zao. (K)

INJILI: Yn. 6:35-40

Yesu aliwaambia: “Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe. Lakini naliwaambia ya kwamba mmeniona wala hamwamini. Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe. Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka. Na mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho. Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.”

TAFAKARI
YESU MKATE WA UZIMA : Injili ina maana ya Habari Njema. Kwa maneno ya injili maneno ya Yesu ni Habari Njema kweli. Wote wenye njaa, ya mwili lakini zaidi ya Neno la Mungu, anawalisha na kuwashibisha kwa chakula kinachodumu. Mwana wa Mungu na Mchungaji Mwema, anafanya mapenzi ya Baba yake, kwamba yeyote ajaye kwake asimtupe nje. Huu ndio ukuu wa neema za Mungu. Kuwajali wenye mahitaji ya kila namna, na kuwatunza wote wanaotamani kukaa karibu naye.
Hata katika changamoto za kushambuliwa na kuteswa, mitume na Kanisa la mwanzo waliendelea kumhubiri Kristo Mfufuka, ili mataifa yote yamtambue yeye anayeshibisha na anayetunza. Hata kwenye mateso na msalaba, tumkimbilie yeye, atushibishe na tufurahie ulinzi wake. Tunapoishi kwake Kristo na kuyasikiliza anayotueleza tunaishi maisha yaliyowajibika. Tumpende na kumtumikia Kristo kwa kuwa yeye ndiye chakula cha uzima.

SALA:Ee Yesu, uliye mkate wa uzima, uwajalie waamini kukutumainia. Lijalie Kanisa lako kuwa sauti yako, ili wanaoteseka na njaa ya Neno lako, wakujue.